Fountain Gate inavyotaka kuzalisha vipaji 32 Ligi Kuu
Muktasari:
- Chuga alijiunga na akademi ya Fountain Gate akiwa na kati ya miaka 11 au 12 na kupitia malezi ya takribani miaka saba kabla ya kufikia hatua ya kucheza soka la ushindani. Baadaye alihamia Yanga, ambako alipata fursa ya kuonyesha uwezo wake.
KUNA wachezaji wanaosajiliwa kwa mamilioni ya fedha baada ya kung’ara ndani ya muda mfupi. Hata hivyo, nyuma ya mafanikio yao kuna safari ndefu ya malezi, uvumilivu na uwekezaji ambao mara nyingi hauonekani.
Kwa Fountain Gate, safari ya Chuga ni miongoni mwa mifano inayotaka kuitumia kuonyesha matunda ya mfumo wake wa kukuza vipaji.
Chuga alijiunga na akademi ya Fountain Gate akiwa na kati ya miaka 11 au 12 na kupitia malezi ya takribani miaka saba kabla ya kufikia hatua ya kucheza soka la ushindani. Baadaye alihamia Yanga, ambako alipata fursa ya kuonyesha uwezo wake.
Hata hivyo, safari yake haikuishia hapo. Rais wa Yanga, Hersi Said, ametangaza kuwa mchezaji huyo anakwenda kuendeleza maisha yake ya soka nje ya nchi. Hatua hiyo inaonyesha namna malezi ya vipaji yanavyoweza kuwa uwekezaji wenye matokeo makubwa kwa klabu inayovilea.
Ndiyo maana Fountain Gate sasa inataka kuongeza nguvu katika mfumo wake wa kukuza vijana, ikiwa na azma ya kuzalisha wachezaji 32 watakaoweza kucheza Ligi Kuu, huku ikijenga msingi wa biashara kupitia mauzo ya vipaji vyake kwa klabu nyingine.
Mkakati huo unalenga kuanzia kwa watoto wadogo, kuwalea katika hatua mbalimbali za maendeleo na hatimaye kuwafikisha kwenye timu ya wakubwa au kuwapeleka kwenye klabu nyingine zenye ushindani mkubwa. Kupitia programu ya Kid Soccer, Fountain Gate inatoa mafunzo kwa watoto wenye umri wa miaka mitatu hadi 17 katika maeneo ya Tabata jijini Dar es Salaam, Morogoro, Mwanza, Manyara, Arusha na Dodoma.
Ofisa Habari wa klabu hiyo, Issa Liponda a.k.a Mbuzi, anasema mfano wa Chuga unaonyesha kuwa mafanikio katika uzalishaji wa wachezaji hayawezi kupatikana kwa haraka, bali yanahitaji uwekezaji wa muda mrefu.
“Kukuza mchezaji ni mchakato mrefu. Chuga alijiunga akiwa na miaka 11 au 12, lakini sasa ana miaka 18. Hiyo inaonyesha kwamba kuna muda ambao tunautumia kumlea na kumjenga mpaka kufikia kiwango alichopo,” anasema Mbuzi.
Anaongeza kuwa lengo lao si kuwa na akademi inayokusanya watoto kwa ajili ya kucheza mpira pekee, bali kujenga mfumo unaoweza kuzalisha wachezaji wa kiwango cha juu watakaokuwa na uwezo wa kuitumikia Fountain Gate na klabu nyingine kubwa.
“Tunataka kujenga mfumo ambao utakuwa unatuzalishia wachezaji wetu wenyewe. Hatutaki akademi iwe sehemu ya watoto kucheza mpira tu, bali kuandaa wachezaji ambao baadaye watacheza timu ya wakubwa,” anasema.
Kwa Fountain Gate, safari ya Chuga ni mfano wa kile inachotaka kukifanya kwa vijana wengi zaidi, huku lengo likiwa kuona uwekezaji wa akademi unazaa wachezaji wenye thamani ndani na nje ya Tanzania.
Issa Mbuzi anaeleza kuwa wameamua kuwekeza katika soka la vijana kwa sababu wanaamini mafanikio ya muda mrefu yanahitaji kujenga msingi wa wachezaji wao wenyewe badala ya kutegemea usajili kila wakati.
“Tunataka kujenga mfumo ambao utakuwa unatuzalishia wachezaji wetu wenyewe. Hatutaki akademi iwe sehemu ya watoto kucheza mpira tu, bali iwe sehemu ya kuwaandaa wachezaji ambao baadaye wataweza kucheza kwenye timu ya wakubwa,” anasema.
MIAKA MITATU HADI 17
Katika kuhakikisha inajenga msingi imara wa vipaji, Fountain Gate imeanzisha programu inayowahusisha watoto wenye umri wa miaka mitatu hadi 17, ikiwa na vituo katika maeneo mbalimbali nchini.
“Tuna Kid Soccer Program ambayo inahusisha watoto kuanzia miaka mitatu hadi 17. Tumeipanua katika maeneo mbalimbali kwa sababu tunataka watoto wengi wapate nafasi ya kujifunza na kukuza vipaji vyao,” anasema Issa Mbuzi.
CHUGA MFANO
Mbuzi anasema Chuga amepitia takribani miaka saba ya mafunzo, jambo linaloonyesha kuwa haiwezekani kutarajia mtoto anayejiunga na akademi kufikia kiwango cha kucheza soka la ushindani muda mfupi.
“Kukuza mchezaji ni mchakato mrefu. Chuga alijiunga akiwa na miaka 11 au 12, lakini sasa ana miaka 18. Hiyo inaonyesha kwamba kuna muda ambao tunautumia kumlea na kumjenga mpaka kufikia kiwango alichopo,” anasema.
WANANE TIMU YA WAKUBWA
Moja ya matokeo yanayoonyesha uwekezaji wa Fountain Gate katika soka la vijana ni kuwa na wachezaji wanane waliotoka kwenye akademi na kujiunga na kikosi cha kwanza cha timu ya wanaume inayoshiriki Ligi Kuu.
Wachezaji hao ni Machupa Juma Kapili, ambaye ni kipa; Ahmad Ramadhan Ahmad Kasuku, anayecheza beki namba mbili; Juma Mgunda, anayecheza kiungo namba sita; na Alois Obadia, anayekipiga namba nane.
Wengine ni Hashimu Omari Kindemile, anayecheza nafasi ya mshambuliaji; Said Ramadhani, anayecheza namba 10; pamoja na winga Jumanne Ramadhani na Abdurrazaki Salum.
“Tayari tuna wachezaji wanane ambao wametoka kwenye akademi na wamefika kwenye timu ya wakubwa. Hilo ni jambo muhimu kwetu kwa sababu tunataka vijana wetu wapate nafasi ya kuonyesha uwezo wao katika kiwango cha juu,” anasema.
“Kwa sasa tunakadiria kuwa tumefikia takribani asilimia 60. Lengo letu ni kufika asilimia 100, kwamba timu yetu iwe na wachezaji ambao wamepitia kwenye mfumo wetu wenyewe,” anasema.
Mbali na kuzalisha wachezaji kwa ajili ya timu ya wakubwa, Fountain Gate inaangalia namna ya kuifanya akademi kuwa chanzo cha mapato kwa klabu.
“Tunataka tuweze kuzalisha wachezaji ambao hawatacheza kwenye timu yetu pekee. Wengine waweze kwenda kwenye timu kubwa ndani na nje ya nchi. Hapo ndipo tunaweza kuona faida ya uwekezaji tunaoufanya,” anasema Mbuzi.
Katika kutafuta vipaji na kuvipa nafasi ya kuonekana, Fountain Gate imekuwa ikiendesha mashindano ya Fountain Gate Academy Scouting Tournament.
Kupitia mashindano hayo, klabu ilimwalika skauti kutoka Ubelgiji, Mr Dick ambaye alifanya tathmini ya vijana na kuchagua wachezaji 20.
Hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa kutafuta vipaji vipya na kuvipa nafasi ya kuonekana kwa wadau wa soka wa kimataifa.
Issa Mbuzi anasema;”Tumekuwa tukifanya mashindano maalumu ya kutafuta vipaji. Tulimwalika skauti kutoka Ubelgiji ambaye alikuja kufanya tathmini na aliweza kuchagua vijana 20.”
NYOTA 32
Anasema Fountain Gate ina lengo la kufikia hatua ambayo angalau wachezaji wawili waliotoka kwenye akademi yake watakuwa sehemu ya kila timu inayoshiriki Ligi Kuu Bara ndani ya miaka mitano ijayo.
“Tunataka ndani ya miaka mitano tuwe na angalau wachezaji wawili waliotoka kwenye akademi yetu katika kila timu ya Ligi Kuu. Hilo litakuwa jambo kubwa kwetu kwa sababu litakuwa linaonyesha kuwa mfumo wetu unazalisha wachezaji wanaoweza kucheza katika kiwango cha juu,” anasema.
MIUNDOMBINU, VYUO
Katika kuhakikisha vijana wanapata mazingira bora ya mafunzo, Fountain Gate imeendelea kuwekeza katika miundombinu.
Morogoro wanaendelea na ujenzi wa uwanja mkubwa wa kisasa, Tabata wana uwanja wa Seven-Aside, huku Dodoma wakiwa na viwanja viwili, Fountain Gate Arena wenye taa za usiku na Gates Arena wenye nyasi za kisasa ulioanza kutumika mwaka huu.