Kagame 2024: Mwisho wa ubishi, ni APR au Red Arrows!
Muktasari:
- Fainali hiyo inayopigwa leo kuanzia saa 9:00 alasiri inazikutanisha APR ya Rwanda inayaosaka taji la nne la michuano hiyo dhidi ya waalikwa kutoka Zambia, Red Arrows.
FAINALI za 47 za michuano ya Klabu Bingwa kwa Nchi za Afrika Mashariki na Kati, maarufu kama Kombe la Kagame 2024 inafikia tamati leo Jumapili.
Fainali hiyo inayopigwa leo kuanzia saa 9:00 alasiri inazikutanisha APR ya Rwanda inayaosaka taji la nne la michuano hiyo dhidi ya waalikwa kutoka Zambia, Red Arrows.
Timu hizo zimefuzu hatua hiyo baada ya kushinda mechi za nusu fainali, APR ikiizima Al Hilal ya Sudan kwa penalti 5-4 baada ya dakika 120 kumalizika bila ya bao lolote, huku Wazambia wakitumia dakika 30 za nyongeza kuwafumua Al Wadi pia ya Sudan kwa mabao 2-0.
Hii itakuwa ni fainali za tisa kwa Wanyarwanda, inayosaka taji la nne la michuano hiyo iliyopewa jina la Kagame Cup kuanzia mwaka 2002 baada ya Rais wa Rwanda, Paul Kagame kujitosa kuidhamini.
APR ilishacheza awali fainali nane tofauti, tatu ikifanikiwa kutwaa ubingwa mwaka 2004, 2007 na 2010, huku ikipoteza nyingine tano za mwaka 1996, 2000, 2005, 2023 na 2014.
Kwa Maafande wa Red Arrows kutoka Zambia walioshiriki kama timu mwalikwa, hizi ni fainali za kwanza za michuano hiyo ya Kagame, na ilipenya hatua ya nusu fainali ikiwa kama mshindwa bora (best looser) kutokea Kundi B.
Red Arrows ilimaliza nafasi ya pili kwa kuvuna pointi sita katika mechi tatu, nyuma ya vinara Al Hilal iliyomaliza na pointi tisa ikiwa timu pekee iliyoshinda mechi zote tatu za makundi ya michuano hiyo iliyoanza
Julai 9 ikishirikisha timu 12 na kuchezwa kwenye viwanja viwili vya KMC uliopo Mwenge na Azam Complex, Chamazi vyote vya jijini Dar es Salaam.
Timu hiyo ni ya kwanza kutoka Zambia kufika fainali za michuano ya Kagame, lakini inakuwa ni ya nne kutoka Ukanda wa Soka wa Kusini mwa Afrika (Cosafa) baada ya Rio Tinto ya Zimbabwe iliyocherzwa fainali za mwaka 1982 na kupoteza mbele ya AFC Leopards ya Kenya.
Klabu ya pili kucheza fainali hizo ilikuwa ni ADMARC Tigers ya Malawi iliyopoteza 2-1 kwa AFC Leopards mwaka 1983 na Big Bullets pia ya Malawi ilikuwa timu ya mwisho kucheza hatua hiyo mwaka 2021 na kulala bao 1-0 mbele ya Express ya Uganda.
Kama itaendeleza kucheza soka ililolionyesha tangu mwanzo wa michuano ya mwaka huu kisha kubeba ubingwa, itakuwa ni timu ya kwanza ya Cosafa kutwaa ubingwa wa Kagame, kwani tangu michuano ilipoasisiwa mwaka 1967 ilikuwa haijawahi kutokea.
MZUKA KIDOGO, ILA FRESHI
Licha ya kwamba kukosekana kwa klabu wenyeji na wazoefu wa michuano hiyo, Simba, Yanga na Azam kumeifanya Kagame Cup 2024 kutokuwa na msisimko mkubwa, lakini boli limepigwa na mashabiki waliohudhuria mechi kuanzia zile za makundi hadi nusu fainali wamepata burudani.
Licha ya wenyeji Singida Black Stars, Coastal Union na JKU kushindwa kufurukuta na kutolewa hatua ya makundi, bado mashabiki waliendelea kuifuatilia michuano hiyo kutokana na kuvutiwa na soka lililopigwa.
Timu zote nne zilizokuwa zimetinga nusu fainali zilionyesha soka tamu kwelikweli na la ushindani, huku Wasudan wakitawala kwa kiasi kikubwa, licha ya kwanza timu zao zote zimetolewa kwenye hatua hiyo kwa maana ya Al Wadi na Al Hilal.
Katika mechi za makundi timu hizo hazikupoteza kama ilivyokuwa kwa APR, huku Red Arrows ikipoteza moja.
Al Wadi ilianza michuano kwa kuinyoa JKU ya Zanzibar kwa bao 1-0, kisha kuifunga Dekadaha ya Somalia kwa mabao 2-1 na kumalizia na sare ya 1-1 na Wagosi wa Kaya, Coastal Union iliyowahi kufika fainali za michuano hiyo mwaka 1989 na kupoteza mbele ya Kenya Breweries (sasa Tusker Kenya) kwa mabao 3-0.
Wababe hao walimaliza kama vinara wa Kundi A kwa kukusanya pointi saba na kupangwa kukutana na Red Arrows iliyoshika nafasi ya pili katika Kundi B ikianza na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Gor Mahia ya Kenya, kabla ya kufumuliwa mabao 5-0 na Al Hilal na kushinda mechi ya mwisho kwa bao 1-0 mbele ya ASAS ya Djibouti.
Kwa upande wa Al Hilal ilianza mechi za kundi hilo la B kwa kuichapa Asas kwa mabao 2-0, kisha kuizima Red Arrows kwa mabao 5-0 na kuinyoosha Gor Mahia kwa mabao 2-0 na kumaliza kama vinara wa kundi kwa pointi tisa na mabao tisa huku wavu wake ukiwa haukuguswa kabisa.
Ndipo ikakutana na APR katika nusu fainali na kuendelea kuonyesha ina ukuta wa chuma usiogusika kwa kucheza dakika 120 bila kufungana kabla ya kung'olewa kwa penalti 5-4.
Wababe wao, yaani APR yenyewe ilitakata katika Kundi C kwa kuanza michuano kwa ushindi bao 1-0 dhidi ya Singida Black Stars ya Tanzania, kisha kuichapa Al Merrikh ya Sudan Kusini pia kwa bao 1-0 na kumalizia na sare ya 1-1 dhidi ya SC Villa ya Uganda.
MWENDO WA NOTI
Kabla ya kupigwa kwa mchezo wa fainali ya michuano hiyo, mapema saa 6:00 mchanai, timu za Al Hilal na Al Wadi zitavaana katika mechi ya mshindi wa tatu ambaye atavuna zawadi ya Dola 10,000 (zaidi ya Sh 26 Milioni).
Tangu Rais Kagame aanze kuidhamini michuano hiyo, amekuwa akiweka zawadi ya Dola 60,000 ( zaidi ya Sh 159 Milioni) ambapo bingwa huvuna Dola 30,000 (karibu Sh 80 milioni), huku inayomaliza ya pili inabeba Dola 20,000 (zaidi ya Sh 53 Milioni).
Mbali na udhamini wa Kagame, michuano ya msimu huu imepigwa tafu pia na Chama cha Soka cha Sudan (SFA), Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Azam TV na City College Of Health ambayo imekuwa ikitoa zawadi wa wachezaji bora wa kila mechi (man of the match) tangu hatua ya makundi.
Hivyo, pamoja na kwamba klabu hizo zinachuana kuacha alama katika michuano hiyo, lakini zitakuwa zikipigia hesabu fedha za zawadi za udhamini sambamba na ubingwa.
MCHANA NYAVU
Wakati michuano ikifikia tamati leo, kuna nafasi kubwa kwa nyota wa Al Hilal, Mohammed Abdelrahman kumaliza kama kinara wa mabao kwani hadi sasa ndiye anayeongoza orodha akiwa na mabao matano.
Nyota huyo anayekumbukwa na mashabiki wa Yanga kwa namna alivyowakatili katika michuano ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika 2022-2023 kwa kuifunga nje ndani na kuifanya iangukie kwenye Kombe la Shirikisho na kufanikiwa kutinga fainali dhidi ya waliotwaa ubinhwa, USM Alger ya Algeria alifunga mabao hayo katika mechi tatu mfululizo za makundi, kabla ya juzi kutibuliwa na APR.
Abdelrahman anafuatiwa kwa karibu na Adama Coulibaly pia wa Al Hilal, mchezaji pekee aliyefunga hat trick katika michuano ya mwaka huu akiwa na mabao matatu, huku kukiwa na msururu wa orodha wa waliofunga bao moja moja wakiwamo Allasane Diarra na Paul Katema wa Red Arrows walioivusha timu hiyo katika mchezo huo wa fainali ya leo alasiri.
Ingawa soka huwa na maajabu yake, lakini bado Msudan ana nafasi zaidi ya kuongeza idadi ya mabao kupitia mechi ya mshindi wa tatu, huku waliopo nyuma yake wakiwa na kazi kubwa ya kufunga mabao mengi zaidi ili wampiku katika mbio za kubeba tuzo ya mfungaji bora wa msimu huu.
Katika fainali za mwisho za Kagame 2021, wachezaji watatu akiwamo Paul Peter wa Azam FC, Muzamiru Mutyaba na Erick Kambale wote wa Express ndio walioibuka wafungaji bora msimu huo, kila mmoja akifunga mabao matatu.
APR NA VINARA WA MATAJI
Ushindi kwa APR utaifanya timu hiyo kujisogeza kwenye orodha wa vinara wa kubeba mataji mengi ya michuano hiyo kwani itafikisha taji la nne na kushika nafasi ya tatu kwa zilizotwaa ubingwa huo mara nyingi nyuma ya vinara Simba na AFC Leopards ya Kenya zilizobeba mara sita kila moja.
APR imetwaa mataji mwaka 2004, 2007 na 2010, ikilingana na timu za Sudan Al Merrikh ya Sudan na SC Villa ya Uganda, huku vinara Simba ilitwaa taji mwaka 1974, 1991, 1992, 1995, 1996 na 2002, wakati AFC Leopards, ilitwaa mara mbili ikitumia jina la Abaluhya mwaka 1967 na 1979 kisha kuendelea ikiwa na jina la sasa 1982, 1983, 1984 ikiwa timu pekee iliyotwaa mara tatu mfululizo kabla ya kubeba mara ya mwisho 1997.
Kwa Yanga ilibeba taji la michuano hiyo mwaka 1975, 1993, 1999, 2011 na 2012, huku Gor Mahia ilianza kubeba ikifahamika kama Luo Union 1976 na 1977 kisha ikiwa na jina la sasa ikarudia tena 1980, 1981 na 1985, wakati Tusker ilibeba 1988, 1989, 2000, 2001 na 2008.
Hivyo mashabiki wa soka wanaoifuatilia michuano hiyo wana kiu ya kutaka kujua ni APR itaongeza mataji au Red Arrows itaandika historia ya kuwa timu ya kwanza nje ya Cecafa kubeba taji hilo la Kagame na katika tuzo binafsi, mchezaji gani atampiku Abdelrahman katika Mfungaji Bora mbali na zile za kipa bora, Mchezaji Bora wa michuano na timu yenye nidhamu? Tusubiri tuone!
02 Mataji iliyotwaa Azam FC katika michuano hii ikifanya hivyo mwaka 2015 na 2018.
2002 Ndio mwaka wa mwisho kwa Simba mmoja wa vinara wa Kagame kubeba ubingwa wa michuano hiyo
1990 Mwaka ambao michuano hii ilishindwa kufanyika tangu 1974 kwa kukosekana muandaaji wake.