Prime
Guede afichua siri... Aitaja Yanga na wanachama
DIRISHA dogo la usajili limekuwa mara kadhaa chanzo cha hadithi kubwa ndani ya Singida Black Stars, na mojawapo iliyoacha alama isiyofutika ni ile ya Jonathan Sowah.
Mshambuliaji huyo ambaye kwa sasa anakipiga Simba, alipotua Singida Black Stars katika dirisha dogo, hakuhitaji muda mrefu kujitambulisha. Mechi yake ya kwanza tu alianza kutupia mabao, hadi kufikisha mabao 13 ya mfululizo yaliyotosha kubadilisha taswira ya kikosi na kuweka rekodi ambayo kwa muda mrefu ilionekana kuwa ngumu kuvunjwa.
Sowah alitua Singida Black Stars dirisha dogo la msimu wa 2024/25 na alifanikiwa kutupia mabao hayo 13 kwenye mechi 14 za Ligi Kuu Bara alizoichezea timu hiyo, jambo lililoivutia Simba iliyomnasa dirisha kubwa la usajili msimu huu.
Sasa, macho yote yameelekezwa kwa Guede, aliyerejea Singida na kuanza upya safari yake kwa mtindo unaofanana kabisa na wa Sowah. Hadi sasa timu hiyo inayoshiriki michuano ya Mapinduzi Cup, mshambuliaji huyo ameanza kutupia mabao akianza dhidi ya mabingwa watetezi Mlandege ambapo timu yake ilishinda mabao 3-1, na amefanya hivyo pia dhidi ya Azam FC walipoambulia sare ya bao 1-1.
Mabao anayoyatupia yameibua mijadala, huku Ofisa Habari wa Singida Black Stars, Hussein Massanza, akisema moto alioanza nao mshambuliaji huyo unamkumbusha Sowah alipokuwa pamoja na timu hiyo.
Guede, ambaye amerejea kwa mara ya pili Singida Black Stars, ambayo ilimalizana naye baada ya kuitumikia kwa miezi mitano msimu wa 2024/25, ameliambia Mwanaspoti kuwa aling’oka Ligi Kuu Bara kutokana na majeraha.
UBORA UMEMREJESHA
Mengi yalizungumzwa baada ya kuondoka Singida Black Stars, wengine wakiweka wazi kuwa ametolewa kwa mkopo kutokana na kushindwa kuonyesha kile kilichokuwa kinatarajiwa baada ya kujiunga na Singida Black Stars akitokea Yanga, ambayo aliitumikia nusu msimu. Amesema ubora umemrudisha Tanzania.
“Sikuwa bora mara baada ya kutua Singida Black Stars kutokana na kuandamwa na majeraha, ambayo ndiyo yaliniondoa Tanzania. Mara baada ya kurudi nchini kwetu nilijitibia na baadaye nikapata timu, kile nilichokifanya nikiwa huko ndicho kimenirudisha Tanzania,” anasema na kuongeza:
“Ubora wa mchezaji, hasa mshambuliaji, ni kutumia nafasi anazotengenezewa au kutengeneza mwenyewe. Ndicho ninachokifanya nikiwa Singida Black Stars, nafurahi nimeanza vizuri, malengo yangu ni kufunga kila nitakapopata nafasi.”
Guede anasema anaifahamu Ligi ya Tanzania, anatambua ubora na madhaifu yake, hivyo uzoefu alionao unamuongezea chachu ya kushindana na anaamini akifuata misingi yote aliyoipata akiwa Yanga na baadaye Singida atafikia malengo.
MZIZE NI HATARI
Licha ya kucheza muda mchache Ligi Kuu Bara akiwa ndani ya kikosi cha Yanga na sasa Singida Black Stars, Guede amemtaja Mzize kuwa ndiye mchezaji anayemvutia.
“Navutiwa na uchezaji wa Mzize kwenye nafasi ya ushambuliaji, ni mchezaji mpambanaji na amekuwa hakoki kupambania anachokifanya,” anasema Guede.
“Ni mchezaji mpambanaji, hakati tamaa. Navutiwa naye licha ya kukosa mabao, amekuwa akipambana na kuhakikisha anafikia malengo yake. Hili linalozungumzwa juu yake anastahili.”
Wakati huohuo, Guede amesema mbali na Mzize anavutiwa pia na uchezaji wa Fei Toto, licha ya kucheza eneo la kiungo, amekuwa bora kwenye umaliziaji na anastahili kuwa mfungaji bora ndani ya Azam FC.
“Sio bahati mbaya kwake kumaliza mfungaji bora ndani ya kikosi cha Azam FC, anastahili. Amekuwa akijituma, ni bora kwenye eneo la umaliziaji na pia ni mpambanaji,” anasema.
BANGALA AMVUTA YANGA
Yanga ilikuwa na wakati mgumu kusaka mbadala wa Fiston Mayele muda mfupi baada ya kufanya biashara ya kumuuza staa huyo kwenda Pyramids FC, baadaye wakamtambulisha Guede akiwa mchezaji huru.
Mwanaspoti lilithibitishiwa na staa huyo kuwa kabla ya kutua ndani ya Yanga alikuwa anaifahamu timu hiyo kupitia staa wake wa zamani Yanick Bangala, ambaye kwa sasa anakipiga Azam FC.
“Yanga ni timu kubwa Afrika, nilipokuwa nacheza nchini Morocco nilikuwa naisikia timu hiyo, nakumbuka wakati huo nilikuwa na Bangala timu moja,” anasema na kuongeza:
“Tulipokuwa Morocco kwenye timu ya FAR Rabat ndipo Bangala alipata nafasi ya kujiunga na Yanga, hivyo haikuwa ngeni kwangu.”
YANGA ALITIMIZA NDOTO
Licha ya kucheza kwa kipindi cha miezi sita ndani ya kikosi cha Yanga akijiunga dirisha dogo la usajili, Guede anasema ameandika alama ndani ya timu hiyo kwa kutimiza ndoto ya Watanzania wengi.
“Ni kweli nimecheza kwa muda mfupi sana ndani ya kikosi cha Yanga, lakini nina kumbukumbu nzuri ambayo ni mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya CR Belouizdad,” anasema na kuongeza:
“Bao nililofunga ambalo lilikuwa la uamuzi wa Yanga kutinga hatua inayofuata lilinipa nguvu na kunifanya niwe mchezaji mwenye bahati baada ya kucheza muda mchache na kuwafurahisha Watanzania walio wengi.”
Guede anasema mchezo huo ndio umekuwa bora kwake na upo kwenye kumbukumbu zake za uchezaji soka Tanzania ndani ya sekunde chache.
14 NI THIERRY HENRY
Kila mchezaji amekuwa akivaa jezi yenye namba mgongoni kama sheria ya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) inavyotaka, hivyo kwa upande wa Guede anayekipiga Singida Black Stars amethibitisha kwanini anavaa jezi namba 14.
“Navaa jezi namba 14 kwa sababu mimi ni shabiki wa Thierry Henry aliyekuwa mshambuliaji wa zamani wa Arsenal, ni mshambuliaji wangu bora katika historia ya wanasoka,” anasema na kuongeza:
“Nilikuwa navutiwa sana na mshambuliaji huyo na nimejifunza mambo mengi kutoka kwake. Hiyo ndiyo sababu kubwa ya mimi kuvaa jezi namba 14 na ndiyo jezi yangu pendwa tangu nimeanza kucheza soka la ushindani.”
YANGA NI STORI NDEFU
Licha ya ubora aliokuwa nao ndani ya miezi sita aliyocheza akiifungia mabao sita kwenye ligi na kuivusha timu hiyo hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika akiifunga CR Belouizdad, na uongozi kuamua kuachana naye, Guede amesema ni mambo mengi yametokea hawezi kuyaweka wazi yote, bado anawapenda wananchi.
“Yanga ni mengi sana yametokea na wengi hawafahamu sababu iliyofanya niondoke. Naomba iendelee kuwa hivyo kwa sababu sipendi kuweka wazi sababu hizo, kwa kuwa nawaheshimu sana wananchi walinipokea vyema na kunipa sapoti,” anasema na kuongeza;
“Nilikuwa na muda mfupi ndani ya Yanga lakini nilifanikiwa kupata marafiki ambao niliishi nao vizuri, lakini hayo yote yamepita, ni sehemu ya maisha ya mpira. Leo nipo Singida Black Stars nafurahia maisha ya huku, kitu ambacho ni muhimu zaidi kwa sasa,” anasema.
TOFAUTI YA YANGA, SINGIDA
Amekipiga miezi sita tu ndani ya Yanga na sasa yupo Singida Black Stars, mshambuliaji huyo amesema kuna tofauti kubwa kati ya timu hizo mbili.
“Yanga tayari ni timu kubwa Afrika, imethibitisha kwa kucheza mashindano makubwa na mataji waliyotwaa ndani ya nchi. Singida Black Stars tuna safari ndefu na muhimu zaidi ni mwaka huu kuhakikisha tunafikia malengo tuliyojipangia mwanzoni mwa msimu,” anasema na kuongeza;
“Naamini tuna uwezo wa kufanya mambo makubwa ndani ya timu hii, hata kama kuna watu hawaamini hilo. Ni timu ambayo tayari imejizatiti na uongozi umewekeza nguvu kubwa kuhakikisha tunafikia malengo.”
Anasema Singida Black Stars ni timu nzuri ambayo itafanya mambo makubwa msimu huu, na mipango yao ni kuhakikisha wanamaliza nafasi nne bora kwenye msimamo, ana imani kubwa na kikosi kilichopo sambamba na benchi la ufundi walilonalo.
MASTAA KUTUA LIGI KUU
Kumekuwa na ongezeko la mastaa kutoka mataifa mbalimbali kutua Tanzania kwa ajili ya kucheza Ligi Kuu Tanzania Bara, Guede amefunguka sababu kuwa ni uwekezaji, ukaribu wa Watanzania na hamasa iliyopo kwenye ligi.
“Soka la nchi hii limekuwa likizungumzwa mataifa mbalimbali pamoja na sifa za nchi husika, ikiwa ni pamoja na uwekezaji mkubwa uliofanywa kwenye mpira, hamasa iliyopo, wananchi wake kuwa na mapenzi na mpira, pia Shirikisho la Soka limekuwa likiruhusu mataifa mengine kuja kucheza,” anasema.
“Mpira ni ajira, nchi ikiwa na uwekezaji mzuri hakuna mtu ambaye anaweza kusita kujumuika kuja kucheza ili kufikia malengo. Nafikiri hayo ni baadhi tu, kuna mengine mengi.”