Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mauaji ya kutisha - Sehemu ya 18

Muktasari:

  • “Hawa watu wanatumia uchawi wa aina gani kuzuia  wasikamatwe?” Akaendelea kujiuliza.

UTANGULIZI

Amour alipoyasikia maelezo hayo alikunja uso akaduwaa kidogo. Kimoyomoyo alikuwa akijiambia watu hao ndio wale wale aliokuwa akiwatafuta. Aliamini moja kwa moja kwamba majambazi waliowakamata na wengine kuwaua hawakuhusika.

“Hii  ni aibu kwa jeshi la polisi,” alijiambia kimoyo  mmoyo.

“Hawa watu wanatumia uchawi wa aina gani kuzuia  wasikamatwe?” Akaendelea kujiuliza.

“Baada ya mtu huyo kumchinja marehemu walifanya nini?” Amour akaendelea kumuuliza maswali yule polisi.

“Ndio wakati  ule tunasimamisha gari. Gari liliposimama tuliwania kutoka ili tuwakamate wale watu lakini hatukuwaona tena.”

“Ni kwanini hamkuwaona wakati walikuwapo mahali hapo?”

“Bila shaka walipotuona tunasimamisha gari walikimbilia msituni. Msitu ulikuwa karibu sana.”

“Una  uhakika kwamba walikimbilia msituni?”

Yule polisi aliyeulizwa alimtazama polisi mwenzake.

“Itakuwa wamekimbilia msituni.” Polisi aliyetazamwa na mwenzake alijibu bila kuulizwa.

“Hamkuweza kuwafuatilia?”

“Hatukujua walikimbilia upande gani. Isitoshe tulikuwa na jukumu jingine la kulinda zile pesa. Tusingeweza kuziacha  na kuingia msituni kuwatafuta.”

SASA ENDELEA


AMOUR aliwaza kidogo kabla ya kumuuliza tena.

“Kulikuwa na gari karibu?”

“Hatukuona  gari yoyote.”

“Sasa unafikiri walifika mahali hapo kwa  kutumia  usafiri gani?”

“Sijui.”

“Baada ya hapo mlifanya nini?”

“Tulipiga simu katika kituo cha polisi cha Chalinze kuwaarifu kuhusu tukio  hilo na tulikaa kuwasubiri hadi polisi hao walipokuja.”

“Vizuri.” Amour alisema na kumtazama yule polisi wa pili.

“Je wewe utakuwa na maelezo ya ziada?”

“Uliuliza kwamba hao watu walifika pale kwa kutumia usafiri gani, inawezekana ni wenyeji wa maeneo ya karibu na pale. Hawakuhitaji kutumia usafiri.”

“Unahisi hivyo?”

“Ndiyo, kwa sababu hata silaha waliyokuwa wakitumia haikuwa bunduki.  Walitumia sime. Inaonesha wale walikuwa majambazi wa vijijini.”

“Uchunguzi wetu umeonesha kwamba hawakuwa wameiba chochote. Mnadhani lengo lao lilikuwa nini?”

“Huenda walitaka kumuibia yule  kijana lakini walishindwa na kukimbia baada ya sisi kutokea.”

“Kuna matukio ya aina ile yaliwahi kutokea hapa Dar na inaaminika wauaji ni hao hao lakini inadaiwa kuwa huenda wanatumia nguvu za kiza zinazowafanya watoweke mbele ya macho ya watu baada ya kufanya tukio. Wewe unakubaliana madai hayo?”

Polisi  hao wakatazamana halafu yule aliyeulizwa akaurudisha uso wake kwa Inspekta Amour.

“Mimi sikubaliani na madai hayo kwa sababu siamini kuwepo kwa  nguvu za kiza.”

“Kwa hiyo  kwa  mawazo yako, wale  wauaji walikimbia lakini hawakutoweka  kwenye macho yenu?”

“Nadhani walikimbia.”

“Unaposema unadhani ina maana huna  uhakika?”

“Sina uhakika kwa sababu hatukuwaona wakiingia msituni.”

“Kwa hiyo basi inawezekana kuwa walitoweka  mbele ya macho yenu?”

“Hilo pia linawezekana.” Polisi wa pili akasema na kuongeza.

“Mimi naamini nguvu za kiza zipo na majambazi wanazitumia sana. Tulishawahi  kukamata majambazi wakiwwa wamefungwa hirizi mikononi na tulipowauliza walisema wanapewa na waganga wa kienyeji ili wasikamatwe au waionekane wanapoiba.”

“Sasa nataka niwaulize swali la mwisho nyote wawili.  Je  mtakapowaona tena wale watu mnaweza kuwatambua?”

“Wakiwa na mavazi yale yale tunaweza kuwatambua. Yule mmoja anajitambulisha kutoka


na na shingo yake.” Polisi mmoja  akajibu.

“Wasipokuwa na yale mavazi hamtaweza kuwatambua?”

“Itakuwa vigumu kwa sababu hatukuwaona kwa karibu.”

“Kwa hiyo tutakapokamata majambazi tunaowashuku tusiwaite kuja kuwatambua?”

“Mnaweza kutuita.  Tunaweza kuwatambua. Tusipowatambua tutasema.”

“Sawa. Sasa nataka msome haya maelezo  yenu kisha  mniwekee sahihi  zenu nyote wawili.”

Amour alimpa polisi mmojawapo ile karatasi aliyokuwa anaandika.

Waliisoma kwa  pamoja kisha wote wawili wakaweka sahihi zao.

“Sasa mnaweza kwenda. Siku yoyote tutakapowahitaji tutawaita.”

Baada ya siku hiyo juhudi za kuwatafuta wauaji  hao zikaanza upya. Watu kadhaa walikamatwa katika maeneo  mbalimbali ya jiji hilo lakini baada ya uchunguzi ilibainika kuwa watu hao sio waliokuwa wanatakiwa. Wakaachiwa.

Ikapita miezi mitatu ya amani. Almasi na wanawe wawili waliobaki walikuwa wameshaanza kusahau matukio  ya kuhuzunisha yaliyotokea.

Alex alikuwa tayari ameanza kujihusisha katika ulevi na kupenda kubadili wanawake. Alikuwa mtu wa starehe aliyekuwa akikesha katika  majumba ya starehe usiku kucha akicheza miziki.

Hata hivyo tabia hiyo alikuwa akiifanya kwa siri sana bila wazazi wake  kujua.  Mdogo wake Benjamin aliyekuwa akiishi  naye alikuwa akijua lakini alimfichia siri. Kwa hiyo mbele  ya wazazi wake Alex alionekana kama malaika lakini huko pembeni alionekana kama shetani.

Kwa lugha  nyingine Alex alikuwa  na sura mbili. Sura ya wema na sura ya ubaya.

Kulikuwa na siku Alex alimpigia simu mpenzi wake Anjela na kumwambia atampitia usiku waende kwenye onesho la muimbaji mmoja  maarufu liliokuwa likifanyika katika klabu moja ya usiku.

Saa tatu usiku Alex akampitia Anjela na gari nyumbani kwao. Anjela alitoka  akajipakia kwenye gari wakaondoka.

“Hivi Alex utajitokeza lini kwetu au tunakula starehe tu halafu tunakuja kuachana?” Anjela akamuuliza Alex.

“Una haraka ya nini  Anjela. Nimeshakwambia nitakuja  kukuoa. Kwanini hunielewi?”

“Ninajua utanioa, kwanini hutaki kujitokeza kwetu  wakakujua?”

“Kila kitu kina wakati wake. Wakati huo wa kujitokeza ukifika  nitajitokeza tu. Usiwe na wasiwasi.”

“Unajua wazazi wangu hawakuaimini. Wameniambia mtakuja kuchokana kabla hata ya uchumba.”

“Wazazi wanapojiingiza ndio  wataharibu kila kitu. Nikuchoke wewe kwa sababu gani?”

“Sasa kwanini hutaki kujitokeza kwa wazazi wangu wakakujua. Yaani siku zote ni kama  unaniiba tu.”

“Sikuibi. Nimekwambia ninajiandaa. Nataka kwanza niongee na wazazi wangu kuwajulisha.”

“Ina maana hadi leo wazazi wako hawajui kama  uko na  mimi?”

“Wanajua lakini sijawambia.”

“Sasa wanajuaje kama hujawambia? Na ni kwanini hujawambia? Una  nia gani na mimi Alex?’

“Nina nia njema  tu, sema sijapata nafasi ya kuzungumza nao lakini nadhani kesho nitawaeleza.”

“Alex sitakuamiini  tena. Nakumbuka kuna siku uliniambia kuwa wazazi wako wana taarifa.”

“Labda nilisahau lakini kesho nitawaambia.”

“Mimi naona kama unanidanganya Alex. Alex nikipata mimba si utaniacha utafute wasichana wengine?”

“Sikuachi. Mimi nakupenda wewe. Sihitaji msichana mwingine.”

“Alex utanipa shida. Nimeshakuona si mkweli.”

“Mpenzi wangu acha kunituhumu. Unajua  kuwa nakupenda sana.”

Anjela akanyamaza kimya. Alex akamuuliza.

“Au wewe hunipendi?’

“Nakupenda.”

“Sasa  nataka uniamini kila  ninachokwambia.”

Walipofika katika  klabu waliyokuwa wanakwenda, Alex aliliegesha gari katika eneo la kuegesha wakashuka na kuingia katika ukumbi wa klabu hiyo.

Kwa karibu saa kadhaa walikunywa, waliserebuka mpaka wakachoka.

Waliondoka katika ukumbi huo saa tisa usiku. Wakati wanajipakia kwenye gari Anjela alimwambia Alex alikuwa amebanwa na haja ndogo hivyo alihitaji kwenda kujisaidia.

Wakati Anjela anakwenda kujisaidia, Alex alibaki kwenye  gari kumsubiri.

Mara tu Anjela alipoondoka Alex aliyekuwa ameuacha wazi mlango wa gari wa siti ya  dereva, aliona watu watatu wakimfuata.

Wawili walikuwa wamevaa mavazi meupe. Mmoja  aliyekuwa katikati yao alivaa mavazi meusi na mkononi alikuwa ameshika upanga.

Hakuweza kuona wala kujua kwamba  watu hao walitokea upande gani. Alishitukia tu akiwaona watu hao wakiwa karibu na gari lake.

Wakati anawaona, Alex alijiambia, watu hao hawakufanana kabisa na watu waliokuwa katika eneo hilo.

Yule aliyekuwa katikati si tu alimshitua Alex kutokana na kushika upanga bali pia kichwa chake kilikuwa kinaning’inia. Alex aligundua shingo yake ilikuwa na athari ya kuchinjwa.

Kumbukumbu ikamjia Alex kwa haraka. Alikumbuka kwamba watu waliowaua kaka zake walikuwa ni kama hao.

Alivyoona wanamfuata kwenye mlango wa gari alitaka kutoka mbio lakini angekimbilia wapi wakati watu hao walikuwa mbele yake. Akasita na kuwatazama. “Wewe ni mtoto wa Almasi?” Mtu alliyekuwa ameshika upanga  akamuuliza Alex kwa sauti kali.

“Ndiyo,  mimi ni mtoto wa  Almasi.” Alex alijibu akiwa amegwaya.

“Baba yako alikuweka dhamana lakini wewe  umeshindwa kutimiza masharti ya dhamna!”

“Aliniweka dhamana wapi?”

“Umechelewa kuuliza swali hilo kwa  sababu muda wako wa kuishi umekwisha!”

Upanga ukalekea kwenye shingo ya  Alex. Alex alitaka  kukurupuka na kurusha ngumi. Wale watu wengine wawili walimuwahi, kila  mmoja  akamshika mkono.

Anjela alikuwa anatoka kujisaidia akawaona watu wamemshika  mpenzi wake. Alimuona  aliyekuwa ameshika upanga akimchinja Alex.

Anjela akapiga ukulele.

“Jamani watu wanamchinja  mume wangu!”

Alirudia kusema hivyo mara tatu akiwa amesimama hatua kadhaa kutoka lilipokuwa gari la Alex.

Wale watu watatu aliowaona waliondoka taratibu  na hakuweza kujua walielekea wapi.