Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Joshua: Yanga imenipa maisha Dar es Salaam

JOSHUA Pict

Muktasari:

  • Joshua anasema kuna maproo wengi wa kigeni ambao walifanya vizuri kipindi anacheza na sasa,  lakini hajawahi kuona vipaji vya aina yake kama walivyonavyo Clatous Chama na Haruna Niyonzima wote wawili waliwahi kuichezea Simba na Yanga.

KAMA kuna kitu alikijenga mapema na kimemsaidia beki wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, Oscar Joshua ni uchaguzi wa marafiki wanaomzunguka ambao ni wapambanaji na wanawaza kufanya vitu vikubwa zaidi, jambo linalompa hamasa ya kujituma.

Katika mahojiano na Mwanaspoti, Joshua anasema ingawa jambo la kwanza kwenye maisha yake ni Mungu, lakini marafiki wakiwa wazuri ni rahisi kufanikiwa na wakiwa wabaya wanakuwa chanzo cha anguko.

“Kufeli kupo mtu yeyote asione aibu kuanza upya, lakini ni jambo la msingi sana kuwa na marafiki wanaojitambua, ambao mnaweza mkawa mnashauriana vitu vya msingi au ukiwa unakosea wanakuambia hapa unafanya sivyo,” anasema Joshua na kuongeza:

JOSH 03

“Nilijua kuna maisha baada ya ustaa, jambo la msingi nilijua kuendana na bajeti tofauti na unapocheza unajua kuna mshahara na posho, sasa ukiwa nyumbani lazima ujue kipi unapaswa kuachana nacho na kukifanya kwa bidii, kitu ambacho kimekuwa kigumu kwa wachezaji wengi kuendana nacho.

“Kitu kingine lazima kukubaliana na hali halisi, kama ulikuwa staa kiasi gani ukiona uchumi unayumba uza hata genge, ili mradi kujipatia kipato, kuliko kuombaomba kwa viongozi ambao hawawezi kukupa kila siku, mfano wachezaji ambao wanacheza kwa sasa watengeneze koneksheni ya watu, ambao watakuwa msaada kwao kwa baadaye.”


JOSH 01

JASHO LAKE LA UWANJANI

Anasema maisha anayoishi kwa sasa, uwekezaji wa biashara zake, koneksheni za watu, familia na mji wake vimetokana na mpira wa miguu, anaokiri umemlipa na anaendelea kula matunda yake kwa njia nyingine.

Kwa sasa anafanya biashara ya vifaa vya michezo,  duka lake lipo Tegeta Kibo na anajiendeleza kusomea baadhi ya kozi ili kuhakikisha anazifanya kwa ubora na ngazi ya kimataifa.

“Biashara zangu zinafahamika kwa jina la VADASA  ina maana V ni  kuleta thamani kwa wateja washirika jamii, A ni kuongeza thamani kwenye bidhaa na huduma, D ni usambazaji wa bidhaa huduma kwa ufanisi, A ni maendeleo ukuaji na kupanua fursa za biashara na SA ni ushirikiano wa kimkakati na washirika wa biashara,” anasema Joshua na kuongeza:

“Nilisoma kozi na bado naendelea kusoma, lengo ni kupanua uelewa wa  kuhakikisha nafanya biashara zangu kwa upana, dunia ya sasa ni ya sayansi na teknolojia, ili biashara uweze kuzifanya kwa ukubwa lazima kujifunza baadhi ya mambo ya msingi.”

Kutokana na mafanikio hayo anakiri yametokana na kucheza Yanga kwa misimu saba, baada ya kujiunga nayo 2010/11 na alistaafu 2017/18.

“Maisha yangu yote ya Dar es Salaam yametokana na Yanga, kila nikiamka asubuhi jambo la kwanza Mungu kitu cha pili Yanga, hivyo vyote vinatoka ndani ya moyo,” anasema mchezaji huyo wa zamani.


JOSH 06

NIYONZIMA, CHAMA NI HABARI NYINGINE

Joshua anasema kuna maproo wengi wa kigeni ambao walifanya vizuri kipindi anacheza na sasa,  lakini hajawahi kuona vipaji vya aina yake kama walivyonavyo Clatous Chama na Haruna Niyonzima wote wawili waliwahi kuichezea Simba na Yanga.

“Chama amelinda kiwango chake tangu ajiunge na Simba 2018 hadi sasa bado  jina lake linatajwa kati ya wachezaji wanaocheza kwa kiwango cha juu,  Chama ana usasa na uzamani nikiwa na maana ya zamani alifanya vizuri, bado anaenda sawa na wachezaji wa sasa” anasema Joshua.

Mbali na hao alikuwepo Pascal Wawa, Thaban Kamusoko, Emmanuel Okwi, Amissi Tambwe, marehemu Patrick Mutesa Mafisango jamaa alikuwa anajua mpira, hao  walitupa chalenji kama wazawa ili tuwe tunapambana kwa kiwango cha juu,” anasema.

“Kwa maproo wanaocheza sasa hivi miongoni mwao ni Maxi Nzengeli, Pacome Zouzoua ingawa kwa sasa ni majeruhi, Djigui Diarra, Chama, Elie Mpanzu aliyemkalisha beki wa Yanga mechi ya dabi Ibrahim Bacca, Rushine De Reuck na Libasse Guaye wanajua walichokuja kukifanya Tanzania.”

Mkongwe huyo anasema maproo wana kiwango cha juu na wanajua kulinda viwango vyao kwa muda mrefu kuliko wazawa, anasisitiza hilo liwaamshe ili kuwe na ushindani mkubwa, ili wanapokutana kila mmoja akiwa na timu ya taifa lake, waweze kufanya vitu vikubwa.

“Ingawa kuna wazawa baadhi ambao wamecheza kwa kiwango kwa muda mrefu, mfano Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ na Shomari Kapombe, wengi wao wanakuwa vizuri msimu mmoja unaofuata wanapotea au miezi sita unasikia ana majeraha, lakini wakiamua wanaweza wakawa na ushindani wa juu, kwani wana vipaji vikubwa pia itasaidia kuongeza ushindani wanapokutana nao wakiwa na timu zao za taifa,” anasema.

Joshua anasema Ligi Kuu inazidi kuwa bora, jambo ambalo linavutia wageni kuja kucheza Tanzania:

JOSH 02

“Ndiyo maana ligi ipo nafasi ya sita kwa ubora Afrika, basi hata wazawa wanapaswa kupambana ili na wao watoke kama ilivyokuwa kwa kina Mbwana Samatta na Simon Msuva ambao wamelitangaza taifa kwa kile walichokifanya nje, basi wengine wafuate nyuma yao.”

Pamoja na hilo anasema,  kipato kwa wachezaji wa sasa kimeongezeka, hivyo anaamini wengi wao watafanya vitu vikubwa vitakavyoendelea kuwavutia wengine kuona soka ni ajira:

“Naamini kupitia kipato chao watakuwa wanajiandaa na maisha nje na uwanjani.”


JOSH 05

TUKIO HILI LINGEMTOA ROHO

Mchezaji huyo wa zamani anasema kuna kipindi Yanga ilikuwa haijalipa pesa hotelini, hivyo ilitakiwa kila mchezaji awe ananunua chakula mwenyewe, ndipo alipokutana na tukio baya ambalo lingehatarisha maisha yake.

“Nikawa nimekwenda kununua chakula nje na kambini pale Jangwani, wakati naanza kula niliikuta pini katikati ya chakula, nikaitoa yule muuzaji alibakia anahofu kwenye macho yake, nimeitunza hadi leo maana ningeimeza ningeenda kufanyiwa upasuaji au ningekufa” anasema na kuongeza:

“Baadaye niligundua yule mdada muuzaji wa chakula, alikuwa anatoka kimahusiano na mchezaji mwenzangu, niliyekuwa nashindana naye namba, niliwaza mbali kwamba hata kama ni ushindani usifike pabaya kwani kuna maisha baada ya uwanjani, niliunganisha tukio hilo maana sehemu ambako nilikokuwa nimepanga alikuwa akipita mtaani na kuanza kuongea  maneno ya hovyo, nilikuwa naambiwa na majirani na mke wangu.”


JOSH 04

DABI HAZIZOELEKI

Joshua anasema kwamba kwa muda aliodumu Yanga alicheza dabi 16 mechi za Ligi Kuu, mbili za Kombe la FA na moja Ngao ya Jamii, lakini hakuwahi kuona kama zinazoeleka, kila wakati kulikuwa na presha kubwa.

“Mechi ambayo sitakaa niisahau ilituumiza kupita kiasi, ilikuwa ni 2012 ambayo Simba ilitufunga mabao 5-0, nyingine ni ile ambayo Shiza Kichuya alisawazisha bao alipiga mpira wa kona na akafunga moja kwa moja, golini alikuwepo Ally Mustapha ‘Barthez’,” anasema Joshua akisisitiza umaarufu unaweza ukawa mbaya kama mtu anakubali umuendeshe.

Mbali na hilo anasema bado anaendelea kucheza ligi ya maveterani na msimu wa 2025/26 alikuwa mfungaji bora wa mabao 18 akiwa na timu ya Yanga.