Prime
‘Viatu’ vya Shomari Kapombe ni vikubwa, size 52
SHABIKI mmoja maarufu wa Simba huko mitandaoni alinichekesha wiki iliyopita. Alisikika akimwambia mwaandishi wa habari kwamba klabu yake Simba haitakuwa ‘serious’ kama ikimchukua mlinzi wa kulia wa Azam, Nathaniel Chilambo kama mbadala wa Shomari Kapombe.
Chilambo anahusishwa Kwenda Simba. Ni nyakati za uvumi kwa sasa. Ligi inakaribia kumalizika. Ilipaswa kuwa imemalizika lakini tupo katika nchi ya ajabu kidogo. Kombe la dunia litakuwa linachezwa Marekani, Canada na Mexico na bado ligi yetu itakuwa inachezwa Tanzania.
Nilicheka baada ya shabiki wa Simba kudai hivyo. Kwake Chilambo ni mlinzi wa kawaida ambaye hawezi kuvaa viatu vya kapombe. Nilijiuliza, nani anaweza kuvaa viatu vya Shomari kwa sasa? Sawa, Chilambo hawezi, nani anaweza?
Hakuna anayeweza. Ni kweli kwamba kuna wakati unatazama mechi unahisi kwamba miguu inamsaliti Shomari. Msimu uliopita kuna mabao ambayo Simba ilifungwa ukahisi kwamba Shomari alikuwa anawajibika moja kwa moja katika kosa hili na lile. Yote haya kwa sababu tunaamini kwamba labda amechoka. Labda ametumika kwa muda mrefu.
Kama tunaamini katika Wikipedia basi ni kweli kwamba Shomari ana miaka 34. Hata hivyo Shomari wa miaka hii bado anaonekana kuwa bora kuliko walinzi wa kulia wa nchi hii. Naona wazi kwamba nchi inatapatapa katika kumpata mrithi wake. Kuanzia ndani ya klabu yake hadi timu ya taifa.
Ndani ya klabu yake majuzi Simba walianza kumpanga mlinzi wake msaidizi, David Kameta ‘Duchu’. Labda kuna kitu kocha, Steve Berker alikiona kwa Shomari. Ukweli ni kwamba bado hakuonyesha kiwango cha umri wake. Hakuonyesha kiwango wala cha nusu ya kile ambacho Shomari alikuwa anaonyesha katika umri wa Duchu.
Nawatazama walinzi wengi wa kulia ambao ni wadogo zake Shomari. Wapo akina Duchu, Israel Mwenda, Lusajo Mwaikenda na wengineo. Ni wachezaji wazuri lakini pengo baina yao na Shomari ni kubwa.
Upande wa kulia nchi hii hauna vipaji vya ajabu sana. Shomari amevaa ‘viatu’ vikubwa kwao. Inakera kusema hili lakini kama Chilambo hajawaweza kumng’oa Mwaikenda katika nafasi yake anaweza vipi Kwenda kurithi viatu vya Shomari Simba?
Hapo hapo tukubaliane na ukweli kwamba hata katika timu ya taifa hakujawa na beki wa kulia ambaye anaweza kutufikirisha kwamba Kapombe hastahili kuwepo katika kikosi kitakachoanza katika michuano ya Afcon mwakani.
Kuna wakati huwa haitwi katika kikosi lakini akiwa amekaa katika kochi nyumbani kwake bado hauoni beki wa kulia ambaye anavaa viatu vyake vema. Wakati mwingine labda Haji Mnoga anayecheza Uingereza huwa anakaribia lakini ni katika eneo la kulihami lango zaidi na sio kusukuma mashambulizi mbele kama ambavyo Shomari huwa anafanya kwa ufasaha.
Upande wa kushoto rafiki yake aliyecheza naye Simba kwa muda mrefu, Mohamed Tshabalala walau anakabiliwa na upinzani wa hapa na pale ingawa bado yeye ndiye mlinzi bora zaidi wa pembeni upande wa kushoto. Kuna Pascal Msindo wa Azam amekuwa katika kiwango bora.
Kuna Nickson Kibabage ambaye amekwenda kuchukua nafasi yake pale Msimbazi naye pia amekuwa katika kiwango kizuri. Simba hawajayumba sana kumchukua Kibabage kuziba nafasi ya Tshabalala lakini unapofikiria kama kuna mlinzi mzawa wa kulia ambaye anaweza akafanya wasiyumbe kwa kumpa viatu vya Shomari unaona wazi kwamba viatu vinakuwa vikubwa. Size 52.
Nini kinatokea kwa sasa? Ukweli ni kwamba tunajaribu kumsukuma Shomari nje. Ametuchosha machoni kwa sababu amecheza mpira kwa muda mrefu. Hili ndio tatizo kubwa la Watanzania. Hata kama mchezaji bado anacheza katika kiwango kizuri bado tunapenda kumuondoa kwa sababu anakuwa ametuchosha machoni.
Mitaa ya Katikati hapo tulitaka kuwaondoa wote wawili. Shomari na Tshabalala. Baada ya muda ikashindikana na wote wakarudi juu hata katika timu ya taifa. Hata Simba wenyewe sasa hivi wakimtazama Tshabalala pale Yanga wanajua kwamba hajaisha. Ni vile tu kitu kinacholeta unafuu ni kwamba Kibabage amekuwa akicheza vizuri katika nafasi yake.
Nini kifanyike? Ninapotazama mrithi halisi wa Shomari katika nafasi yake natazama nje ya mipaka yetu. Labda kama kuna maajabu ya kumchukua Yao Kouassi kutoka kwa watani zao Yanga basi watakuwa wamepata mrithi sahihi wa upande wa kulia.
Vinginevyo wanaweza kutupa jicho nje. Watani zao kwa muda mrefu wamekuwa wakihangaika kuiziba nafasi hiyo kwa kujaribu wachezaji kutoka nje. Waliwahi Kwenda Kinshasa wakamchukua, Djuma Shabani ambaye licha ya kuanza vema baadae alichuja.
Baadae wakaenda kwa Yao Kouassi ambaye hata hivyo hapo Katikati alikaa nje kwa muda mrefu kutokana na kuwa na majeraha. Sasa hivi amerudi uwanjani na unaona wazi utofauti wake na Mwenda. Kwa walinzi wa pembeni Yanga huwa hawajidanganyi sana nchini. Hata kule kushoto wamewahi kuja akina Joyce Lomalisa ‘Mutambala’, na sasa Chadrack Boka pia anasaidia.
Simba ndio walifanikiwa kwa wazawa. Kipindi kirefu sana Tshabalala na Shomari wameokoa fedha za kuleta walinzi wa pembeni wageni. Lakini baada ya Tshabalala kuondoka naona kuna mchakato wa kuumiza Kichwa kuachana na Shomari.
Tatizo wakitazama hapa nchini sidhani kama wataona sana aliyekaribiana na Shomari. Ni ama wakubali kuendelea na Shomari mpaka pale gari litakaposhindwa kusogea, au walete mlinzi kutoka nje. Ni ukweli ambao unaumiza lakini ndio hali halisi. Kulia kuna shida. Hauwezi kulinganisha sana na ule upande wa Tshabalala na wadogo zake. Kule wanakaribiana japo kwa mita chache.