ATM YA WIKI: Walker pesa zinamfuata

Muktasari:
- Ukiondoa mapito yake na usajili wake wa kutimkia Italia, Walker ambaye amekuwapo katika kikosi cha Man City kwa muda mrefu ni mmoja kati ya wachezaji matajiri ndani ya England kutokana na mshahara wake na miradi mbalimbali anayoendesha nje ya uwanja, leo tumekushushia hapa utajiri anaomiliki na jinsi anavyopiga pesa.
MANCHESTER, ENGLAND: KATIKA dirisha hili la usajili, beki wa Manchester City, Kyle Walker ameachana na timu hiyo kujiunga na AC Milan kwa mkataba wa mkopo wa nusu msimu ikidaiwa anataka kubadilisha mazingira baada ya kumaliza sintofahamu kati yake na mkewe.
Ukiondoa mapito yake na usajili wake wa kutimkia Italia, Walker ambaye amekuwapo katika kikosi cha Man City kwa muda mrefu ni mmoja kati ya wachezaji matajiri ndani ya England kutokana na mshahara wake na miradi mbalimbali anayoendesha nje ya uwanja, leo tumekushushia hapa utajiri anaomiliki na jinsi anavyopiga pesa.

ANAPIGAJE PESA?
Anakadiriwa kuwa na utajiri unaofikia Dola 50 milioni ambao kwa kiasi kikubwa umechangiwa sana na mshahara wake aliokuwa anaupata ndani ya Manchester City tangu ajiunge nayo mwaka 2017 ambako alikuwa akikunja Pauni 150,000 kila wiki.
Mbali ya mshahara, beki huyu amekusanya mkwanja wa kutosha kupitia mikataba yake ya udhamini aliyosaini na kampuni mbalimbali.
Kati ya kampuni ambazo zinamlipa mkwanja mrefu ni Puma. Pia amewekeza hisa katika kampuni mbalimbali ndani ya England.
Kwa mujibu wa tovuti ya Sports Dunia, Kyle anakunja karibia Pauni 4.4 milioni kwa mwaka kutokana na mikataba hiyo mbali ya mshahara wake.
Vilevile anapata pesa kupitia mitandao yake ya kijamii hususani Instagram na TikTok ambako analipwa kwa kila chapisho analoliweka.
MSAADA KWA JAMII
Machi 2024, Walker alianzisha mpango maalumu wa kutoa msaada wa masomo katika chuo cha Sheffield College, ambako amekuwa akisaidia wanafunzi wasio na uwezo wa kipesa gharama za masomo pamoja na mahitaji mengine muhimu.
Vilevile mwaka 2021, beki huyu alitoa msaada wa Pauni 1,000 kwa mtoto mmoja shabiki wa Man City ambaye anasumbuliwa na tatizo la kupooza kwa ubongo. Mchango huu ulimsaidia shabiki huyo kupata msaada wa matibabu na vifaa muhimu.

MJENGO
Anamiliki nyumba yenye thamani ya Pauni 3.5 milioni iliyopo huko Cheshire, England ambako amekuwa akiishi pamoja na mkewe Kilner, ikiwa ni miezi kadhaa baada ya kutengana kutokana na kuthibitika kwamba staa huyo alizaa nje ya ndoa.
Vilevile fundi huyu anajenga mjengo mpya huko kaskazini mwa Jiji la London.
NDINGA ZAKE
Lamborghini Huracan- Pauni 235,000
Bentley Bentayga-Pauni 200,000
Audi RS7, Pauni -115,000
Mercedes AMG-GT R-Pauni £160,000
Mercedes S-Class-Pauni 92,000

MAISHA NA BATA
Kyle Walker amekuwa kwenye uhusiano ya muda mrefu na Annie Kilner, ambaye walifunga ndoa mwaka 2021, ingawa uhusiano wao umekuwa ukipitia changamoto za hadharani, ikiwa ni pamoja na tuhuma za usaliti wa mara kwa mara ambazo zimeleta mvutano hususani hivi karibuni ambako ilitoka taarifa ya Walker kuzaa nje ya ndoa na mrembo Lauryn Goodman. Licha ya hayo, Annie na Walker wamesameheana na kusimama pamoja na kulea familia yao yenye watoto watatu.