Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Waziri Mkuu, Diamond, Zuchu wachangia matibabu ya Mkubwa Fella

MATIBABU Pict

Muktasari:

  • Mwigulu amechangia Sh10 milioni kwa ajili ya matibabu ya Fella, huku Diamond akitoa Sh50 milioni. Diamond hakuhudhuria hafla hiyo, lakini alimtuma Zuchu kumwakilisha na kuwasilisha mchango wake. Zuchu naye amechangia Sh10 milioni.

WAZIRI Mkuu wa Tanzania, Dk Mwigulu Nchemba, mwanamuziki Diamond Platnumz na Zuchu, ni miongoni mwa watu mashuhuri waliojitokeza kuchangia gharama za matibabu ya meneja mkongwe wa muziki wa Bongo Fleva, Said Fella maarufu kama Mkubwa Fella, katika hafla maalumu iliyopewa jina la Heshima kwa Mkubwa iliyofanyika leo, Novemba 29, 2026, Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam.


Mwigulu amechangia Sh10 milioni kwa ajili ya matibabu ya Fella, huku Diamond akitoa Sh50 milioni. Diamond hakuhudhuria hafla hiyo, lakini alimtuma Zuchu kumwakilisha na kuwasilisha mchango wake. Zuchu naye amechangia Sh10 milioni.


Hata hivyo, zoezi la kuchangisha fedha bado linaendelea huku wasanii, viongozi, watu maarufu na wadau mbalimbali wa muziki na burudani wakiendelea kujitokeza kutoa michango yao kwa ajili ya kumsaidia Fella katika safari yake ya matibabu.


Hafla hiyo imeandaliwa kwa lengo la kumuenzi Fella kutokana na mchango wake mkubwa katika kukuza muziki wa Bongo Fleva na kusimamia vipaji vya wasanii mbalimbali, huku ikitumika pia kama nafasi ya kuhamasisha wadau kumsaidia katika kipindi hiki ambacho afya yake inahitaji uangalizi na matibabu zaidi.



ALIANZA KUUMWA MWISHO WA 2024

Historia ya changamoto za afya ya Mkubwa Fella ilianza kujulikana zaidi kwa umma mwishoni mwa mwaka 2024, ambapo Desemba 31, 2024, Mwanaspoti lilimfuata nyumbani kwake Mbagala Kilungule jijini Dar es Salaam.


Wakati huo, taarifa zilizokuwa zikienea zilieleza kuwa, Fella alipooza miguu na alikuwa akizungumza kwa shida. Baadhi ya ndugu zake walithibitisha alikuwa anaumwa na alihitaji kupumzika.


Februari 3, 2025, Fella alipoulizwa na Mwanaspoti kuhusu hali yake, alikiri kuumwa huku akisema ameanza kupata nafuu kidogo tofauti na alivyokuwa nayo awali.


Machi 4, 2025, Mwanaspoti liliripoti kwa kina kuhusu hali yake baada ya kuzungumza na ndugu yake, Said, aliyefafanua kuwa Fella alikuwa akisumbuliwa na presha iliyosababisha kupooza upande mmoja wa mwili.


Kwa mujibu wa ndugu huyo, katika hatua za awali za matibabu, Fella alipelekwa Hospitali ya Mloganzila, baadaye akahamishiwa Hospitali ya Taifa Muhimbili, kisha Hospitali ya TMJ, ambako alianza kupata nafuu.


Baadaye alisafirishwa kwenda India kwa ajili ya matibabu ya mwezi mmoja, huku gharama za matibabu na safari hiyo zikigharamiwa na Diamond Platnumz.



ALIKATA TAMAA YA KUPONA

Mei 8, 2025, Fella alizungumza tena na Mwanaspoti na kueleza jinsi ugonjwa ulivyokuwa umemtesa kiasi cha kufikia hatua ya kukata tamaa ya kupona.


Hata hivyo, alisema wakati huo alikuwa ameanza kuona mabadiliko ya afya yake, akiweza kuzungumza vizuri na kufanya mazoezi ya kutembea kila jioni.


Alisema alikuwa na furaha kwa sababu hali yake ilikuwa ikiimarika kila siku, huku akimshukuru Mungu kwa hatua aliyokuwa amefikia baada ya kipindi kigumu cha kuumwa.


FAMILIA YAOMBA MSAADA

Januari 6, 2026, mke wake, Sweet Fella, aliandika ujumbe kwenye akaunti yake ya Instagram akieleza changamoto alizokuwa akipitia katika kumuuguza mumewe na kukosekana kwa baadhi ya watu wa karibu waliokuwa wakimtembelea na kumjulia hali.


Januari 7, 2026, Sweet alipozungumza na Mwanaspoti, alifafanua kuwa baadhi ya watu walidhani Diamond alikuwa akigharamia kila kitu, hivyo wengine walishindwa kujitokeza kumsaidia Fella.


Januari 8, 2026, Sweet aliiambia Mwanaspoti kuwa mumewe alikuwa bado anaendelea na matibabu, kliniki mara mbili kwa wiki na mazoezi ya kila siku asubuhi. Alieleza kuwa gharama za mazoezi zilikuwa zikifikia Sh1.2 milioni kwa mwezi, mbali na dawa alizokuwa akitumia.


Sweet alisema pia Fella alihitaji kurejea India kwa mara ya pili kwa ajili ya matibabu zaidi, hivyo familia ilikuwa tayari kupokea msaada kutoka kwa yeyote aliyeguswa na hali yake.


Ikumbukwe kuwa, wakati taarifa za ugonjwa wa Fella zikisambaa mwanzoni mwa mwaka 2025, Diamond alitajwa na baadhi ya watu mitandaoni kuwa amemtelekeza meneja huyo aliyekuwa na mchango mkubwa katika safari yake ya muziki.


Hata hivyo, taarifa zilizotolewa na ndugu wa Fella na Babu Tale zilieleza Diamond alikuwa ameshiriki kumsaidia tangu hatua za mwanzo za matibabu yake.


Aprili 5, 2026, Diamond alizungumzia kuhusu tuhuma hizo katika mahojiano na Lil Ommy, akieleza alihusika kumtafutia Fella matibabu na kugharamia safari yake ya kwenda India.


Alisema aliamua kujiondoa kwenye usimamizi wa moja kwa moja wa baadhi ya mahitaji ya matibabu baada ya kuelewa kuwa uwepo wake uliwafanya baadhi ya watu washindwe kujitokeza kutoa msaada, kwa kudhani yeye alikuwa akigharamia kila kitu.


Alieleza kuwa, aliweka watu wake wa karibu kusimamia mahitaji ya matibabu na malipo yaliyohitajika.


Sasa, kupitia hafla ya Heshima kwa Mkubwa, wadau mbalimbali wameendelea kuungana kumsaidia Fella, huku michango ikiendelea kupokelewa kwa ajili ya safari yake ya matibabu na mahitaji mengine yanayohusiana na afya yake.