Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Dili iliyokufa -16

Muktasari:

  • SHARIFA alisita kuzungumza akawa amemtumbulia macho Majaliwa. Hapo hapo Majaliwa alianza kusinzia.

ILIPOISHIA

Majaliwa alipoambiwa hivyo akanyamaza kimya.

“Sasa nakwambia kama umeshaanza kuharibika kiasi hicho, ujue nyumba hii itakushinda.”

“Sasa iko wapi hiyo kete yangu?”

“Unaona jinsi ambavyo umerukwa na akili! Unauliza kete yako, unataka kuendelea kuvuta? Wewe mtoto unaelekea pabaya sasa...”

SASA ENDELEA...


SHARIFA alisita kuzungumza akawa amemtumbulia macho Majaliwa. Hapo hapo Majaliwa alianza kusinzia.

Sharifa akatikisa kichwa kusikitika.

“Nakusikitikia mwanangu umshaharibika, sijui nitakupeleka hospitali gani…!”

Majaliwa akagutuka na kufumbua macho.

“Unasemaje mama, bado upo tu”

“Hivi mnapata raha gani mnapokuwa hivyo jamani. Mimi naona mnateseka tu!”

Majaliwa alikuwa akisinzia tena.

“Mama bwana…!” akasema huku amefumba macho.

“Umeshakula huko unakotoka?”

“Sijakula bado”

“Unakula unga na njaa…si utapata kichaa!”

“Nitala tu”

“Hebu toka twende ukale chakula na kesho namwambia baba yako”

Sharifa alimshika mkono Majaliwa akatoka naye chumbani. Alikwenda naye kwenye meza ya chakula akamuandalia chakula na kumuwekea.

“Kula wende ukalale, mimi narudi chumbani” Sharifa alimwambia na kuingia chumbani.

Alimkuta Wakwetu akiwa bado amelala. Lakini kwa upande wa Sharifa akili haikumtuma kulala. Alikuwa hamuamini tena Majaliwa. Alikaa kwenye kitanda huku akiwaza.

Kubadilika kwa tabia ya mwananwe kulikuwa kumemtia wasiwasi mkubwa. Mwanawe alikuwa ni yeye peke yake. Alijiambia kama mwana mwenyewe ameshaanza kuwa teja ategemee nini tena?

Atakuja kufanya mambo makubwa na ya ajabu hapa nyumbani, nitaiweka wapi roho yangu jamani! Sharifa aliwaza kwa uchungu.

Baada ya kupita nusu saa alitoka tena. Alimkuta Majaliwa amelala kwenye kiti. Chakula alikula kidogo tu.

“We Majaliwa…osha mkono uende ukalale chumbani. Baba yako asije akaamka na kukukuta hapa”

Sharifa alimuamsha mwanawe, akaosha mikono na kuingia chumbani.

Aliporudi tena chumbani mwake, Sharifa alikuta Wakwetu ameamka.

“Ni saa ngapi sasa” Wakwetu akamuuliza.

“Ni saa nane” Sharifa alimjibu kwa wasiwasi.

“Unatoka wapi?”

“Natoka jikoni. Nilisahau kuweka mboga kwenye friza” Sharifa akasema uongo.

“Nilisikia kama ulikuwa unazungumza na mtu.”

Sharifa akashituka.

“Hapana, labda ulikuwa unaota”

“Nilikusikia wakati nimeshaamka”

“Ni mawazo yako tu, sikuwa nikizungumza na mtu yeyote”

“Majaliwa ameshakuja?”

“Mbona alikuja mapema sana”

“Wakati tunalala alikuwa hajarudi”

“Baadaye kidogo aligonga geti, nikaenda kumfungulia”

“Siku hizi ana tabia ya kurudi usiku mwingi”

“Lakini hakuchelewa sana”

Wakwetu hakusema kitu tena.

Asubuhi kulipokucha baada ya Wakwetu kwenda kazini kwake Sharifa alimuweka kikao mwanawe, akamsema sana kuhusiana na kubadilika kwa tabia yake.

Alimuonya juu ya matumizi ya kula unga na kuvuta bangi na kumueleza kuwa vitu hivyo vitamuharibia maisha yake.

“Kama baba yako atajua kuwa unakula unga na kuvuta bangi anaweza kukufukuza hapa nyumbani na maisha yako huko utakakokwenda yataharibika zaidi” akamwambia.

“Bado. Tulikuwa tuna malengo kwamba wewe uje umrithi huyu mzee mali zake kwa sababu hana mtoto mwingine zaidi yako lakini kwa mwendo unaokwenda malengo yetu hayatatimia” Sharifa aliendelea kumueleza mwanawe.

Baada ya kusemwa sana na mama yake, Majaliwa alikiri makosa yake na kuahidi kuwa hataendelea tena kutumia madawa ya kulevya na kuvuta bangi.

“Sasa hayo makundi ya marafiki zako uyaepuke. Hao ndio waliokuharibu wewe” Sharifa alimwambia.

“Ni kweli lakini nitajitahidi kuwa mbali na marafiki wabaya”

Kutoka siku ile Majaliwa alijifanya kama amebadilika lakini alikuwa akiendelea kutumia mihadharati kisirisiri.

Ikapita kama wiki moja hivi. Ilikuwa saa nne usiku wakati Wakwetu akijiandaa kulala, simu yake ilipoita. Alipoitazama sikrini ya simu aliona namba ya Majaliwa, akaipokea.

“Baba nilichukua gari mara moja bila kukuambia lakini kwa bahati mbaya nimegonga mtu hapa kwenye barabara ya Mkwakwani. Hivyo nimeliacha gari na kukimbia kwani wananchi walitaka kunipiga…”

Taarifa ile ilimshitua Wakwetu, akamuuliza Majaliwa.

“Unasema nini?”

Hapo hapo Majaliwa akakata simu.

Wakwetu akampigia na kukuta simu ya Majaliwa imeshazimwa.

Akatoka kwenda kuliangalia gari lake, akakuta gari halipo!

“Huyu mtoto alilitoa muda gani hili gari?” akajiulia bila kupata jibu.

Alirudi ndani. Sharifa alikuwa anaoga akamsubiri, alipotoka alimuuliza.

“Majaliwa alichukua gari?”

“Sijui” Sharifa akamjibu na kuuliza.

“Kwani gari halipo?”

“Halipo na amenipigia simu sasa hivi. Ananiambia kuwa alichukua gari na amegonga mtu, gari ameliacha na amekimbia…”

“Amegonga mtu wapi?”

“Ameniambia amegonga mtu barabara ya Mkwakwani. Nataka nimuulize vizuri amekata simu”

“Mpigie umuulize ili tujue huyo mtu amemgonga wapi’

“Nimempigia, simu yake haipatikani tena. Ameizima. Huyu mtoto ana akili mbovu sana”

“Sasa itakuwaje?”

“Kwanza funguo za gari langu alizipataje?”

“Labda aliingia huku chumbani na kuzichukua”

Wakwetu alijaribu tena kumpigia, simu ya Majaliwa iilikuwa bado haipatikani. “Upumbavu wake mwingine ni huu wa kuzima simu. Sasa hatujui huyo mtu aliyemgonga yuko katika hali gani, yeye anazima simu”

“Sasa ungekwenda kulitazama hilo gari, yule ni mtoto tu hana akili”

“Angekuwa hana akili asingeiba gari langu. Anataka kuniletea matatizo tu. Mtu mwenyewe hana leseni ya kuendeshea halafu anagonga mtu. Mimi mwenye gari ndiyo nitaonekana mzembe”

“Sasa tukae chini tupange tutafanyaje, kama ni ajali imeshatokea”

“Itabidi nimpigie simu James niende naye. hilo gari hivi sasa litakuwa mikononi mwa polisi”

“Uende na james wa nini?”

“Tufanye kama hilo gari alikuwa akiliendesha yeye. James ana leseni. Majaliwa hana leseni”


“Sawa. Basi fanya hivyo”

Wakwetu akampigia James.

“Chukua teksi uje hapa haraka” Wakwetu akamwambia James kwenye simu.

“Sawa mzee ninakuja”

Baada ya saa moja hivi James akawasili. Wakwetu alilipia ile teksi aliyompeleka James kisha akamueleza James tatizo lililokuwepo.

James akakubali kujifanya ndiye aliyemgonga huyo mtu kwa vile Wakwetu alimhakikisha kuwa atagharamikia matibabu ya huyo mtu aliyegongwa pamoja na kulipa faini itakayotakiwa.

“Makosa ya trafiki ni ya kifungo na faini. Nitakulipia faini na kama kuna mtu ameumizwa nitagharamikia matibabu yake” Wakwetu alimwambia.

Wakwetu na james wakatoka. Walikwenda kukodi teksi iliyowapeleka barabara ya Msimbazi.

Walishindwa kupagundua mahali ilipotokea ajali wakaenda kituo cha polisi kilichokuwa karibu.

Wakwetu alilikuta gari lake likiwa nje ya kituo. Yeye na james waliingia katika kituo hicho na kujitambulisha.

“Wewe ndiye uliyemgonga yule mtu?” Polisi mmoja aliyekuwa kaunta alimuuliza james kwa taharuki.

“Ndiye mimi”

Hapo hapo James akakamatwa.

“Mpaka sasa uko chini ya ulinzi” James aliambiwa.

“Nitamuwekea dhamana” Wakwetu akawambia polisi.

Kosa linalomkabili yeye halina dhamana”

“Kosa lolote la  trafiki lina dhamana”

“Mbali na kosa la kumgonga mtu, huyu anakabiliwa na kosa la mauaji”

Wakwetu na James wakashituka.

“Mauaji ya nani tena?” Wakwetu akauliza.

“Dereva wako amempiga mtu risasi katika gesti moja huko Mabawa na alikuwa anakimbia na gari kabla ya kugonga mtu”

Wakwetu akajiuliza kimoyomoyo “Mwanangu alikwenda Mabawa kumpiga mtu risasi na kumuua?”

Wakwetu hakupata jibu, akamkazia mcho yule polisi.

“Sijakuelewa, unasema dereva wangu amempiga mtu risasi na kumuua?”

“Hizo taarifa tayari zimesambazwa katika vituo vyote vya polisi. Alama yetu ilikuwa ni namba ya usajili ya hilo gari kwani alipofika hapo gesti, watu waliona namba ya gari alilokuwa nalo. Kwa hiyo ilipotokea hii ajali, polisi walipofika wakaona namba ya usajili ya gari hilo ndiyo namba ya gari ya huyo mtu aliyefanya mauaji.”

“Haiwezekani. Dereva wangu si jambazi. Inawezekana mmekosea kusoma namba”

“Kuna kachero aliyekwenda katika hiyo gesti kufanya uchunguzi na kupata ukweli. Kwa hiyo hadi kesho asubuhi ukweli utakuwa umefahamika”