Sababu ukimya wa Harmonize hii hapa
Muktasari:
- Kumekuwapo na maswali mengi juu ya ukimya wa msanii huyo ambaye kila kukicha alikuwa hakauki mitandaoni kuanzia kutangaza kazi zake na mambo ya mahusiano na hivyo mashabiki kuhoji nini kimemkuta.
MSANII wa Bongo Fleva, Harmonize amesema ameamua kuwa kimya na kutojihusisha na mitandao ya kijamii kwani ameona inampotezea muda.
Kumekuwapo na maswali mengi juu ya ukimya wa msanii huyo ambaye kila kukicha alikuwa hakauki mitandaoni kuanzia kutangaza kazi zake na mambo ya mahusiano na hivyo mashabiki kuhoji nini kimemkuta.
Wapo wanaodai ni mawazo ya mahusiano na wengine wakisema ameamua kubadilika na kuangalia zaidi kazi yake, hata hivyo, Mwanaspoti lilimtafuta na kuzungumza naye na alifunguka ukimya wake ni kuipisha mitandao ya kijamii na yeye aendelee na kazi zake.
Pia alisema kuna wakati mtu anakubali tu kuandamwa na mitandao ya kijamii, akiamini kuna muda watanyamaza na mtu utaendelea na mambo yako vizuri kama ilivyokuwa kwake hasa akiwa kwenye mahusiano.
“Kwa sasa nimeipisha mitandao kwanza, maana kila kukicha ilikuwa ni mimi, lakini mwishowe nilikubali tu kila kitu nikaa kimya na walisema na wakamaliza yote, sasa wametulia,” alisema Harmonize.
Harmonize ambaye anamiliki lebo ya muziki ya Konde Music, sasa hivi kwenye akaunti yake Instagram, amekuwa akiposti kazi zake tu tofauti na ilivyozoeleka kuchanganya posti za mahusiano au ujumbe wa mafumbo.
Kwa sasa Harmonize ameuachia wimbo unaoitwa 'Lala' aliomshirikisha msanii Abigail Chams unaoendelea kufanya vizuri kwenye Vituo mbalimbali vya redio.
Kabla ya wimbo wa Lala, Harmonize ametamba na nyimbo kama Aiyola, ujana, Single again, Kwangwaru, Niambie na nyingine nyingi.
Khadija Yusuf ataja siri ya urembo, kutozeeka
RHOBI CHACHA
MSANII wa Muziki wa Taarabu, Khadija Yusuf amefunguka siri ya kuendelea kuonekana mrembo licha ya umri mkubwa alionao unaowapa maswali mashabiki zake.
Akizungumza na Mwanaspoti, Khadija ambaye ni mdogo wa Mzee Yusuf na anayekadiriwa kuwa na zaidi ya miaka 40, alisema amekuwa akiulizwa ni nini anatumia kiasi cha kumfanya asizeeke na kufichua ni kutokana na muda mwingi kuwa na hana mawazo ya maisha.
“Kwa kweli sina mawazo na siyo sina matatizo ila niliamua siyo kila jambo baya au linaloniumiza nalibebe, huwa naamua kuyapotezea kwa sababu nikisema nibebe dunia hii kuna mambo mengi, nitazeeka bure,” alisema Khadija.
Alisema mara nyingi amekuwa na mbinu nyingi za kutafuta nini cha kufanya ili kichwa chake kiwaze kazi na siyo kushindwa au kuwaza kitu ambacho kitamfanya akose amani.
Khadija amewahi kupita katika bendi tofauti nchini kama East African Melody, Zanzibar Stars, Jahazi Morden Taarabu, Five Stars na Wakali Wao. Ametamba na nyimbo kama, Sina uzuri wa sofa, Mkodombwe, Nilijua mtasema, Mkuki kwa Nguruwe na nyingine nyingi.