Kwa nini vita ya urais TFF

Rais wa TFF, Wallace Karia

Muktasari:

KILA wakati uchaguzi mkuu wa viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) unapofika, mjadala mkubwa, mizozo, kutofautiana kimtazamo, matusi, sifa na mambo mengine hujikita katika nafasi ya Rais wa chombo hicho kinachoongoza mchezo maarufu kuliko yote nchini.

KILA wakati uchaguzi mkuu wa viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) unapofika, mjadala mkubwa, mizozo, kutofautiana kimtazamo, matusi, sifa na mambo mengine hujikita katika nafasi ya Rais wa chombo hicho kinachoongoza mchezo maarufu kuliko yote nchini.

Nafasi za ujumbe wa Kamati ya Utendaji, ambazo sasa zimebakiwa sita tofauti na awali, huwa kama za kusindikizia uchaguzi wa Rais wa shirikisho.

Hivyo, magenge ya kampeni na mikakati hujigawa kutokana na wagombea wa nafasi ya urais, hasa kunapokuwa na wagombea wenye nguvu kubwa, hali ambayo inaonekana tofauti na ilivyo sasa baada ya wale wanaonekana kuwa wangeweka upinzani mkubwa kuenguliwa na masharti mapya ya kuwa na wadhamini watano ambao ni wanachama wa shirikisho.

Kwa maana nyingine, nafasi ya Rais wa TFF ndiyo kubwa inayoubeba mpira wa Tanzania, hivyo ni lazima asifiwe pale mambo yanapokwenda vizuri kiendeshaji au uwanjani na lazima pia awe tayari kupokea lawama pale mpira unapoyumba.

Mabadiliko ya Katiba ya TFF yaliyofanywa mwaka jana kwenye Ukumbi wa Benki Kuu (BoT) jijini Dar es Salaam yamemuongezea nguvu zaidi Rais wa shirikisho, tofauti na ilivyokuwa awali, hali inayofanya nafasi hiyo kuwa nyeti na kusababisha mijadala mikubwa kila kipindi cha uchaguzi.

Kwa mujibu wa toleo la 2020 la katiba, majukumu ya kimsingi ya Rais wa TFF ni kutekeleza maamuzi yaliyofanywa na Mkutano Mkuu na Kamati ya Utendaji kwa kutumia Sekretarieti.

Maana yake, mkutano mkuu utakapofanya maamuzi katika ajenda 18 zilizopo kikatiba, na baadaye kujadiliwa na kamati ya utendaji na kutoa maelekezo, Rais ndiye atakayeisamamia sekretarieti kutekeleza maamuzi hayo na yeye na kamati yake watawajibika kurudisha majibu kwa mkutano mkuu katika ajenda ya yatokanayo na mkutano uliopita au taarifa ya utekelezaji.

Kwa mujibu wa ibara ya 42 (b), Rais wa TFF pia ana jukumu la kuhakikisha vyombo vya shirikisho hilo vinafanya kazi kwa ufanisi ili vifanikishe malengo yaliyoelekezwa katika katiba. Hapa haimaanishi kuingilia utendaji wa kamati ndogo au kamati za maamuzi na uchaguzi.

Rais hapa anatakiwa ahakikishe vyombo hivyo vinafanya mikutano yake kama inavyotakiwa na kupewa ushirikiano stahiki na sekretarieti. Kamati hizo ni kama ile ya fedha, ya katiba, sheria na hadhi za wachezaji, Bodi ya Ligi, na kamati huru ambazo ni ya uchaguzi, maadili na nidhamu pamoja na zile za rufaa.

Rais wa TFF pia ndiye msimamizi wa sekretarieti, kwa maana anatakiwa ajue chombo hicho kinafanyaje kazi katika uendeshaji wa shughuli za kila siku, kuhakikisha idara zake zinafanya kazi kama inavyotakiwa na kuchukua hatua pale inapotakiwa.

Hapa maana yake ni kwamba iwapo mdau anaona tatizo lake halishughulikiwa kikamilifu na sekretarieti, ambayo iko chini ya Katibu Mkuu, anaweza kuwasiliana na Rais kutoa malalamiko yake.

Mfano mchezaji ambaye anataka barua ya uthibitisho kutoka nje ya nchi kuwa, hana mkataba na klabu nyingine na amefuatilia kwa Mkurugenzi wa Ufundi na Katibu Mkuu bila ya mafanikio, ana uwezo wa kumfuata Rais na kumweleza ili alichukue suala hilo na kulifanyia kazi.

Hapa kama rais atakuwa hachukui hatua, maana yake imani kwake itapotea na malimbikizo ya matatizo yataongezeka na mwishoni ni wachezaji wachache sana watakaokuwa wanapenya kwenda nje kwa sababu ya tatizo la kutokuwa na usikivu na kuchukua hatua.

Ibara hiyo pia inampa rais mamlaka ya kuongoza mauhusiano baina ya TFF na wanachama wake pamoja na vyombo vingine vya kimataifa kama Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa), Shirikisho la Soka Afrika (CAF) na Baraza la Soka la Afrika Mashariki na Kati (Cecafa).

Mamlaka haya ndiyo yanamfanya rais wa shirikisho atumie muda mwingi nje ya nchi akihudhuria vikao vya mashirikisho hayo. Vikao hivyo ni mikutano mikuu, mikutano ya vikao vya kamati za mashirikisho hayo kuanzia kamati za utendaji kama akichaguliwa na nyingine ndogondogo.

Hizi nafasi pia ndizo humtamanisha Rais kugombea urais kama wa Cecafa, CAF na Fifa au kuingia katika Kamati za Utendaji za mashirikisho hayo. Leodegar Tenga, Rais wa zamani wa TFF, alikuwa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya CAF na kamati mbalimbali za shirikisho hilo pamoja na Fifa. Said El Maamry, Mwenyekiti wa zamani wa FAT, alikuwa Mtanzania wa kwanza kuwa Mjumbe wa kamati hiyo na pia alipewa ujumbe wa heshima.

Wallace Karia, Rais wa sasa wa TFF, ni Mwenyekiti wa Cecafa na alitaka kugombea ujumbe wa Kamati ya Utendaji ya CAF.

Na bila shaka, kashfa za wagombea urais wa mashirikisho hayo kurubuni wapigakura haziwezi kumkwepa rais kama nchi inatajwa kuhusika.

Katiba mpya pia inampa rais mamlaka ya kumteua Makamu wa Kwanza wa Rais, tofauti na ilivyokuwa awali wakati anayeshika nafasi hiyo alikuwa akigombea sambamba na rais. Utaratibu huu wa Rais kumteua Makamu wa Kwanza na baadaye kuthibitishwa na mkutano mkuu umekuwa ukitumiwa na mashirikisho mengi kutokana na ule wa zamani wakati mwingine kuibua kambi mbili na kusababisha migogoro katika uendeshaji mpira.

Lakini Makamu ni lazima awe Mjumbe wa Kamati ya Utendaji. Makamu wa Kwanza wa sasa ni Athuman Nyamlani, ambaye aliteuliwa kuwa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji na baadaye kuteuliwa kuwa Makamu wa Rais kabla ya kuteuliwa tena baada ya marekebisho ya katiba na kuthibitishwa na mkutano mkuu uliofanyika BoT mwaka jana.

Marekebisho ya katiba ya TFF pia yanampa rais mamlaka ya kupendekeza jina la Katibu Mkuu wa Shirikisho hilo kwa Kamati ya Utendaji, tofauti na awali wakati jukumu hilo lilikuwa la kamati hiyo ambayo wakati fulani ilikaimisha kazi hiyo kwa kampuni binafsi baada ya kutangaza nafasi hiyo kwenye vyombo vya habari.

Mwandishi wa Makala hii ni mmoja wa walioajiriwa katika nafasi hiyo kwa TFF kutumia mfumo wa kuajiri kwa kutumia kampuni binafsi, ambayo inapokea maombi, kuyachambua, kusaili wanaoomba kazi hiyo na baadaye kupeleka majina matatu kwa Kamati ya Utendaji, ambayo inawahoji wote na baadaye kutangaza jina la mmoja anayefaa. Rais pia ndiye anayependekeza kutimuliwa kwa katibu huyo.

Kazi nyingine ya rais ni kuendesha mkutano mkuu na vikao vya kamati ya utendaji, ambavyo kikatiba vinatakiwa viwe sita, na pia atakuwa na kura ya kawaida katika vikao vya kamati ya utendaji na ya ziada ya kufanya maamuzi katika vikao vya kamati ya dharura.

Rais anaweza kuitisha Kamati ya Dharura katika kipindi ambacho ni nje ya vikao vile sita. Kamati hiyo itamhusisha rais, makamu wake wawili na wajumbe wawili wa kamati ya utendaji. Iwapo itakuwa vigumu kwao kukutana, kikao kinaweza kufanywa kwa njia nyingine za mawasiliano.

Hili limeingizwa, kwa maoni yangu, baada ya janga la virusi vya corona ambalo lilisababisha mikusanyiko kupigwa marufuku na hivyo taasisi nyingi kuendesha vikao vyao kwa njia ya programu tumishi ya Zoom ambayo inawezesha watu kuongea wakiwa wanaonana licha ya kuwa sehemu tofauti.

Mwaka 2012, TFF ilifanya uamuzi kwa njia ya barua—circular resolution—kwa ajili ya kuingiza kamati ya rufaa ya uchaguzi na suala la leseni za klabu. Uamuzi huo ulipingwa vikali na baadhi ya wadau, wengi wao wakionekana kutaka kutumia mkusanyiko kwa shughuli za siasa za uchaguzi. Maamuzi hayo yalipitishwa baadaye na mkutano mkuu.

Rais pia ana mamlaka ya kuteua wajumbe wanne wa kamati ya utendaji, mmoja wao lazima awe mwanamke.

Hapa ndipo nguvu ya rais inapokuwa kubwa zaidi katika kamati ya utendaji kwa kuwa anakuwa na watu wengi ambao hawawezi kutofautiana naye.

Kesho tutakuwa na mwendelezo wa mfululizo wa makala hizi za kuelimisha kuhusu uchaguzi mkuu wa TFF.

Mwandishi wa safu hii alikuwa Katibu Mkuu wa TFF