MAUMIVU ya mapenzi ukiyasikia kwa anayepitia hali hiyo, unaweza ukamchukulia kama mzembe na anajiendekeza, lakini siku ukiipitia utajua uhalisia wake.
Katika stori za hapa na pale Nyuma ya Kamera na msanii wa Bongo Fleva, Rashid Said 'Bright', anasema kabla ya kuumizwa, alikuwa anashangazwa na watu wanaojiua au kuua kisa mapenzi, lakini lilipomfika tukio alielewa hali halisi wanayoipitia watu.
Anasimulia miongoni mwa matukio ya kuumizwa kimapenzi, yaliyoacha alama ya funzo la kuwa na kiasi cha kumpenda mtu na kuacha nafasi kubwa ya kumtanguliza Mungu, ili ikitokea yakaisha asiwe na maumivu makubwa, yanayoweza kuleta madhara.
Anakumbuka mwaka 2015 alikuwa na mchumba, aliyekuwa anamhudumia kila kitu na kutoa msaada kwenye familia ya msichana huyo, hakutegemea ingefika siku akageukwa vibaya tena kwa simu bila sababu yoyote.
"Baada ya kuhitimu masomo yake ya kidato cha sita, alitakiwa kupitia jeshini kwenye mafunzo ya uzalendo kisha akajiunge chuo, nilifanya kila kitu cha safari yake, sikutaka kuacha nafasi ajione ni mpweke au anakosa msaada, hivyo nilisimama kama mwanamume katika jukumu la kumhudumia, nilikuwa namchukulia kama mke wangu mtarajiwa, ndiyo maana nilikuwa na kila sababu ya kumsapoti katika hatua zake za elimu, nilijua yeye akisoma zaidi itakuwa manufaa kwa watoto wetu," anasema Bright na kuongeza;
"Mbali na hilo nilianza kununua baadhi ya vitu vyake vya kwenda navyo chuo, nilijua nisingefanikisha kuvipata kwa wakati mmoja kwani nilijua kipato changu ni cha kuungaunga sana, ujue mwanamume akimpenda mwanamke hawezi kujificha, siyo kitu cha ajabu unaowaona wanakwambia nimemsomesha halafu kanisaliti.
"Penzi letu lilikufa baada ya wiki ya yeye kuwa kambini jeshini ambako alikwenda kupata mafunzo, nakumbuka nilimpigia simu aliyepokea ni mwanamume, aliyeniambia unapiga simu unataka nini kwa mke wa mtu na iwe mwanzo na mwisho sitaki kuona simu zako za usumbufu, nilihisi utani ingawa nilijikuta mwili mzima umepata ganzi, nikawa siamini kilichotokea."
Anasema simu aliyopiga kwa upendo, alijinyima kula na kuweka vocha ili mradi tu kumfurahisha mchumba wake, alidhani akisikia salamu yake angefanya awe na siku nzuri, badala yake yaligeuka majuto na maumivu makali, yaliyodumu kwa takribani mwaka mzima.
"Kitendo cha mwanamume mwenzangu kupokea simu kwa ujasiri, kilitokana na mchumba wangu kumpa nguvu huyo jamaa, naamini alimwambia kuhusu uhusiano wake, kwani hakuwa kichaa wa kupokea simu na kuanza kufoka, angejuaje kama ni simu kapiga kaka yake au ndugu yake, nilipoona hivyo nikakubaliana na kila kitu, lakini niliumia kupita kiasi, nilijitoa sana kwake kumpatia mahitaji yake na kuisapoti familia yake, licha ya kipato changu alikiona kidogo, lakini nilijituma usiku na mchana ili nisimwangushe," anasema Bright na kuongeza;
"Wasichana wengi wana ndoto za kuwa na wanaume wenye vipato vikubwa, hawajui kuna changamoto zake, hicho ndicho kilichomtokea mchumba wangu, maana alimaliza mafunzo ya uzalendo akaenda chuo, baada ya kuendelea na mwanajeshi huyo, akaanza kuona anadharauliwa, haoni thamani niliyokuwa namuonyesha, baadaye akaanza majuto na kuniomba msamaha ili tuarudiane, nilimsamehe ila tayari moyo wangu ukawa na nafasi za watu wengine ya kwake ilikuwa imeishafutika.
"Mwanamume akipenda humwambii kitu, anakuwa tayari kujitolea kwa hali na mali, ndiyo maana unasikia mtu kaua au kujiua pindi anaposhindwa kuhimili maumivu, wanawake wengi wanapokuwa na mtu akifanikiwa analolitaka, anakwenda kwa mtu wa ndoto zake."
Baada ya kupita mwaka mmoja, anasema alianza kujihusisha na mahusiano na watu wazima, ambao walikuwa wanamhudumia kwa kila kitu, ingawa mapenzi hayo anakiri yalikuwa ya mateso na alijiona yupo kifungoni.
"Mwanamke ni mwanamke tu, kula pesa yake inakuwa na masimango, ukitaka kwenda sehemu lazima utoe taarifa na ikubalike, nilikuwa nikipiga picha na mashabiki zangu wanawake unakuwa ugomvi, hapo ndipo nilipotunga wimbo unaoitwa 'King'asti Sugu' ingawa nilikusanya ushuhuda wa wengi ambao wamepitia hali kama yangu," anasema na kuongeza;
"Sababu ya kuachana alinifokea mbele ya watu, hakuishia hapo akaanza kuwaambia yaani huyo jamaa, kila kitu ananitegemea mimi, hakuna analoweza kulifanya mwenyewe, kuanzia kwenye kula, kuvaa, nauli za kwenda mishe zake, kauli zake ziliniumiza sana na kuamsha akili yangu kuanza kupambana.
"Nilijisemea moyoni, mimi bado ni kijana, nina nguvu ya kuyajenga maisha yangu upya, iwaje nianze kupitia maisha ya kuwa chini ya amri ya mtu, nikamwambia mimi na yeye tumefika mwisho, alijua namtania na siwezi kuishi bila kumtegemea yeye, baadaye akaona ni kweli nimeamua na alipokuwa ananitafuta nikawa nampotezea hadi akaacha kunisumbua."
Anasema alishaoa na Mungu amemsaidia kupata watoto wawili, mmoja wa kike na wa kiume: "Tuna miaka mitano kwenye ndoa, namuomba Mungu huyu wa sasa nizeeke naye, ikiwezekana tuje tushuhudie watoto wetu na wao waje kuwa na familia zao.
Anaongeza: "Maumivu yalinikomaza na kunifanya kuwa mtu mwingine, kwa sasa siwezi kuumia kama zamani, badala yake nawekeza nguvu kupambana na kazi, ingawa mke wangu wa sasa nampenda na natamani tufanye vitu vikubwa kwa pamoja kwa maendeleo ya familia yetu."