Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

TASUBA yafunga Tamasha kwa kishindo!

TASUBA Pict

Muktasari:

  • Tamasha hilo lililoanza Oktoba 28, mwaka huu, katika viwanja vya Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa), limekuwa jukwaa la kuonesha vipaji, kubadilishana uzoefu na kutangaza utajiri wa sanaa na utamaduni wa Tanzania.

BAADA ya siku nne za shamrashamra za sanaa, utamaduni na burudani zilizowakutanisha washiriki kutoka ndani na nje ya nchi, Tamasha la 44 la Kimataifa la Sanaa na Utamaduni Bagamoyo limefunga pazia lake Jumamosi, Oktoba 31, 2026, huku likiacha gumzo na matarajio makubwa kwa wadau wa sanaa.

Tamasha hilo lililoanza Oktoba 28, mwaka huu, katika viwanja vya Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa), limekuwa jukwaa la kuonesha vipaji, kubadilishana uzoefu na kutangaza utajiri wa sanaa na utamaduni wa Tanzania.

Katika siku hizo nne, Bagamoyo imekuwa sehemu ya kukutana kwa tamaduni tofauti, huku vikundi na wasanii kutoka mataifa mbalimbali wakipata nafasi ya kuonyesha kazi zao na kujifunza kutoka kwa wenzao.


TASU 02

UMATI WAONGEZEKA SIKU ZA MWISHO

Idadi ya watu waliojitokeza kushuhudia burudani ilionekana kuongezeka zaidi siku za mwisho za tamasha hilo, ikilinganishwa na ya ufunguzi na zile za katikati ya tamasha.

Mbali na wananchi, wasanii mbalimbali ambao hawakuwa wamealikwa kutumbuiza nao walifika kwa wingi kushuhudia maonyesho hayo, jambo lililoonyesha namna tamasha hilo lilivyovutia wadau wa sanaa na burudani.


TASU 04

WASANII WAFUNGA PAZIA KWA BURUDANI

Siku ya mwisho ya tamasha hilo, burudani ziliendelea kwa maonyesho ya ngoma za asili, maigizo, sarakasi na muziki katika majukwaa mbalimbali. Miongoni mwa waliotumbuiza ni Landaa Cultural Group, Kikundi cha Utamaduni cha Kusini, Sauti ya Umoja, Kandiri Art Group, Bagamoyo Acrobatic Club na Magomamoto Theatre Group.

Burudani iliendelea kwa maonyesho ya Gifted Muneka kutoka Zambia pamoja na Mose Iyobo na Iyobo's Family waliowasilisha dansi za kisasa.

Usiku uliendelea kuwa na burudani za muziki hadi alfajiri, huku Sauti Marley & The Band, Baob Cypher, Siza Segere Stars na Vitali Maembe & Watupamawe wakipanda jukwaani, kabla ya Ziro MC 77 kuhitimisha ratiba kwa muziki wa Singeli.

Mchanganyiko wa burudani hizo, ongezeko la watu waliojitokeza na ushiriki wa wasanii mbalimbali waliokuja kushuhudia uliifanya siku ya mwisho kuwa kilele cha shamrashamra za tamasha hilo, lililofunga pazia kwa kishindo.

TASU 05

Akizungumza wakati wa kufunga tamasha hilo, Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Shaibu Ndemanga amesema mwaka huu wamepokea washiriki kutoka zaidi ya nchi tisa, akitaja Italia, Uingereza, Ghana, Kenya, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Uganda miongoni mwa mataifa yaliyowakilishwa.

Amesema ushiriki huo unalifanya tamasha kuwa la kimataifa kwa sababu si jukwaa la kuonyesha sanaa ya Tanzania pekee, bali pia linatoa nafasi kwa wageni kujifunza na kufurahia utamaduni wa mataifa mengine.

TASU 01

“Tunaposema ni tamasha la kimataifa tunamaanisha ni mahali na watu wanakusanyika kuonyesha utamaduni wa maeneo mbalimbali duniani. Lakini si tu kuonyesha, tunapata fursa pia ya sisi kuonyesha dunia tuna nini katika Tanzania ambacho wao wanaweza kuja kujifunza kwetu au kuja kufurahi wakifika kwetu,” amesema Ndemanga.

Anaeleza tamasha hilo halihusishi sanaa na utamaduni pekee, bali pia limegusa maeneo ya michezo, utalii na maendeleo ya vijana na kundi kubwa la washiriki waliokuwepo ni vijana.

Kwa mujibu wa Ndemanga, uwepo wa wadau na viongozi kutoka Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo pamoja na Wizara ya Maendeleo ya Vijana ni fursa ya kutambua shughuli zinazofanywa na vijana na namna sanaa inavyoweza kuwa sehemu ya maendeleo yao.


TASU 03

MATARAJIO MAPYA 2027

Hata hivyo, kufungwa kwa tamasha hilo kumeacha matarajio ya toleo lijalo, huku Mkuu huyo wa Wilaya akitoa kauli inayowapa matumaini wapenzi wa sanaa na utamaduni.

Ndemanga amesema tayari amezungumza na viongozi wa wizara zinazohusika, ambao wameonyesha utayari wa kushiriki katika maandalizi ya tamasha lijalo ili liwe kubwa zaidi ya mwaka huu.

“Tamasha lijalo ambalo litakuwa Oktoba 27 hadi 30, ninaamini litakuwa kubwa mara mbili au tatu ya hili la mwaka huu. La mwakani tunataka tulianze kwa nguvu ya aina yake,” amesema.

Kauli hiyo inaweka matarajio mapya kwa wadau wa sanaa, hasa ikizingatiwa tamasha hilo limeendelea kuwa moja ya majukwaa muhimu ya kukuza vipaji na kutangaza utamaduni wa Tanzania kwa wageni kutoka mataifa mbalimbali.

Kwa upande mwingine, historia ya tamasha hilo inaonyesha limekuwa na nafasi muhimu katika kuendeleza sanaa na utamaduni nchini, huku TaSUBa ikiendelea kuwa sehemu ya kukuza wasanii na kutoa elimu katika fani mbalimbali za sanaa.

Hivyo, pazia la toleo la 44 limefungwa, lakini safari ya kuendeleza sanaa na utamaduni kupitia jukwaa hilo inaendelea, huku macho ya wadau yakielekezwa kwenye toleo lijalo litakalofanyika Oktoba 27 hadi 30, 2027.