Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Maswali 'tata' ujio wa Davido Bongo

Muktasari:

  • Zaidi ya hilo, mashabiki bado hawajajua hasa ujio wa Davido nchini, maswali ni mengi, lakini makubwa ambayo hata Mwanaspoti linajiuliza ni huenda amekuja kwa ajili ya kazi za kimuziki, utalii, kukutanisha familia zao au shughuli binafsi.

UJIO wa nyota wa muziki wa Afrobeat kutoka Nigeria, Davido umeendelea kutikisa kuanzia mapokezi yake aliyofanyiwa na Diamond Platnumz na sasa gumzo kubwa ni bata wanalokula wasanii hao ambao walikutana mara ya kwanza miaka 13 iliyopita.

Zaidi ya hilo, mashabiki bado hawajajua hasa ujio wa Davido nchini, maswali ni mengi, lakini makubwa ambayo hata Mwanaspoti linajiuliza ni huenda amekuja kwa ajili ya kazi za kimuziki, utalii, kukutanisha familia zao au shughuli binafsi.

Wakati tukisubiri kujua kilichomleta Davido nchini, hebu tuangalie ni lipi kati ya haya yana uwezekano wa kutokea baada ya ujio wake.

KUNA SHOO INAANDALIWA?

Ni wazi kila msanii anayekuja nchini imekuwa ikitangazwa mapema ujio wake kwenye vyombo vya habari ili mashabiki wajiandae kwa tiketi na mtoko wa siku hiyo.

Hata hivyo, ujio wa Davido umekuwa wa ghafla sana na mapokezi yake yameishia kwa Diamond tu na hivyo kuwaacha mashabiki wasielewe kuna shoo imeandaliwa ya pamoja au ya kwake binafsi na kama ni hivyo, mbona haijasikika kokote?

Davido alishawahi kuja nchini na kufanya shoo na ilitangazwa mapema na mashabiki kufika kwa wingi, zikiwamo za Serengeti Fiesta (2013), 30 Billion World Tour (2018) na ile ya Februari 7, 2026 kwenye Uwanja wa Lugalo Golf Club huko Kawe, Dar es Salaam.


KUKUTANISHA FAMILIA?

Tangu wasanii hao walipokutana miaka 13 iliyopita na kutoa ngoma mapoja ya 'Number One Remix', mawasiliano yamekuwapo licha ya tetesi za mika ya nyuma waliwahi kutofautiana.

Kila mmoja amekuwa akifanya kazi zake na kupata mafanikio na ujio wa Davido nchini unatafsiriwa pia amekuja kukutana na familia ya Diamond ili kuzidi kuwa karibu kwani ameambatana na mkewe, Chioma Adeleke, Davido na Chioma wameonekana wakifurahia mandhari ya bahari, vyakula na maisha ya utulivu jijini Dar es Salaam wakiwa na wenyeji wao Diamond Platnumz na Zuchu.

KUNA KAZI YA PAMOJA?

Hadi sasa, Diamond na Davido wana collabo moja tu rasmi iliyowahi kutoka hadharani, ambayo ni Number One (Remix) ya mwaka 2014.

Wimbo huu unatajwa ndiyo wimbo uliovunja mipaka ya muziki wa Bongo Flava na kumtambulisha Diamond kwa kishindo Afrika Magharibi na kimataifa.

Licha ya mazingira ya mapumziko, wawili hao wameonekana wakirekodi muziki na kufanya mazungumzo ya kikazi. Watu wa karibu na Diamond Platnumz wamedokeza kuhusu uwepo wa mradi mkubwa wa pamoja wa kimuziki na uwezekano wa kurekodi video ya wimbo mpya.

Hivyo, ujiwa wake unaacha maswali ikiwamo kama wataachia wimbo mpya au hata albamu ya pamoja? Tusubiri tuone.


KULA BATA?

Wawili hao wameonekana wakiwa kwenye boti ya kifahari 'yacht' wakifurahia burudani pamoja na familia na watu wao wa karibu. Ni jambo linaloacha maswali, je ujio wake ni kwa ajili ya bata ambalo tayari ameanza kulila na mwenyeji wake au kuna mengine.

Katika tukio hilo lililofanyika usiku wa kuamkia Alhamisi, Novemba 12, 2026, Diamond na mkewe Zuchu walikuwa pamoja na Davido aliyeambatana na mkewe Chioma, huku familia ya Diamond pamoja na baadhi ya marafiki na watu wa karibu wa wasanii hao wakishiriki burudani hiyo.

Kilichovutia zaidi katika burudani hiyo ni namna nyimbo za wasanii hao pamoja na Zuchu zilivyotawala.

Pia Davido alionekana akimwimbia mkewe wimbo wake Already Falling huku watu waliokuwa nao wakifurahia tukio hilo.


AMEKUJA KUTALII?

Baadhi ya mastaa wakubwa duniani ikiwamo wa muziki na michezo wamekuwa wakija Tanzania kimya kimya kwa ajili ya kufanya utalii kwenye vivutio mbalimbali vya hifadhi za Taifa na Mlima Kilimanjaro.

Kutokana na kutokuwekwa wazi wa ujio wake kama ni kufanya shoo au muziki, wengine wanarejelea ujio wa watu maarufu waliofika nchini kufanya utalii na ujio wa Davido huenda ameamua kuitembelea Tanzania kujionea vivutio hivyo.

Ndiyo, ujio wa Davido bado haujaeleweka na hadi sasa hakuna tangazo rasmi kutoka kwa Diamond au yeye mwenyewe kuhusu kazi zao au tamasha kama vitafanyika.

Hata hivyo, ukaribu wao umeongeza matarajio ya mashabiki wanaotamani kuona wakizidi kushirikiana kwa kutoa kazi ya pamoja.