Prime
Kariakoo yasubiri makombora ya Toure na Doumbia
Muktasari:
- Yanga ambao ni mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya NBC, imetambulisha wachezaji wapya tisa, huku nyota anayesubiriwa zaidi na mashabiki ni mshambuliaji mwenye uraia wa nchi za Senegal na Ufaransa, Cheikh Ibrahima Toure.
VIGOGO wa soka nchini, Yanga na Simba zinaendelea kutunishiana misuli kwa ajili ya msimu ujao wa 2026-2027, kutokana na usajili uliofanyika hadi sasa, hususani katika maboresho ya eneo la ushambuliaji.
Yanga ambao ni mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya NBC, imetambulisha wachezaji wapya tisa, huku nyota anayesubiriwa zaidi na mashabiki ni mshambuliaji mwenye uraia wa nchi za Senegal na Ufaransa, Cheikh Ibrahima Toure.
Nyota huyo aliyejiunga na Yanga akiwa mchezaji huru baada ya kuachana na Al-Jabalain FC ya Saudi Arabia, msimu wa 2025-2026, alionyesha kiwango kizuri na kikosi hicho, kufuatia kuhusika na mabao 25, akifunga 20 na kuasisti mengine matano.
Yanga imeamua kuimarisha eneo hilo muhimu la ushambuliaji kwa ajili ya kuongeza ushindani msimu wa 2026-2027, baada ya aliyekuwa mshambuliaji, Prince Dube aliyefunga mabao 10 ya Ligi Kuu msimu uliopita, kujiunga na Hardrock FC ya kwao Zimbabwe.
Sababu za mabosi wa Yanga kuongeza mshambuliaji wa kimataifa, ni kutokana na kutoridhishwa na kasi katika eneo hilo na msimu wa 2025-2026, kiungo, Allan Okello alimaliza akiwa ndiye kinara wa ufungaji kikosini hapo akifunga mabao 14.
Nyota mwingine wa Yanga atakayeangaliwa zaidi ni kiungo mshambuliaji, Albert Kangwanda aliyejiunga na timu hiyo akitokea Red Arrows FC ya kwao Zambia, ambaye kwa msimu wa 2025-2026, alikuwa ni mchezaji bora wa msimu wa Ligi ya Zambia (MVP).
Katika Ligi Kuu ya Zambia msimu wa 2025–2026, Kangwanda alionyesha kiwango kizuri akiwa na Red Arrows FC kwa kufunga mabao 13, huku mashindano yote akihusika na mabao 25, kufuatia kufunga 17 na kuasisti manane.
Licha ya kiwango bora kwa Kangwanda, ila anapaswa kufanya vizuri Yanga, kwani mshambuliaji wa mwisho wa Zambia kuchezea kikosi hicho alikuwa ni Kennedy Musonda aliyeondoka Julai 7, 2025 na kujiunga na Hapoel Ramat Gan Givatayim ya Israeli.
Musonda anayeichezea kwa sasa Hapoel Nof HaGalil FC ya Israeli, alijiunga na Yanga, Januari 13, 2023, baada ya kuachana na Power Dynamos ya kwao Zambia, ambapo msimu wa 2024-2025, alifunga mabao matatu tu ya Ligi Kuu Bara.
Katika kipindi chote cha misimu miwili alichokaa Yanga, Musonda alifunga mabao 10 ya Ligi Kuu, baada ya msimu wa 2022-2023 kufunga mawili, kisha 2023-2024 akafunga matano na 2024-2025 alifunga matatu.
Hata hivyo, rekodi hizo za Musonda zilimfanya mshambuliaji huyo kushindwa kuwika na Yanga na sasa Kangwanda anatakiwa kupambana ili kutoa jinamizi hilo.
Ms hambuliaji mw ingine wa Yanga anayesubiriwa kwa hamu ni Housseine Zakouani aliyezaliwa Marseille, Ufaransa mwenye uraia wa Comoros aliyejiunga na kikosi hicho cha mi taa ya Twiga na Jangwani, baada ya kuondoka Al-Zulfi SFC ya Saudi Arabia.
Toure, Kangwanda na Zakouani ni miongoni mwa wachezaji watatu wa kigeni waliotambulishwa na Yanga dirisha hili la msimu wa 2026-2027, wakiungana na viungo washambuliaji, Juma Issa Abushiri aliyetoka Fountain Gate na Erick Mwijage kutoka KMC.
Wengine ni beki wa kulia, Abdulnasir Assa ‘Gamal’, beki wa kati, Mohamed Mussa, mshambuliaji, Hussein Juma Mihambo wote wakisajiliwa kutokea Mashujaa, sambamba na kiungo mshambuliaji, Suleiman Mbarouk ‘Mpemba D’ akitokea JKU FC ya Zanzibar.
Kwa upande wa watani zao wa jadi Simba, imefanya maboresho mbalimbali kwa ajili ya kuongezea nguvu kwa msimu wa 2026-2027, ambapo mabingwa hao watetezi wa Kombe la CRDB kwa msimu wa 2025-2026, wamemsajili mfungaji bora wa Ligi ya Mali.
Msh ambuliaji huyo ni Ibrahim Doumbia raia wa Mali aliyeshinda Tuzo ya Mfungaji Bora wa Ligi Kuu ya Mali msimu wa 2025-2026, baada ya kufunga mabao 17, katika mechi 24 na kuasisti pia matano, japo alihusika na mabao 21 ya mashindano yote.
Simba imefanya maboresho eneo hilo baada ya kuondoka kwa Mghana, Jonathan Sowah aliyerejea Singida Black Stars na licha ya kutabiriwa kufanya makubwa kwa msimu wa 2025-2026, ila nyota huyo alishindwa kuwika na kurejea timu aliyotoka.
Ujio wa Doumbia unaongeza nguvu katika eneo la ushambuliaji ambalo kwa msimu wa 2025-2026, lilikuwa linamtegemea zaidi mshambuliaji Seleman Mwalimu ‘Gomez’ aliyejiunga na kikosi hicho kwa mkopo akitokea Wydad Casablanca ya Morocco.
Mwalimu atakayeendelea kuichezea Simba kwa mkopo wa msimu wa 2026-2027, ndiye aliyemaliza kinara wa ufungaji katika kikosi hicho kwa msimu wa 2025-2026, baada ya kufunga mabao tisa ya Ligi Kuu, huku Kombe la CRDB akifunga mabao matatu.
Nyota wengine wa kimataifa walioongezwa katika kikosi hicho ni viungo Keletso Makgalwa aliyetokea Sekhukhune United ya kwao Afrika Kusini na Mnigeria, Ibraheem Jabaar aliyetokea Stellenbosch pia ya Afrika Kusini. Kwa wazawa, kuna kiungo mshambuliaji Bakari Msimu ambaye kwa msimu wa 2025-2026, akiwa na Coastal Union aliifungia mabao matatu ya Ligi Kuu, akienda kuongeza ushindani zaidi kutokana na kiwango chake bora.
Pia kuna beki wa kulia, Nathaniel Chilambo ambaye ameachana na Azam FC, akitazamiwa kuongeza pia ushindani katika nafasi hiyo anayocheza mchezaji mwenzake nyota, Shomari Kapombe.
Mchezaji mwingine ni kiungo mkabaji, Kelvin Nashon aliyejiunga na timu hiyo akitokea Pamba Jiji ya jijini, Mwanza, japo licha ya maboresho hayo kwa Yanga na Simba ila eneo linaloangaliwa zaidi ni la ushambuliaji kwa klabu hizo zote mbili, hivyo kutakuwa na vita ambao inasubiri kuamuliwa na Toure au Doumbia.