Habib Kinyogoli: Miaka 78 bado hajachoka na ngumi
Muktasari:
- Ni katika 'gym' ya Kinyogoli inayopatikana katika eneo la Ilala jijini Dar es Salaam.
Ni alfajiri lakini vijana wengi wanaendelea kutupa makonde kwenye magunia 'Punching bags', wengine wakifanya mazoezi ya viungo na wengine wakibadilishana makonde kwenye ulingo.
Ni katika 'gym' ya Kinyogoli inayopatikana katika eneo la Ilala jijini Dar es Salaam.
Pembeni ya mabondia hao yupo mtu ambaye kwa haraka haraka namtambua kuwa ni kocha wa masumbwi ambaye ameitumikia mchezo huo kwa zaidi ya miongo sita.
Huyu si mwingine bali ni Habib Kinyogoli 'Master',ambaye ni kocha maarufu wa mchezo wa masumbi Tanzania.
Kinyogoli ambaye kwa sasa ana miaka 78, amezungumza na Spoti Mikiki na kuelezea hali ya mchezo huo pamoja mustakabali wa kazi yake hiyo, hasa baada ya umri wake kuonekana kusogea.
NDOTO ANAYOISHINAYO
Anasema licha ya umri wake mkubwa, bado ana ndoto ya kuhakikisha anawatengenea vijana wengi ili waje kuwa mabondia wakubwa na kuipeperusha vema bendera ya Tanzania nje ya mipaka.
“Sina mpango wa kuacha kufundisha ngumi kwa sababu ya umri, labda niugue maradhi yatakayonifanya nishindwe kufanya kazi yangu au umauti utakaponikuta.
Mimi sina kazi nyingine ya kufanya zaidi ya hii na kwa hakika naifurahia, niache ngumi ili nifanye nini, vijana bado wanahitaji mafunzo yangu,” anasema Kinyogoli na kuongeza.
"Kwanza michezo ni afya, hivi unavyoniona ni kwasababu ya kushiriki mazoezi, kama ningekuwa sijishughulishi afya yangu ingekuwa imetetereka."
VIJANA WAMIMINIKA
Anasema amekuwa akipokea vijana wengi wapya wanaotaka kujiunga na gym yake na kupata mafunzo ya mchezo huo.
"Kama kazi yako unaifanya vizuri lazima watu wataipokea, vijana wengi wanakuja hapa wakitaka kujiunga na sisi.
"Uwa tunawapokea na kuwapa utaratibu wa kawaida lazima ambao watatakiwa kuuzingatia ikiwemo kujaza fomu na kutoa kiingilio ambacho ni fedha kidogo,akitimiza hayo atapopewa sheria za hapa kisha ataendelea na mafunzo,"anasema Kinyogoli na kuongeza.
"Na si mafunzo ya ubondia pekee yake,hapa pia atapata mafunzo ya kusimamia mchezo wenyewe kwa maana uamuzi, kuna semina huwa zinafanyika hapa, asubuhi tunakuwa wengi, lakini mchana kutwa watu wanafanya mazoezi maana kuna wale wanaokuja mmoja mmoja."
Anasema hana kumbukumbu sahihi ya idadi ya mabondia wanaofanya mazoezi kwenye gym yake, lakini anakiri kuwa na idadi kuwa inayojumuisha pia wanawake watatu.
"Katika gym yangu kuna mabondia wengi ambao sina idadi yao kamili, pia kuna mabondia wa kike watatu wanafanya mazoezi hapa,"anasema Kinyogoli.
Namuuliza kama kuna mwanae yeyote aliyefuata nyayo zaidi, anajibu kwa kusema: "Watoto watatu nao wameingia kwenye ngumi kama mimi, kuna Siraji ambaye tayari amestaafu ngumi, Maliki ambaye ni marehemu na Jawadu.
Huyu ni mdogo namwangalia kama ananishawishi kweli au ana malengo yake mengine ya kimaisha maana ndio kwanza ametoka kumaliza kidato cha nne,” anasema Kinyogoli.
ENZI ZAO NA SASA
Kuhusu mtazamo wake kwa mabondia wa kizazi cha sasa na nyakati zao, anasema kuna utofauti mkubwa hasa katika ufanyaji wa mazoezi.
“Mabondia wa sasa akishamaliza mazoezi ya pamoja ndio mpaka kesho, hawajiongezi. Mimi nilikuwa nikimaliza ya pamoja nafanya mengine binafsi, kipaji peke yake hakitoshi bila jitihada.
“Mimi nilikuwa sipandi gari kwenda kazini, nilikuwa nakimbia huku mgongoni nikiwa na beki langu, ilikuwa sehemu ya mazoezi kwangu ni tofauti kabisa vijana wetu wa sasa.”
Kinyogoli anasema kwake mazoezi yalikuwa sehemu ya maisha, si shughuli ya kufanya kwa muda maalumu pekee.
Anasema bondia anayetaka kufika mbali lazima ajenge nidhamu inayozidi muda anaoutumia akiwa na kocha.
“Ili bondia awe bora lazima azingatie misingi ya mchezo wenyewe, apate muda wa kupumzika na kuachana na mambo yatakayoathiri afya yake kama ulevi wa kupindukia,"anasisitiza.
REKODI MBAYA NJE
Napata fursa ya kumuuliza kwanini mabondia wa Tanzania hawana rekodi nzuri wanapopanda ulingoni nje ya nchi anajibu kwa kusema:
“Nikuambie kitu, wapo wanaouza mechi kwa wapinzani, wanapewa hela ili wapigwe na kuwatengenezea rekodi wapinzani.
"Wengine wanapigwa kutokana na tamaa ya fedha,wanalazimika kucheza uzito usiokuwa wao,"anasema Kinyogoli.
URITHI KWA WATOTO
"Nina watoto watatu ambao wameingia kwenye ngumi kama mimi, Siraji ambaye amestaafu ngumi, Maliki (marehemu) na Jawadu. Huyu ndiye mdogo naye anakuja vizuri,” anasema.
Kuhusu mtazamo wake kwa mabondia wa kizazi cha sasa na nyakati zao anasema kuna utofauti mkubwa hasa katika ufanyaji wa mazoezi.
“Mabondia wa sasa akishamaliza mazoezi ya pamoja ndio mpaka kesho, hawajiongezi. Mimi nilikuwa nikimaliza ya pamoja nafanya mengine binafsi, kipaji peke yake hakitoshi bila jitihada.
“Mimi nilikuwa sipandi gari kwenda kazini, nilikuwa nakimbia huku mgongoni nikiwa na beki langu, ilikuwa sehemu ya mazoezi kwangu ni tofauti kabisa vijana wetu wa sasa.”
Kinyogoli anasema kwake mazoezi yalikuwa sehemu ya maisha, si shughuli ya kufanya kwa muda maalumu pekee.
Anasema bondia anayetaka kufika mbali lazima ajenge nidhamu inayozidi muda anaoutumia akiwa na kocha.
“Ili bondia awe bora lazima azingatie misingi ya mchezo wenyewe, apate muda wa kupumzika na kuachana na mambo yatakayoathiri afya yake kama ulevi wa kupindukia,"anasisitiza.
Napata fursa ya kumuuliza kwanini mabondia wa Tanzania hawana rekodi ya ushindi wanapopanda ulingoni nje ya nchi anajibu kwa kusema:
“Nikuambie kitu, wapo wanaouza mechi kwa wapinzani, wanapewa hela ili wapigwe na kuwatengenezea rekodi wapinzani.
"Wengine wanapigwa kutokana na tamaa ya fedha,wanalazimika kucheza uzito usiokuwa wao,"anasema Kinyogoli.
WAKALI WALIOPITA MIKONONI MWAKE
Kinyogoli anasema kuwa, mikononi mwake wamepita mabondia wengi maarufu ambao anasema vigumu kuwakumbuka kwa majina, lakini kwa sasa katika gym yake anaapatika Ibrahim Class.
Ibrahim Class ni miongoni mwa mabondia maarufu na wanaofanya vizuri nchini akiwa na rekodi ya kutwaa mikanda kadhaa lakini wa hivi karibuni ni ule wa WBC International Super Featherweight Title alipomtwanga Kritiphak Duangnut kwa TKO ya raundi ya tano.Pambano hilo lilifanyika Aprili 25, mwaka huu Bangok Thailand.
Class anamzungumzia Kinyogoli akisema kwake anamchukulia kama mzazi na si kocha pekee.
"Kinyogoli kwangu ni baba na si kocha tu, mimi mama yangu alifariki nikiwa mdogo na baba akatutelekeza kwa bibi.
"Ni huyu mzee unayemwona hapa ndio alinichukua nakunipeleka kwenye mchezo huu,"anasema Class na kuongeza.
"Kwanza ananishangaza kitu kimoja, licha ya umri wake mkubwa lakini anajua mbinu za kisasa wakati huwa aingii hata 'you tube'.
"Mimi wakati mwingine naweza kwenda gym nyingine kufanya mazoezi lakini nikipamba pambano tu lazima nirudi hapa kupata baraka."
USHAURI KWA MAMLAKA
Kinyogoli anasema hafurahishwi na mwenendo wa mchezo huo kwa sasa, akidai kwamba umeegemea kwenye biashara na si kuboresha viwango vya mabondia.
Anasema kuwa,mabondia wengi wamekuwa wakishawishika kucheza mapambano ya kulipwa huku wakiwa hawajapitia misingi sahihi, hivyo kupelekea kukosa ubora unaostahili.
"Misingi ya mchezo wa ngumi inakiukwa, turudi kwenye misingi. Ngumi za ridhaa lazima ziwepo, tusipozingatia hili tutakuwa na mabondia wengine lakini wachache wenye ubora,"anasema na kuongeza.
"Siwezi kuwapangia nini cha kufanya lakini hao wanaosimamia mchezo waje waombe ushauri tutaaambia nini cha kufanya,"anasema Kinyogoli.
KINYOGOLI AMETOKA WAPI?
Kinyogoli alizaliwa Oktoba2,1948, katika kijiji cha Mwaneromango, Kisarawe mkoani Pwani.
Anasema alianza kujifunza mchezo wa ngumi akiwa na miaka 10, akifundishwa misingi ya mchezo huo na kaka yake ambaye kwa sasa ni marehemu anayemtaka kwa jina la Saidi Uliza 'Sheni'.Anasema kaka yake huyo alikuwa akiishi jijini Dar es Salaam.
"Wakati wetu kama wewe si mbabe basi utapata shinda sana mtaa, ili kuondokana na unyonge huo, nilimwambia kaka yangu(Sheni)ambaye wakati huo alikuwa anaishi Dar es Salaam, kuwa na mimi nataka kujifunza ngumi, alikubali na safari ikaanzia hapo,"anakumbuka.
Anasem baada ya kumaliza shule, alielekea Dar es Salaam na kujiunga na klabu ya masumbwi ya Magomeni, ambako alipata mafunzo kutoka kwa makocha Kassim Saidi na Joseph Okalla.
Anakumbuka pambano lake la kwanza ulingoni kuwa alilicheza mwaka 1966, dhidi ya Ally Kanduru wa JKT, katika uzani wa light-welterweight.
Anakumbuka kuwa alishinda kwa KO raundi ya pili, kisha mwaka uliofuata alitwaa ubingwa wa taifa wa uzani wa light baada ya kumshinda Jack Laimon wa Anartouglou.
Anasema umahiri wake uliongozi ulimfanya kujumuishwa katika timu ya taifa iliyoshiriki mashindano mbalimbali ya kimataifaa ikiwemo Jumuiya ya Madola mwaka 1970, Olimpiki 1972 na Michezo ya Africa iliyofanyika Lagos, Nigeria mwaka 1973.
Anasema katika mashindano ya Afrika alifanikiwa kushinda medali ya fedha.
Anataja mapambano mawili ambayo hawezi kuyasahau kuwa ni dhidi ya bondia wa Uganda Deo Musoke, katika mashindano ya Afrika Mashariki yaliyofanyika kwaka 1971,Nairobi,Kenya.
Kinyogoli anasema kumbukumbu hiyo haiwezi kufutia katika kichwa chake kwakua hakuwa anapewa nafasi ya kushinda.
Jingine lile lililomkutanisha na bondia Mnigeria, Eddy Nduku, ambapo alifanikiwa kumchapa kwa KO ya raundi ya tatu
Anasema kuwa, hadi aliamua kustaafu ndondi za ridhaa alikuwa amecheza takribani mapambano 110, akishinda 95 na kupoteza 15, huku akikusanya medali kadhaa.
Kinyogoli anasema kuwa, baada ya kupumzika kupanda uliongoni, mwaka 1976 aligeukia ukocha wa mchezo huo, akiamini anao mchango kwa vijana wa Tanzania kufikia malengo yao.
Anasema katika safari yake ya ukocha, aliwahi kufundisha Klabu ya Masumbwi ya Simba, ambapo pia ilikuwa na michezo mingine ikiwemo soka na kikapu.
Anawataja baadhi ya mabondia maarufu wa zamani aliopata fursa ya kuwanoa akiwa kocha wa masumbwi wa klabu ya Simba kuwa ni kutoka familia maarufu ya Matumla akiwemo Rashid Matumla.
Huyu ndiye Kinyogoli ambaye kwake umri mkubwa si kigezo cha kuacha kufundisha masumbwi.