Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Maseke:  Kukosa namba inaumiza ...Amtaja Dube, ishu ya kupanda ndege

MASEKE Pict

Muktasari:

  • Ndivyo kipa Wilbol Maseke anavyoanza kusimulia mapito yake katika soka tangu aanze kucheza soka la ushindani akitokea kikosi B cha Azam FC, kabla ya kupandishwa ya wakubwa na baadaye kujiunga na KMC na sasa Coastal Union.

“KILAmchezaji msimu unapoanza, anatamani awe anapata nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza ili kufanya makubwa ya kuisaidia timu. Inapotokea akakwama, inaumiza sana. Hata hivyo, hiyo siyo sababu ya kukata tamaa, inabidi kupambana zaidi.”

Ndivyo kipa Wilbol Maseke anavyoanza kusimulia mapito yake katika soka tangu aanze kucheza soka la ushindani akitokea kikosi B cha Azam FC, kabla ya kupandishwa ya wakubwa na baadaye kujiunga na KMC na sasa Coastal Union.

Kipa huyo aliyezaliwa Agosti, 8 2000 (umri wa miaka 25) Coastal inakuwa timu ya tatu kuichezea na anasimulia mengine ikiwamo urafiki wake na Prince Dube na kwa nini hapendi kupanda ndege huku akitaja sababu.

MASE 02

KUKOSA NAMBA KUNAVYOMUUMIZA

Kipa huyu ambaye alijiunga na Coastal Agosti 1, 2025, msimu huu hadi sasa anamiliki ‘Cleansheets’ tatu sawa na za msimu uliopita akiwa na KMC, analiambia Mwanaspoti, kila mwaka kwake unakuwa na malengo makubwa, hata hivyo, haijalishi yatatimia au la.

“Nimecheza mechi saba, nilitamani nicheze zaidi lakini hilo nalichukulia kama chachu ya kujituma kwa bidii kuhakikisha kiwango changu kinazidi kuwa juu.”

Pamoja na kutopata nafasi ya kucheza mara kwa mara, hilo halijazuia kuuona ni msimu mzuri wa ushindani na kila mchezaji anaonyesha kipaji chake na kiwango cha kuisaidia timu iliyomuajiri.

“Ugumu wa mechi iwe nyumbani ama ugenini, linatusaidia muda wote kujiweka fiti na kulinda kiwango, hilo linafanya Ligi Kuu Bara iwe bora zaidi,” anasema.

MASE 05

HAJAKATA TAMAA

Kuhusu kulidai soka anasema bado ana safari ndefu ya kusaka mafanikio kutokana na kazi hiyo, ingawa hadi sasa milango imefunguka jambo la muhimu zaidi kwake ni kucheza kama mchezaji wa kulipwa.

“Nalidai, naamini nitafanikiwa, kikubwa ni bidii na kutokukata tamaa,” anasema Maseke na kuongeza, katika timu tatu alizocheza kila moja imempa hatua katika maisha yake.

“Azam imenitambulisha hadi nikacheza KMC na sasa nipo Coastal ila nilichojifunza huku Tanga ni watu ambao wanaipenda timu yao kwa moyo mmoja, hilo linasaidia kuleta hamasa kwa mashabiki,” anasema.

Mechi aliyodaka dhidi ya Yanga akiwa na Coastal Union licha ya kufungwa bao 1-0 mfungaji akiwa Dube, lakini anaiona ni mechi bora kwake, kwani anakumbuka akiwa na KMC alivyofungwa mabao 5-0 na hapa anasema, “Nilicheza kwa kiwango cha juu, licha ya kuwahi kufungwa tano, lakini mimi siyo kipa mbovu.”


MASE 03 (1)

AMPA MWANAYE JINA LA DUBE

Kutokana na kukikubali kiwango cha mshambuliaji wa Yanga, Dube anayemiliki mabao manane msimu huu hadi sasa na uliopita alifunga 13, hata mwanaye aliamua kumpa jina la nyota huyo wa kimataifa wa Zimbabwe.

“Mtoto wangu ana miaka sita, nimempa majina ya Prince Dube Wilbol, kwani ni straika ninayemkubali muda wote tangu aanze kucheza ligi ya Tanzania, ana kipaji kikubwa na msumbufu uwanjani, inawezekana asikufunge yeye ila wengine wakiwa makini wanafunga kupitia yeye,” anasema na kuongeza;

“Dube ni rafiki yangu tangu tupo Azam na anafahamu kijana wangu nimempa majina yake, jambo lingine ninalolipenda kutoka kwake ni ana hofu ya Mungu na nidhamu ya hali ya juu.”

Anasema japokuwa kijana wake bado ni mdogo lakini anapenda kuchezea mipira na kufunga, lakini kama mzazi anamwelekeza zaidi katika elimu anayoamini itampa muongozo wa maisha yake: “Kuna wachezaji wengi wasomi, natamani akiwa mchezaji basi awe na elimu kubwa kichwani.”

Ukiachana na Dube mshambuliaji mwingine anayemkubali amemtaja Paul Peter wa Azam: “Kwa upande wa makipa ninaowaangalia kama mfano ni Ronwen Williams wa Mamelodi Sundowns na Ederson Moraes wa Manchester City najifunza mambo mengi ya kiufundi kutokana na wao.”

MASE 03

HAPENDI KUPANDA NDEGE

Wakati wengine wanaona fahari kutumia usafiri wa ndege ni tofauti kabisa kwa Maseke na anasimulia tukio moja la kushangaza.

Akiwa na Azam aliwahi kurudia uwanja wa ndege kisa? “Ilikuwa mwaka 2022 tulikuwa tunakwenda Arusha, sasa kulitokea matukio ya ndege kuanguka, nikamwambia kocha sipandi ndege akanibembeleza hadi nikakubali.”

Anaongeza: “Tukafika hadi uwanja wa ndege, tumepanda vizuri tu, wachezaji mara nyingi tunapenda kukaa siti za nyuma kabisa, nakumbuka ile ndege ilikuwa na abiria wa kizungu wasiozidi watano, mara tukaambiwa tufunge mikanda, tukafunga baada ya dakika kadha likatoka tangazo lingine kuna tatizo kidogo limetokea tutapandishwa ndege nyingine.”

“Matangazo ni ya Kiingereza nikasimama nikatoa begi langu, wachezaji wenzangu wakaanza kucheka na kuniona nimechanganyikiwa, nikawaambia ni kweli sijui sana Kiingereza ila nimeelewa, mara wazungu nao wakachukua mabegi yao na kuanza kushuka.

“Baada ya muda fulani wakasema tatizo ilikuwa mlango wamerekebisha tunatakiwa kuendelea na safari, mimi nikakataa, akaja meneja wa ndege kuniomba nikamkatalia, akaja kocha na meneja wa timu nikasimamia msimamo wangu, nikachwa na kurejea kambini, kila mtu alibaki ananitazama na kunishangaa, ila mimi kwenye kuyatetea maisha yangu sifanyi mzaha kabisa.”

Anasema ni zaidi ya mara 10 kazikataa safari za ndege akiwa na Azam, badala yake alikuwa anatumia usafiri wa basi.

“Kuna kipindi nilipanda basi peke yangu ilikuwa safari ya kwenda Kagera, nilifika miguu imevimba wachezaji wenzangu ambao walitumia muda mchache kufika wakaanza kunicheka na kuniambia wee jamaa una mambo ya ajabu, niwe wazi na mkweli mimi usafiri wa anga siuwezi,” anasema