TRA yamrejeshea Ommy Dimpoz gari lake
Muktasari:
- Septemba 26, 2026, gari aina ya Mercedes-Benz G-Wagon inayomilikiwa na Ommy Dimpoz ilikamatwa na TRA kutokana na dosari hizo.
MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imemrejeshea msanii wa muziki wa Bongo Fleva, Omary Nyembo maarufu kama Ommy Dimpoz, gari lake lililokuwa limekamatwa kutokana na ukiukwaji wa taratibu za forodha, baada ya kukamilisha malipo ya kodi ya ziada iliyobainika.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam wakati wa makabidhiano ya gari hilo, Kaimu Mkurugenzi wa Elimu kwa Mlipakodi na Mawasiliano wa TRA, Paul John Walalaze, amesema gari hilo lilikamatwa baada ya kubainika kuwepo kwa taarifa zisizo sahihi katika nyaraka za uingizaji wake nchini.
Walalaze amesema TRA imetoa msamaha wa riba na adhabu kwa wamiliki wa magari yaliyoingizwa nchini kwa kukiuka taratibu za forodha, ikiwemo kutumia njia za transit, vibali vya muda au kuwasilisha taarifa zisizo sahihi kuhusu chassis, modeli na mwaka wa kutengenezwa kwa magari hayo.
Amesema wamiliki wa magari hayo wanapaswa kujitokeza katika ofisi za TRA na kutumia fursa hiyo kulipa kodi inayostahili bila riba na adhabu kabla ya Desemba 31, 2026, akibainisha kuwa magari 168 yalikuwa yamejitokeza katika mwezi Oktoba pekee.
Kwa upande wake, Ommy Dimpoz amesema awali aliamini gari lake lilikuwa limeingizwa nchini kwa kufuata taratibu, lakini baada ya TRA kumweleza dosari zilizokuwepo katika taarifa za gari hilo, alikubali kufuata utaratibu na kulipa kodi iliyobainika kuwa haijalipwa.
Msanii huyo amesema ameamua kuweka wazi changamoto hiyo ili kutoa elimu kwa Watanzania kuhusu umuhimu wa kufuatilia taarifa na taratibu za forodha wanaponunua magari kutoka nje ya nchi, akisisitiza kuwa kushirikiana na TRA ni muhimu katika kuhakikisha ulipaji kodi unazingatiwa.
Ametoa wito kwa wamiliki wengine wa magari yenye dosari za kiforodha kutumia fursa hiyo kabla ya muda wa msamaha kumalizika, huku akiahidi kuendelea kuwa balozi wa ulipaji kodi nchini.
Septemba 26, 2026, gari aina ya Mercedes-Benz G-Wagon inayomilikiwa na Ommy Dimpoz ilikamatwa na TRA kutokana na dosari hizo.