Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

CFFA; Kutoka kulea vipaji hadi kusaka historia kwa Yanga CAF

CFFA Pict

Muktasari:

  • Matokeo hayo yamekuja baada ya mchezo wa kwanza ugenini Yanga kulazimisha sare ya bao 1-1, kisha nyumbani kushinda 2-1.

YANGA imefuzu hatua ya pili ya mchujo katika Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya juzi Jumamosi kuiondosha Gaborone United kwa jumla ya mabao 3-2.

Matokeo hayo yamekuja baada ya mchezo wa kwanza ugenini Yanga kulazimisha sare ya bao 1-1, kisha nyumbani kushinda 2-1.

Ushindi huo wa Yanga ni mwendelezo wa kikosi hicho kufanya vizuri katika mashindano ya CAF kwani tangu msimu wa 2022-2023 ilipocheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, imekuwa na wakati mzuri huku misimu yote iliyofuatia ikiwafanikiwa angalua kucheza makundi.

Baada ya fainali ya 2022-2023 ilipopoteza kwa USM Alger kufuatia kanuni ya bao la ugenini ilipofungwa nyumbani 2-1 na ugenini kushinda 1-0, 2023-2024 ikacheza robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, kisha 2024-2025 na 2025-2026 ikakwamia makundi ya michuano hiyo.

Hesabu za Yanga hivi sasa ni kucheza tena robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika ilipoishia msimu wa 2023-2024, kisha kusonga mbele zaidi ya hapo jambo ambalo haiwezi kufika huko kama haitaitoa CFF Andoharanofotsy kutoka Madagascar ambayo ndiyo mpinzani wake ajaye.

Usiitazame CFF kama jina geni tu katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, kwani timu hiyo ya Madagascar imejenga historia yake kutoka kuwa kituo cha kulea vipaji hadi kuwa moja ya timu zinazowania ubingwa nchini humo, sasa ikiwa mbele ya safari ngumu ya kuikabili Yanga.

CFFA ndiyo mpinzani wa Yanga katika raundi ya pili ya mchujo wa Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2026-2027, hatua ambayo mshindi wa jumla wa mechi mbili atafuzu moja kwa moja kwenda makundi.

Mechi hizo zinatarajiwa kuchezwa kati ya Oktoba 16 na 18, 2026 kwa mchezo wa kwanza na Oktoba 23 na 25, 2026 kwa marudiano, huku CFFA ikiingia kwenye vita hiyo ikiwa na hamu kubwa ya kuandika historia mpya kwenye soka la Afrika.


CF 04

KUTOKA KITUO CHA VIJANA

Jina kamili la timu hiyo ni Centre de Formation de Football d’Andoharanofotsy, ikiwa na makao yake Andoharanofotsy, Wilaya ya Antananarivo-Atsimondrano, mkoani Analamanga nchini Madagascar.

Kama jina lake linavyoashiria, CFFA ilianza kama kituo cha kulea na kuendeleza vipaji vya vijana, lakini hatua kwa hatua imekua na kuwa klabu yenye ushindani mkubwa katika soka la Madagascar.

Chini ya uongozi wa Rais Tota Henintsoa Rakotoarimanana, klabu hiyo imeendelea kujijenga na kufanikiwa kuvuka mipaka ya soka la ndani. Benchi la ufundi la CFFA limewahi kuwa chini ya makocha mbalimbali akiwemo Franck Rajaonarisamba na Titi Rasoanaivo.


MABINGWA MARA MBILI

CFFA si timu inayokwenda kuikabili Yanga ikiwa na historia ndogo ndani ya Madagascar.

Timu hiyo imewahi kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Madagascar mara mbili, ikifanya hivyo katika misimu ya 2021-2022 na 2025-2026.

Msimu uliopita, CFFA ilitwaa ubingwa baada ya kuifunga AJESAIA (AJSA Inter-arrondissement) mabao 2-1 katika fainali iliyochezwa kwenye Uwanja wa By-pass.

Kabla ya hapo, mwaka 2021, ilitwaa pia Kombe la Madagascar baada ya kuifunga CNaPS Sport mabao 3-1 kwenye fainali.

Hivyo, Yanga itakutana na timu inayokwenda kwenye mechi hizo ikiwa na morali ya ubingwa wa ndani na kiu ya kuendeleza mafanikio yake kimataifa.


CF 02

USHIRIKI WAO CAF

Safari ya CFFA katika mashindano ya CAF si ya muda mrefu sana. Ilianza kushiriki katika Kombe la Shirikisho Afrika msimu wa 2021-2022, ambapo katika raundi ya kwanza ya mchujo iliiondoa Kabwe Warriors ya Zambia.

Baada ya kutoka sare ya 0-0 nyumbani, CFFA ilishinda 2-1 ugenini na kusonga mbele kwa jumla ya mabao 2-1.

Hata hivyo, safari yao ilikwamia raundi iliyofuata walipokutana na GD Interclube ya Angola.

CFFA ilipoteza mchezo wa kwanza nyumbani kwa mabao 3-0, kabla ya kushindwa kucheza mechi ya marudiano baada ya kujitoa kutokana na changamoto za kifedha na usafiri.

Timu hiyo pia ilishiriki raundi za mchujo za Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2022-2023. Hata hivyo, hadi sasa haijawahi kufika hatua ya makundi ya michuano ya CAF, huku hatua ya pili ya mchujo ikiwa ndiyo imekuwa mafanikio yake makubwa.


KAZI IPO

CFFA imefika hatua hii baada ya kuanza kampeni yake ya Ligi ya Mabingwa msimu huu dhidi ya Lijabatho FC ya Lesotho.

Katika mchezo wa kwanza uliochezwa nyumbani Septemba 5, 2026, CFFA ilishinda 2-0, kabla ya kwenda Lesotho na kulazimisha sare ya 1-1, Septemba 12, 2026. Kwa matokeo hayo, CFFA imefuzu kwa jumla ya mabao 3-1. Kwa upande wa Yanga, ilianza safari yake dhidi ya Gaborone United ya Botswana na kupata sare ya 1-1 ugenini. Katika mchezo wa marudiano, Yanga ilishinda 2-1 na kusonga mbele kwa jumla ya mabao 3-2.

Sasa timu hizo zinakutana kwenye raundi inayofuata huku kila moja ikiwa na sababu yake ya kutaka kuvuka kuingia makundi.


CF 03

YATAMANI HISTORIA

CFFA kwao hatua hii ni zaidi ya mechi mbili. Ni nafasi ya kuandika historia kwa kufuzu kwa mara ya kwanza hatua ya makundi ya michuano ya CAF. Timu hiyo inaingia ikiwa na nguvu ya ubingwa wa Madagascar uliopatikana msimu uliopita, pamoja na matokeo mazuri iliyoyapata katika raundi ya kwanza dhidi ya Lijabatho.

Hata hivyo, mbele yao kuna Yanga, timu yenye uzoefu mkubwa zaidi katika mashindano ya kimataifa, ambayo imekuwa ikishiriki mara kwa mara hatua za juu za michuano ya CAF.

Yanga pia inaingia kwenye hatua hiyo ikiwa miongoni mwa timu zenye viwango vya juu zaidi barani Afrika, jambo linaloifanya kuwa na faida kubwa upande wa uzoefu na ubora wa kikosi.

CFFA bila shaka mpango wao utakuwa ni kutumia mchezo wa nyumbani kupata matokeo yatakayowapa nafasi nzuri kabla ya kwenda kwenye mchezo wa marudiano kama ilivyofanya hatua ya kwanza na kufanikiwa.


CF 01

VITA YA HESHIMA

Kwa upande wa Yanga, mchezo huo utakuwa vita ya kulinda heshima yake katika soka la Afrika na kuhakikisha inaendelea na safari yake ya kutafuta nafasi ya hatua ya makundi. Kwa CFFA, ni fursa ya kuvunja ukuta uliowazuia kwa miaka yote na kuingia kwa mara ya kwanza kwenye hatua hiyo ya makundi.

Yanga inaonekana kuwa na uzoefu na ubora mkubwa zaidi, huku CFFA ikiwa timu changa, lakini katika mchezo wa mpira wa miguu lolote linaweza kutokea.