Prime
Assinki kwenye mtego mzito Yanga
Muktasari:
- Assinki raia wa Ghana pamoja na uwezo wa juu ambao anao, lakini atakutana na wakati mgumu sana wa kupata nafasi kwenye kikosi cha Yanga kutokana na uwepo wa Dickson JoB na Ibrahim Hamad Bacca ambao wamekuwa wakicheza nafasi hiyo.
Beki wa kati Frank Assinki wiki iliyopita alitangazwa mchezaji mpya wa Yanga akijiunga na timu hiyo kutokea Singida Black Stars kwa mkataba wa mwaka mmoja, hata hivyo ana kazi kubwa ya kufanya ili kupata nafasi.
Beki huyo alionyesha kiwango cha juu akiwa na Singida msimu uliopita ambapo aliiongoza timu hiyo kumaliza nafasi ya nne kwenye Ligi Kuu Bara na kuipa nafasi ya kushiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Assinki raia wa Ghana pamoja na uwezo wa juu ambao anao, lakini atakutana na wakati mgumu sana wa kupata nafasi kwenye kikosi cha Yanga kutokana na uwepo wa Dickson JoB na Ibrahim Hamad Bacca ambao wamekuwa wakicheza nafasi hiyo.
Mabeki hao wa kati tayari wameshaweka ufalme wao kwenye kikosi hicho cha Jangwani na mastaa kibao wameshindwa kuwatenganisha kwenye kikosi hicho, akiwemo nahodha Bakari Nondo Mwamnyeto.
Kabla ya ujio wa Assinki kwenye kikosi hicho mabeki wawili wageni walishatua kwenye timu hiyo na kushindwa kupata nafasi, siyo kwa kuwa hawakuwa na uwezo bali uwepo wa mastaa hao ambao wamekuwa pia panga pangua kwenye kikosi cha Taifa StarS.
Beki, Gift Fred raia wa Uganda ni mmoja kati ya wachezaji ambao walisajiliwa kwenye timu hiyo kwa ajili ya kucheza nafasi hiyo, lakini aliondoka Yanga baada ya kukosa nafasi mbele ya Bacca na Dickson Job.
Pia Yanga iliwahi kumsajili Mamadou Doumbia ambaye alitua kwenye kikosi hicho akitoka kuonyesha kiwango bora katika michuano ya CHAN, huku akipewa sifa kemkem na aliyekuwa kocha wa Yanga, Nasreddine Nabi, lakini bado alishindwa kupata nafasi kutokana na uwepo wa mabeki hao mahiri wazawa ikiwa ndio sehemu pekee ambayo Yanga wamekuwa hawaibadilishi mara kwa mara.
Assinki anatakiwa kuhakikisha anaonyesha uwezo wa juu zaidi ili kumuondoa mmoja kwenye kikosi hicho kama anataka kupata nafasi ya kudumu kwenye timu hiyo, jambo ambalo watangulizi wake wameshindwa.
"Moja ya sehemu ngumu Yanga ni beki wa kati, kihistoria huyo amewahi kucheza pia pembeni lakini kwa mujibu wa mwalimu amemsajili ili acheze katikati akawape upinzani, Bacca na Job, ni kweli kila mmoja anaamini kuwa atakuwa na wakati mgumu, lakini tusubiri tuone atakachofanya mazoezini na kwenye mechi," kilisema chanzo Yanga.
Usajili wa Assinki umemuondoa kwenye mfumo aliyekuwa beki wa kulia wa timu hiyo, Yao Kouassi Atohola siyo kwa sababu ya uwezo bali majeraha ya mara kwa mara, huku akiondolewa kwa lengo la kutimiza kigezo cha wachezaji 12 wa kigeni.
Uwepo wa beki huyo ambaye alicheza michezo mingi akiwa na Singida msimu uliopita akiwa pacha na nahodha, Kennedy Juma, unaifanya Yanga sasa kuwa na wachezaji 12 wa kimataifa wanaotakiwa ambao ni Djigui Diarra, Duke Abuya, Mohammed Douambia, Celestine Ecua, Andy Boyell, Prince Dube, Maxi Nzegeli, Lassane Kouma, Moussa Balla Conte, Chadrack Bocca na Pacome Zouzoua.
Usajili huu unaifanya Yanga kuwa imesajiliwa wachezaji sita wa kigeni kwenye dirisha hili, ikiwa itaanza kuonyesha makali yake kwenye mechi ya Ngao ya Jamii Septemba 16 dhidi ya Simba kabla ya kuanza harakati za michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo itavaana na Wiliete ya Angola hatua ya awali.