Hawa ni mwiba kwenye Dabi ya Kariakoo
MASTAA waliyowahi kuzichezea Simba na Yanga wamezungumzia Dabi ya Kariakoo itakavyokuwa na ushindani na ugumu, huku wakiweka wazi kumbukumbu zao katika mechi hizo.
Mwanaspoti limefanya mahojiano na baadhi ya mastaa hao kwa nyakati tofauti na miongoni mwa mambo wanayotarajia kuyaona katika dabi itakayopigwa leo, Oktoba 10, 2026, katika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam ni mbinu za makocha na wachezaji ambao watakaotakiwa kuchungwa.
ALLY SALIM
Kipa wa zamani wa Simba na Taifa Stars, Ally Salim ambaye kwa sasa anaichezea Dodoma Jiji anaitazama dabi ya leo jinsi itakavyoamuliwa kwa mbinu na kutumia nafasi, bila kuangalia nani ni bora zaidi ya mwingine
“Hakuna dabi rahisi, kwa eneo la golikipa ninalocheza Djigui Diarra wa Yanga na Mahamadou Kassali wa Simba wote wana kazi ngumu, wajipange na kuongeza umakini kwani anaweza akafunga mchezaji yoyote, anayepata nafasi ya kufanya hivyo, pengine tofauti na matarajio ya wengi,” anasema.
Anaitaja dabi ya Aprili 10, 2023 Simba ilishinda mabao 2-0 dhidi ya Yanga, ambayo ilikuwa na mastaa wenye uwezo mkubwa kama Fiston Mayele, Bernard Morison, Jesus Moloko na Aziz Ki.
“Nilikuwa kipa namba tatu, namba moja alikuwa Aishi Manula na wa pili alikuwa Beno Kakolanya, kitendo cha kuaminiwa mechi ngumu na nikafanya sevu nyingi ilinipa heshima kubwa nikapewa nafasi ya kuaminiwa na mechi ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Wydad Casablanca ya Morocco tulifungwa bao 1-0,” anasema.
BENO KAKOLANYA
Kipa mwingine wa Polisi Tanzania, Beno Kakolanya aliwahi kuichezea Yanga kuanzia 2018/19, akitokea Tanzania Prisons na kuanzia 2023/24 Simba, anaiona itakuwa dabi ngumu na ushindani mkali, kulingana na pafomasi za timu hizo kwa msimu huu.
“Haijawahi kuwa dabi rahisi, inawagawa Watanzania katika makundi mawili, jambo ambalo kama wachezaji wanapaswa kujipanga na kujitoa kwa ajili ya timu zao, ili mashabiki wakiona wanaona walipambana,” anasema Kakolanya na kuongeza:
“Mechi iliyosalia katika kumbukumbu ya maisha yangu ya mechi za dabi ilikuwa ya Septemba 30, 2018, ukiacha kufanya vizuri uwanjani, mama yangu mzazi kwa sasa marehemu aliniombea kwa kuniwekea mkono kichwani ili nifanye vizuri na ilikuwa hivyo, inanifanya nisisahau.”
Kiushindani anawakumbuka washambuliaji wa Simba waliyokuwa hatari zaidi golini kwake na kuokoa mashuti yao ni Meddie Kagere, Emmanuel Okwi, Shiza Kichuya, kiungo Clatous Chama na beki Shomari Kapombe, ingawa katika mechi ijayo anawaona mastaa wa kuchungwa zaidi ni Maxi Nzengeli, Peter Shalulile, Clatous Chama na Libasse Gueye hao ni baadhi.
SHIZA KICHUYA
Aliyekuwa mshambuliaji wa Simba, Shiza Kichuya anayekipiga Coastal Union ya Tanga, anasema kuna mechi nyingi za dabi zenye kumbukumbu kwake lakini hataisahau ya Oktoba Mosi, 2016 ambayo alifunga bao la kusawazisha kwa mpira wa kona.
“Ilikuwa mechi yenye presha, bao la Yanga lilifungwa na Amissi Tambwe, mimi nikasawazisha kwa mpira wa kona ambao uliingia moja kwa moja golini golikipa alikuwa Ally Mustapha ‘Barthez’ mashabiki wa Simba walikuwa na furaha sana siku hiyo, sasa naiona Dabi nyingine yenye ushindani mkubwa sana kesho (leo),” anasema.
SAID MAKAPU
Kwa upande wa kiungo mkabaji wa Mbuni ya Championship, Said Makapu ambaye aliwahi kuichezea Yanga kuanzia mwaka 2015-2023 anaikumbuka dabi ya Novemba 7, 2020/21 iliyomalizika kwa sare ya bao 1-1, Uwanja wa Benjamin Mkapa.
“Dabi hiyo ilikuwa ngumu na utata wa matukio mengi, mashabiki wa Simba walikuwa wanalalamika kwamba Joash Onyango hakumshika ndani ya 18 Tuisila Kisinda, wakati mwamuzi aliamuru ipigwe penalti ambayo ilipigwa na Michael Sarpong, hivyo tukawa tunaongoza kwa bao 1-0 lakini akaja akasawazisha Onyango mwenyewe kwa kufunga kwa kichwa baada ya kupokea mpira wa kona ambao ulipigwa na Luis Miquissone, ukiacha hilo wachezaji hatari kwa mechi ijayo Simba itatakiwa iwachunge Shalulile na Maxi na Yanga itakuwa na kazi ya kuwazuia Libase na Chama, Oura,” anasema.
DITRAM NCHIMBI
Staa mwingi wa zamani wa Yanga, Ditram Nchimbi aliungana na Makapu kuona mechi ambayo kwake anaiona ilikuwa ngumu na ushindani mkali ni ya Novemba 7, 2020/21.
“Simba ilikuwa na wachezaji hatari kama John Bocco,Chama, Pascal Wawa, Onyango, Shomari Kapombe, Miquissone, Jonas Mkude licha ya Yanga kuwatangulia bao moja hawak ukata tamaa hadi wakasawazisha, Yanga pia ilikuwa na wachezaji wenye viwango vya juu kama Kisinda, Mukoko Tonombe,Feisal Salum ‘Fei Toto’ kifupi kila timu ilikuwa na wachezaji wa levo za juu,” anasema mchezaji huyo na kuongeza:
“Ndiyo maana ilikuwa na ushi ndani na burudani kali, lakini wachezaji wa kuchungwa bado Chama yupo vizuri anaweza akawa mwiba Yanga pamoja na Libase, kwa Yanga kuna Shalulile, Nzengeli na wengine.”
SAID NDUDA
Kipa wa zamani wa Simba na Yanga, Said Mohamed ‘Nduda’ anasema dabi ambayo haijawahi kusahaulika katika maisha yake ni ya mwaka 2012.
“Nakumbuka wakati nacheza Yanga tulifungwa mabao 5-0 matokeo yaliniumiza sana, ingawa kwa sasa naona kwa mashabiki imepungua kuwa mfano wa kufungwa mabao mengi baada ya Yanga kuifunga Simba mabao 5-1, lakini kwa wachezaji ambao nawaona wapo kwenye kiwango cha juu, kwanza makipa wote wa timu mbili wapo imara, ila kwa wachezaji wa ndani kuna Shalulile, Nzengeli, Libase, Chama, Shomari Kapombe ana uzoefu mkubwa anaweza akafanya lolote lenye kuleta madhara kwa Yanga,” anasema mkongwe huyo.