Dorothea: Nilipigana na wanaume na sasa nina ndoto ulingoni
Muktasari:
- Dorothea ni mmoja wa mabondia wa kike wanaojitengenezea njia katika mchezo ambao kwa muda mrefu ulionekana kuwa wa wanaume zaidi.
MIONGONI mwa mabondia walioanza kupata umaarufu hivi karibuni ni Dorothea Teddy Moza maarufu kama ‘Malkia wa Uswazi’, alipachikwa jina hilo na mashabiki zake wa mitaa ya Gongo la Mboto.
Dorothea ni mmoja wa mabondia wa kike wanaojitengenezea njia katika mchezo ambao kwa muda mrefu ulionekana kuwa wa wanaume zaidi.
Kwenye mahojiano na Mwanaspoti Dorothea anasema aliamua kuuchagua mchezo huo kwa sababu aliupenda kutoka moyoni.
“Nilikuwa naupenda tu mchezo wa ngumi muda mrefu lakini kwenye familia zetu wanachukulia kama mchezo wa kihuni,” anasema Dorothea.
PAMBANO LAKE NA DEBORA
Moja ya mapambano yaliyompa umaarufu zaidi ni lile la Dar Boxing Derby dhidi ya bondia Debora Mwenda, pambano lililokuwa na ushindani mkubwa na mwanadada huyo alishinda kwa kura za majaji wote wawili.
Akizungumzia pambano hilo, Dorothea anaamini ushindi wake ulitokana na kazi aliyofanya ndani ya ulingo na siyo msaada wowote.
“Pale hakuna upendeleo wala nini. Kila mmoja aliona nilivyopambana kuanzia mwanzo na majaji pia wanajua kilichotokea. Nilipanda ulingoni kufanya kazi yangu na nilipambana kwa uwezo wangu wote,” anasema Dorothea.
Bondia huyo anasema hivi sasa kila pambano analocheza ni nafasi ya kuonyesha uwezo wake na kuthibitisha kuwa wanawake wanaweza kufanya vizuri katika mchezo wa ngumi.
SAFARI YA NGUMI
Dorothea alianza rasmi safari yake ya ngumi mwaka 2019, lakini mwanzo wa safari hiyo haukuwa mwepesi. Familia yake haikufurahishwa na uamuzi wa kuingia kwenye mchezo huo kutokana na hofu ya usalama wake.
Anakumbuka jinsi wazazi wake walivyokuwa wakimshauri achague mchezo mwingine ambao waliona ungekuwa na nafuu kwake.
“Familia yangu ilikataa mwanzo. Walikuwa wanauliza mchezo gani huu? Walisema labda nicheze mchezo mwingine kwa sababu ngumi ni hatari lakini jitihada zangu zimewafanya hadi leo wanikubali na kunisapoti,” anasema.
Dorothea anasema kikubwa alichofanya ni kuwas hawishi wazazi wake kwa vitendo kuwa anaweza kucheza ngumi kwa kuwa ni ndoto yake ya muda mrefu.
RONDA ROUSEY
Dorothea anasema bondia ambaye alikuwa anamvutia na kumfuatilia ni Ronda Rousey raia wa Marekani ambaye ana rekodi mbalimbali kimataifa.
Anasema anamfuatilia bondia huyo kuanzia ulingoni na maisha yake nje ya Ndondi ambayo yamekuwa yakimvutia na kutamani siku moja kufikia levo yake.
“Ronda Rousey nampenda na kumfuatilia jinsi anavyofanya vizuri ulingoni ananipa hamasa ya kuona mwanamke ana weza kufika mbali kwenye michezo ya migumu kama ngumi,”€ anasema.
MAISHA YA MITAANI
Kama ilivyo kwa wanamichezo wengi wanaochagua njia ambayo si ya kawaida, Dorothea amekutana pia na maoni tofauti kutoka mtaani kwake.
Anasema baadhi wanampa moyo na wengine wanamkatisha tamaa, lakini aliamua kuendelea kuchagua kile anachok ipenda.
“Maneno ya binadamu hayaishi. Mwin gine akikuona anakupenda anakupa moyo uendelee na unachofanya, mwin gine anaku om bea mabaya kwamba hutafika popote,”€ anasema.
Anasema mwanzoni baadhi ya watu walimshangaa kuona anachagua ngumi huku wengine wakimuogopa lakini kadri walivyoendelea kumuona akifanya mazoezi na kushiriki mapambano, walimzoea
CHANGAMOTO YA KUFIKA KIMATAIFA
Dorothea anasema bado hajafanikiwa kufika anapopata kwani anatamani kwanza kuwa bondia namba moja Tanzania kisha kushindania mataji mengine kimataifa.
Anasema changamoto kubwa kwake kwa sasa ni ukosefu wa fursa za kimataifa na kutokuwa na meneja anayemsimamia vizuri.
“Sijafika ninapopahitaji sijawahi kucheza pambano la nje hata ndani bado sina rekodi nzuri. Wakati mwingine napata mechi jirani tu Uganda, lakini sina meneja wa kuniangalia hiyo ndiyo changamoto kubwa,” anasema.
Anaamini akipata promota au mtu wa kumsogeza mbele, ana uwezo wa kupigania heshima ya Tanzania kimataifa akiamini ana uwezo wa kufanya vizuri.
NJE YA NGUMI
Bondia huyo anasema ngumi bado hazijamlipa kiasi cha kusema kila anachofanya sababu imetokana na ngumi.
Dorothea anasema kuwa ngumi pekee hazitoshi kumuwezesha kuishi. Nje ya ulingo, anafanya kazi kwenye saluni ili kujipatia kipato cha kusaidia maisha yake ya kila siku.
“Nipo kwenye saluni nasuka tu watu, najipatia riziki ndogondogo maana huwezi kutegemea ngumi tu ambazo unapigana kwa mwaka mara tatu hadi nne,”€ anasema.
Anasema ngumi zinaweza kulipa kwa baadhi ya mabondia, lakini kwake bado hajafikia hatua ambayo anaweza kusema amepata maendeleo makubwa kifedha kupitia mchezo huo.
PAMBANO HILI HASAHAU
Pambano ambalo hatalisahau kwenye maisha yake na lilimpa somo kubwa ni dhiti ya bondia Jesca Mfinanga ambapo alipoteza kwa KO.
Anasema siku hiyo hakuwa katika hali nzuri kiafya na hakucheza kama wengi waliofahamu uwezo wake.
“Nilikuwa sipo sawa, nilikuwa naumwa ndiyo maana sikucheza vizuri. Lakini nataka kurudiana naye hata leo na naamini safari hii hatoboi,” anasema kwa kujiamini.
SIKU YA KWANZA ULINGONI
Dorothea anasema pambano lake la kwanza lilikuwa gumu kwani hakuwa anajua chochote kuhusu mchezo huo zaidi ya kurusha mikono tu.
“Nilipopanda kwenye ringi sikuwa naelewa nini nafanya. Sikujua maana ya jab wala fight, Nilikuwa narusha mikono tu na kukimbia hadi raundi nne zikaisha,” anakumbuka bondia huyo.
Anasema alikuwa amefanya mazoezi kwa wiki mbili tu kabla ya pambano hilo, lakini baada ya kuona maumivu na ugumu wa mchezo huo, aliamua kuanza kujifunza na kuujua vizuri zaidi.
Dorothea anasema tangu akiwa mtoto alikuwa na tabia ya kupenda kupigana na wenzake hata watoto wa kiume wakimchokoza alikuwa na uwezo wa kuwapiga.
“Nilikuwa mkorofi sana nilikuwa napigana hata na watoto wa kiume kwa hiyo hata ngumi ni kama nafanya mwendelezo tu wa utoto wangu,” anasema.
Kwa sasa tabia hiyo ya utoto imegeuka kuwa kipaji kinachompa nafasi ya kutengeneza jina kwenye ngumi.