Harry Kane: Mabao 73 yataongea Ballon d’Or
Muktasari:
- Katika mahojiano na MARCA, amefichua pia nini anachofikiria kufanya katika safari ya soka ambayo bado inaendelea. Twende pamoja...
MUNICH, UJERUMANI: HARRY Kane, nyota wa kimataifa wa England na Bayern Munich amezungumza mambo kibao katika mahojiano yake ya hivi karibuni, lakini akigusia namna tuzo ya mchezaji bora Ulaya (Ballon d’or) inavyowatesa wengi, lakini upande wake akiamini mabao 73 aliyofunga msimu uliopita katika Bundesliga, Ligi ya Mabingwa Ulaya na England yatambeba.
Katika mahojiano na MARCA, amefichua pia nini anachofikiria kufanya katika safari ya soka ambayo bado inaendelea. Twende pamoja...
Swali: Tuanzie Ligi ya Mabingwa. Umekwishashinda kila kitu ndani ya Ujerumani, hivyo Ligi ya Mabingwa inaonekana kuwa changamoto yako kubwa ukiwa Bayern. Hili lipoje?
Jibu: Ndiyo, hasa. Msimu uliopita ulikuwa mzuri sana kwetu. Tulimaliza nafasi ya pili katika hatua ya ligi, tukishinda mechi saba na kupoteza moja. Baadaye tulicheza vizuri dhidi ya Atalanta, Real Madrid na PSG. Mchezo dhidi ya Real ulikuwa wa kipekee, huku mechi mbili dhidi ya PSG zikiwa za kuvutia sana kwa mashabiki. Ilikuwa vigumu kukubali kufungwa kwa tofauti ndogo. Tulikuwa karibu sana na tulikuwa na ubora na kujiamini kufika fainali. Hata hivyo, ndivyo Ligi ya Mabingwa ilivyo; mambo huamuliwa na tofauti ndogo sana.
Swali: Vipi msimu huu?
Jibu: Tunataka kufanya mambo karibu kama tulivyofanya msimu uliopita, kisha kupiga hatua ya mwisho. Timu yetu ina njaa ya mafanikio, wachezaji na kocha pia.
Swali: Fainali itafanyika Madrid, na katika hatua ya ligi mnakutana na Atletico, unazungumziaje
Jibu: Ndiyo. Sidhani kama nimewahi kucheza dhidi yao, kwa hiyo itakuwa mara yangu ya kwanza. Atletico wameonyesha ubora wao kwa kufika nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa msimu uliopita. Ninawaheshimu sana. Itakuwa mechi ngumu, lakini tutajiandaa. Nilipoteza fainali ya Ligi ya Mabingwa nikiwa Tottenham katika Uwanja wa Metropolitano, na ilikuwa wakati mgumu. Natumaini kurejea hapo na kupata matokeo tofauti.
Swali: Ni jambo lisilo la kawaida kuona unavyoongeza mabao kadiri umri unavyoongezeka. Siri yako ni nini?
Jibu: Moja ya siri hizo ni mtu mnayemfahamu vizuri; daktari wangu binafsi wa michezo, Alejandro Elorriaga, aliyezaliwa Madrid. Alejandro amekuwa na mchango mkubwa katika mafanikio yangu.
Swali: Amekusaidiaje tangu mlipoanza kufanya kazi pamoja miaka saba iliyopita?
Jibu: Alejandro ana nafasi muhimu katika hali yangu ya sasa. Tunafanya kazi nyingi nyuma ya pazia na tumekuwa tukishirikiana kwa miaka sita. Ni miongoni mwa sababu kuu zinazonifanya niweze kucheza katika kiwango hiki na kushiriki mechi nyingi. Siyo bahati kwamba nimeendelea kuboresha kiwango changu, licha ya baadhi ya watu kuamini uwezo hupungua kadiri umri unavyoongezeka. Kwangu imekuwa karibu kinyume chake. Kazi tunayofanya inanipa matokeo mazuri na kutufurahisha wote. Pia ni mtu mzuri, na tunatumia muda mwingi pamoja. Ninataka kumshukuru sana kwa kila anachonifanyia.
Swali: Una siri gani nyingine?
Jibu: Soka wakati mwingine linahusu muda sahihi. Kuwa Bayern, nikiwa na timu bora inayonizunguka, kunaniwezesha kufunga mabao mengi na kuchangia pia katika pasi, ulinzi na mambo mengine ninayofurahia kufanya kwa ajili ya timu. Kwa kweli, sijawahi kujisikia vizuri kimwili na kiakili kama sasa. Lazima nitumie vizuri kipindi hiki kwa sababu muda hauwezi kudumu milele kadiri unavyozeeka. Kwa sasa niko katika hali nzuri sana.
Swali: Huchoki kushangilia mabao?
Jibu: Kamwe! Kufunga bao ni hisia nzuri zaidi. Kunatoa msisimko mkubwa wa mwili na pia kunaleta nafuu. Najua nitayakosa sana mambo hayo nitakapoacha kucheza.
Swali: Wewe ni mmoja wa wanaowania Ballon d’Or. Mabao 73 katika mechi 65 za Bayern na England msimu wa 2025/26 yanastahili kukubeba?
Jibu: Ni jambo gumu. Sijawahi kupenda kujizungumzia sana. Msimu uliopita ulikuwa wa ajabu kwangu binafsi na kwa timu. Ulikuwa msimu bora zaidi maishani mwangu. Kufunga mabao 73, idadi ya pili kwa wingi katika historia baada ya Lionel Messi aliyefunga 82 katika mechi 69 msimu wa 2011/12, kunajieleza. Ninajivunia sana na ninawashukuru wachezaji wenzangu pamoja na wote walionisaidia. Lakini Ballon d’Or haiko mikononi mwangu; inategemea wapigakura. Kwangu msimu uliopita umekwisha. Sasa nimeelekeza fikra zangu msimu huu na nina hamu ya kuona nitafanya nini zaidi. Najua tuzo hiyo itazungumziwa sana hadi Oktoba kwa sababu ni tuzo kubwa.
Swali: Sherehe za mwaka 2026 zitafanyika London kwa mara ya kwanza. Hilo linaeleza nini?
Jibu: Watu wengi wamenitajia jambo hilo, na huenda ikawa ishara nzuri. Kufanyika katika mji nilikozaliwa kungeifanya iwe ya kipekee zaidi. Inashangaza kuona sherehe hizo zikifanyika huko mwaka huu. Tusubiri tuone kitakachotokea.
Swali: Unawapongeza wenzako unapopokea tuzo ya Kiatu cha Dhahabu? Ukishinda cha tatu, utaungana na Messi aliyeshinda sita na Cristiano Ronaldo aliyeshinda vinne. Hakuna mwingine aliyefikisha vitatu, hili lipoje?
Jibu: Messi na Ronaldo walitawala soka kwa kizazi kizima (kinachoondoka). Ni miongoni mwa wachezaji bora zaidi katika historia. Kutajwa pamoja nao ni jambo la kipekee. Kama mshambuliaji, ninatarajiwa kufunga mabao. Kiatu cha Dhahabu siyo lengo langu pekee, lakini kukishinda kunamaanisha pia nimeisaidia timu. Kila ninaposhinda nataka kingine. Msimu huu hautakuwa tofauti. Natumaini kufunga mabao mengi Bundesliga na kuona kama nitaweza kushinda tena.
Swali: Ulikutana na Messi katika nusu fainali yenye utata ya Kombe la Dunia (2026) kati ya England na Argentina. Baadaye mlionyeshana heshima kubwa. Unakumbukaje tukio hilo?
Jibu: Ilikuwa siku ngumu kwangu kuondolewa mashindanoni kwa namna ile. Lakini ninamheshimu sana Messi. Nimemuona akikua kama mwanasoka. Ni mchezaji wa ajabu na, kwa mujibu wa wanaomfahamu. Pia ni mtu mzuri. Nimekutana naye mara chache, lakini anaonekana mnyenyekevu. Daima ameitanguliza timu, na naamini hiyo ni sababu mojawapo ya mafanikio ya Argentina. Nakumbuka nilimkumbatia na kumtakia kila la heri katika fainali. Kombe hilo halikuwa letu, lakini ndivyo ilivyo; wachezaji bora hukutana kwenye mashindano makubwa na lazima kuwe na anayepoteza. Nilijitahidi kukubali matokeo na kuiheshimu timu pinzani, hasa Messi kwa mafanikio yake ya muda mrefu.
Swali: Jose Mourinho, kocha wako wa zamani Tottenham, alikuwa mtu wa kipekee kwako?
Jibu: Ndiyo, nampenda sana Jose. Tulikuwa na uhusiano mzuri Tottenham. Mambo hayakuishia tulivyotaka, na ilikuwa vigumu kwake kukosa nafasi ya kuiongoza timu katika fainali ya Kombe la Carabao 2020/21 baada ya kutimuliwa Aprili. Hilo lilikuwa gumu kwangu pia. Nilicheza baadhi ya mechi zangu bora chini yake, nikashinda Kiatu cha Dhahabu na tuzo ya mtoa pasi nyingi za mabao katika ligi mwaka huohuo. Alinipa uhuru wa kucheza kwa namna yangu na kushuka nyuma kupokea mpira. Anaelewa kila kipengele cha mchezo, kuanzia mbinu hadi namna ya kucheza na bila mpira. Ninamheshimu sana. Hatukukutana sana tangu aondoke Tottenham, lakini huenda tukakutana Ligi ya Mabingwa msimu huu.
Swali: Mourinho akiwa Real Madrid, je, itakuwa vigumu zaidi kwa Bayern kuwakabili?
Jibu: Real wamesajili wachezaji wazuri, na Mourinho ni kocha mkubwa anayeweza kupata ubora wa wachezaji wake. Madrid daima huwa na baadhi ya wachezaji bora duniani. Tunajua tunaweza kukutana nao katika hatua za baadaye. Mwaka jana tuliwashinda katika robo fainali, lakini ilikuwa mechi ngumu. Mourinho akiwa hapo, changamoto itakuwa kubwa zaidi.
Swali: Jude Bellingham ameanza vizuri msimu. Unamuonaje?
Jibu: Tulielewana vizuri sana Kombe la Dunia kutokana na namna tulivyocheza na kupasiana. Tulijenga pia uhusiano mzuri nje ya uwanja, jambo linaloweza kuisaidia timu ya taifa. Nafurahi kuona alivyoizoea Madrid. Nilizungumza naye kuhusu Mourinho wakati wa Kombe la Dunia na nilijua angempenda. Pia nilijua Jose angempenda Jude. Inaonekana tayari wana uhusiano mzuri. Ameanza msimu vizuri, na kwa upande wa England hilo ni jambo zuri.
Swali: Ungeweza kucheza La Liga wakati fulani huko nyuma?
Jibu: Kulikuwa na nyakati ambazo hilo lingewezekana, ingawa siwezi kusema kulikuwa na nafasi rasmi. Kulikuwa na mazungumzo. Ninaiheshimu sana La Liga. Barcelona, Madrid na Atletico ni klabu kubwa duniani. Nilikuwa nikimtazama Ronaldo, Messi na wengine. Sifungi mlango kwa chochote kwa sababu kila kitu kinawezekana katika soka. Kwa sasa nina furaha sana Ujerumani.
Swali: Hispania ilikutana na England Wembley katika Ligi ya Mataifa ya Ulaya. Uliionaje mechi hiyo?
Jibu: Ilikuwa ngumu. Hispania ni mabingwa wa sasa wa Ulaya na dunia. Tumekuwa karibu nao katika miaka ya hivi karibuni, lakini wao wamefanikiwa kufika mwisho huku sisi tukishindwa. Tunawaheshimu sana. Hispania walishinda mashindano ya Ulaya miaka michache iliyopita, na mafanikio hayo yaliwasaidia kufikia kiwango walichonacho sasa. Kwa England, ni mfano wa kuigwa. Hatujashinda taji kwa muda mrefu, hivyo huenda tukafanya hivyo mwaka huu. Hispania ni timu ngumu kutokana na umiliki wao wa mpira na wachezaji walionao.
Swali: Mwisho, familia yako; mke uliyekutana naye ukiwa kijana na watoto wanne ni moja ya siri za mafanikio yako?
Jibu: Nafikiri, ndiyo. Watu hawazungumzi vya kutosha kuhusu umuhimu wa utulivu wa familia katika soka la kulipwa, hasa kwa wachezaji vijana. Nina bahati kuwa na mke wangu ambaye tulisoma naye shule moja, pamoja na wazazi wangu, kaka yangu na wakwe zangu. Najua hali siyo sawa kwa kila mtu. Lakini, ukiwa na furaha nje ya uwanja na maisha yakiwa katika utulivu, hali hiyo husaidia pia kiwango chako uwanjani. Nashukuru sana kwa kila wanachonifanyia na msaada wanaonipa. Kila nachofanya ninajitahidi kukifanya kwa pamoja nao. Wao ndio nguzo yangu kubwa.