Kofia inavyoweza kubamba kwenye mtoko wako
Muktasari:
- Kwa wanaopenda matembezi ya mwisho wa wiki, kofia inaweza kuwa nyongeza inayobadilisha kabisa muonekano. Inapendeza zaidi unapojua fulana gani uvae, suruali ipi ichanganye nayo, viatu gani vikamilishe mavazi na ni nguo zipi unapaswa kuziepuka ili usionekane umechanganya mitindo isiyohusiana.
UNAWEZA kuvaa nguo za kawaida kabisa, lakini ukiongeza kofia inayolingana na mavazi yako, watu wakaanza kukuona umejipanga kisawasawa. Vilevile, unaweza kuvaa nguo za bei kubwa, lakini ukazichanganya vibaya na kofia na kuharibu kila kitu. Ndiyo maana katika ulimwengu wa mitindo, si suala la kuvaa tu, bali ni kujua nini kinaendana na nini.
Kwa wanaopenda matembezi ya mwisho wa wiki, kofia inaweza kuwa nyongeza inayobadilisha kabisa muonekano. Inapendeza zaidi unapojua fulana gani uvae, suruali ipi ichanganye nayo, viatu gani vikamilishe mavazi na ni nguo zipi unapaswa kuziepuka ili usionekane umechanganya mitindo isiyohusiana.
FULANA NA SURUALI ZA JEANS
Huu ni mchanganyiko rahisi ambao unaweza kukupa muonekano wa kuvutia bila kutumia fedha nyingi. Fulana nyeupe, nyeusi au ya rangi moja ikiunganishwa na suruali ya jeans ya bluu au nyeusi, viatu vya michezo na kofia, inaweza kukufanya uonekane nadhifu kwenye matembezi.
Unaweza kuongeza miwani ya jua ili kukamilisha muonekano huo. Muhimu ni kuhakikisha rangi za fulana, suruali na kofia hazigongani. Kwa mfano, fulana nyeupe, suruali nyeusi na viatu vyeupe vinaweza kuendana vizuri na kofia nyeusi.
KAPTULA NA FULANA ZISIZOBANA
Kama unapanga kwenda sehemu ya starehe, ufukweni au matembezi ya mchana, kaptula inaweza kuwa chaguo zuri. Ichanganye na fulana isiyobana sana, viatu kama raba au vya wazi na kofia.
Muunganiko huu unakupa mwonekano unaovutia na wa kisasa. Unaweza kuchagua kaptula ya kaki na fulana nyeupe, kisha kuongeza kofia yenye rangi iliyotulia sana.
SHATI LA MIKONO MIFUPI NA SURUALI YA KITAMBAA
Kwa mtu anayetaka kuonekana nadhifu zaidi bila kuvaa suti, shati la mikono mifupi linaweza kufanya kazi vizuri. Lichanganye na suruali ya kitambaa au suruali ya kadeti, viatu safi na kofia inayolingana na rangi za mavazi.
Kwa mfano, shati la bluu nyepesi, suruali ya kaki na viatu vya kahawia vinaweza kutoa muonekano mzuri wa matembezi ya mchana. Kofia ya rangi tulivu kama nyeupe inaweza kukamilisha mavazi hayo bila kung'aa kupita kiasi.
JEANS PANA NA FULANA KUBWA
Kwa vijana wanaopenda mitindo ya kisasa ya mitaani, suruali pana za jinsi na fulana kubwa ni mchanganyiko unaoweza kubamba sana. Ukiunganisha mavazi hayo na viatu vya michezo pamoja na kofia, unapata muonekano wenye mvuto wa vijana.
Unaweza kuvaa fulana nyeusi, suruali pana ya bluu na viatu vyeupe. Kofia inayokamilisha rangi hizo itafanya muonekano uwe na mpangilio.
JAKETI, FULANA NA VIATU VYA MICHEZO
Jacket nyepesi inaweza kuongeza mvuto kwenye mavazi ya kawaida. Ukiivaa juu ya fulana, ukaichanganya na suruali ya jinsi na viatu vya michezo, kofia inaweza kuwa nyongeza inayokamilisha mtoko wako.
Kwa mfano, jacket ya jeans, fulana nyeupe na suruali nyeusi vinaweza kuendana vizuri na viatu vyeupe. Huu ni muonekano unaoweza kutumika kwenye matembezi ya jioni au kukutana na marafiki.
NGUO ZA KUEPUKA KUCHANGANYA NA KOFIA
Si kila vazi linapendeza likivaliwa pamoja na kofia. Suti, shati la ofisini, tai na viatu rasmi vya ngozi mara nyingi havihitaji kuongezewa kofia za kawaida za kimatembezi. Mchanganyiko huo unaweza kuondoa ule muonekano wa kistaarabu unaotakiwa na mavazi rasmi.
Pia, nguo zenye michoro mingi, maandishi makubwa na rangi zinazoshindana zinaweza kufanya kofia isipate nafasi ya kukamilisha muonekano. Kama fulana ina maandishi makubwa, ni vizuri kuchagua suruali na viatu visivyo na mapambo mengi.
USHAURI
Kabla ya kutoka, usiishie kuangalia kama nguo zako ni nzuri kila moja peke yake. Jiulize kama zinaendana zinapovaliwa pamoja. Kofia inapaswa kuwa sehemu ya mavazi yako, si kitu kinachoonekana kama umeongeza kwa sababu tu unataka kufunika kichwa.