Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ligi Kuu ya Wanawake Bara kuna vita nzito

WPL Pict

Muktasari:

  • Tofauti na misimu iliyopita ambako baadhi ya timu zilionekana kutawala mapema, safari hii mambo yanaonekana kuwa magumu zaidi, kuanzia kwa wanaowania ubingwa hadi wanaopigania kubaki.

MZUNGUKO wa kwanza wa Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania (WPL) umemalizika kwa kasi na takwimu zikionyesha ushindani mkubwa ndani na nje ya uwanja.

Tofauti na misimu iliyopita ambako baadhi ya timu zilionekana kutawala mapema, safari hii mambo yanaonekana kuwa magumu zaidi, kuanzia kwa wanaowania ubingwa hadi wanaopigania kubaki.

Mabao, hat-tricks, ushindani wa upachikaji mabao na presha ya pointi vyote vimechangia kuifanya ligi kuwa na ladha ya kipekee, ikizingatiwa msimu huu timu mbili zimeongezeka kutoka 10 hadi 12, jambo ambalo limeongeza ushindani.

Hadi mzunguko wa kwanza unatamatika, Simba Queens inaongoza ligi ikiwa na pointi 31, moja tu juu ya watani wao, Yanga Princess, wenye kwa pointi 30, na tofauti ya pointi 11 dhidi ya mpinzani wao wa miaka yote katika kuwania makombe, JKT Queens wenye pointi 20 katika nafasi ya tatu.

WP 01

MABAO 190

Hadi mzunguko wa kwanza unamalizika, jumla ya mabao 190 yamefungwa, huku takwimu zikiyoonyesha kuwa bado washambuliaji wana kazi ya kufanya kuongeza makali kwenye mzunguko wa pili.

Kwenye orodha hiyo, Yanga Princess ndiyo kinara wa kufumania nyavu ikifunga mabao 34, idadi inayoweka wazi uimara wao wa safu ya ushambuliaji.

Yanga Princess imezipita Simba Queens iliyofunga mabao 25 na JKT Queens yenye mabao 24, ikiwa imecheza mechi tisa. Hata hivyo, tofauti hiyo si kubwa sana, jambo linaloashiria kuwa ushindani bado uko wazi na lolote linaweza kutokea katika mzunguko wa pili.

Msimu uliopita hadi kufikia hatua kama hii, JKT Queens ilikuwa inaongoza kwa kufunga mabao 40, lakini safari hii imefunga 24 tu karibu nusu ya yale ya msimu uliopita.

Hii inaonyesha wazi kuwa ushindani umeongezeka na timu zimejipanga zaidi kukabiliana nao, hata hivyo safu za ushambuliaji hazijaonekana kuwa na makali kama ilivyokuwa awali.

Kwa upande wa timu zenye wakati mgumu, Bilo Queens ya Mwanza ndio yenye rekodi mbaya zaidi hadi sasa, ikiwa imefunga mabao mawili tu. Takwimu hiyo inafanana na rekodi mbaya iliyowekwa na Mlandizi Queens msimu uliopita, ambayo ilifunga mabao mawili tu hadi mzunguko wa kwanza na hatimaye kushuka daraja.

Hali hiyo inaweka presha kubwa kwa Bilo Queens kubadili gia katika mzunguko wa pili ili kuepuka hatma ya kushuka daraja.

WP 04

HAT-TRICK 6

Msimu huu umeonekana kuwa mgumu pia kwa washambuliaji kufunga mabao matatu katika mechi moja. Hadi sasa zimepatikana hat-trick sita tu kutoka kwa wachezaji wanne, tofauti na msimu uliopita ambapo zilifungwa 12 katika kipindi kama hiki.

Jeaninne Mukandayisenga wa Yanga Princess na Jentrix Shikangwa wa Simba Queens ndio wanaongoza kwa kufunga hat-trick mbili kila mmoja. Mbali na hilo, wawili hao pia wanaongoza katika orodha ya wafungaji bora.

Mukandayisenga ana mabao 15 na ndiye kinara wa ufungaji hadi sasa, huku Shikangwa akiwa amefunga mabao 10.

Wengine waliofunga hat-trick moja ni Veronica Mapunda wa Mashujaa Queens na Winifrida Gerald wa JKT Queens. Kwa Gerald, takwimu zinaonyesha kupungua kwa makali yake kwani msimu uliopita hadi sasa alikuwa tayari ameshafunga hat-trick tatu.

Msimu uliopita ulikuwa wa kipekee zaidi kwani Stumai Abdallah alifunga hat-trick nne peke yake, huku Shikangwa akifunga tatu. Wengine waliokuwa na moja kila mmoja ni Neema Paul, Asha Djafar, Ariet Adong, Milembe Ndalahwa na Annastazia Lucian.

Tofauti ya takwimu hizo na msimu huu inaonyesha wazi kuwa timu zimeboresha safu zao za ulinzi, hali inayowapa wakati mgumu washambuliaji kung'ara.

WP 02

JKT INA KAZI

Kwa upande wa JKT Queens, hali yao inahitaji umakini mkubwa katika mzunguko wa pili. Hadi sasa wamecheza mechi tisa, wameshinda sita, kutoa sare mbili na kupoteza moja dhidi ya Yanga Princess.

Matokeo hayo si mabaya, lakini hayatoshi kuwafanya wawe na uhakika wa kutetea ubingwa wao.

Msimu uliopita hadi mzunguko wa kwanza walikuwa hawajapoteza hata mechi moja, wakitoa sare mbili tu. Tofauti hiyo inaonyesha kupungua kwa ubora wao. Kipigo dhidi ya Yanga Princess sio tu kimepunguza kasi yao, bali pia kimewapa Simba Queens nafasi ya kuendelea kukaa kileleni.

Iwapo JKT hawataongeza kasi na kurejesha makali kwenye eneo la ushambuliaji, wanaweza kujikuta wakishuhudia ubingwa ukichukuliwa na Simba Queens au hata Yanga Princess ambao wanaonekana kuimarika kila mechi na ambao hwajawahi kutwaa taji hili. Presha kwa JKT ni kubwa, hasa ukizingatia wao ndio mabingwa watetezi.

WP 03

MBIO ZA UBINGWA

Kwa ujumla, mbio za ubingwa msimu huu zinaonekana kuwa wazi zaidi kuliko ilivyokuwa msimu uliopita. Simba Queens wanaonekana kuwa na uimara wa pointi, Yanga Princess wana makali ya mabao, huku JKT wakijaribu kurejea kwenye kiwango cha ubora.

Tofauti ya mabao na hat-trick inaonyesha ushindani wa kiufundi umeongezeka. Makocha wamejifunza kutoka misimu iliyopita na sasa wanajipanga zaidi kiulinzi. Hii ndiyo sababu hata timu zilizokuwa zikifungwa mabao mengi sasa zimepunguza idadi hiyo.

Mzunguko wa pili unatarajiwa kuwa na vita kali zaidi, hasa kwa timu zinazowania ubingwa na zile zinazopambana kuepuka kushuka daraja.

Maswali mengi yanabaki. Je, Simba Queens wataendeleza ubora wao? Yanga Princess wataendeleza moto wa mabao? Au JKT wataamka na kurejea kwenye makali yao ya msimu uliopita?