Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Platform: Miezi saba ya ukimya ni darasa tosha

Muktasari:

  • Katika mahojiano na Mwanaspoti, msanii huyo amezungumza kuhusu sababu za ukimya huo, maisha binafsi, historia ya muziki na mipango ya baadaye.

BAADA ya kukaa kimya kwa miezi saba bila kutoa kazi mpya, msanii wa Bongofleva, Platform TZ amerejea kwenye gemu akiwa na mradi wa nyimbo tatu alioupa jina la Hatua Tatu.

Katika mahojiano na Mwanaspoti, msanii huyo amezungumza kuhusu sababu za ukimya huo, maisha binafsi, historia ya muziki na mipango ya baadaye.

Platform, aliyejijengea jina kupitia nyimbo zikiwemo ‘Chuki’, ‘Fall’ aliyomshirikisha Marioo na ‘Kuachana Sh’ngapi’ aliyoshirikishwa na D Voice, sasa amerejea na nyimbo kama ‘Siwezi’, ‘Tilalila’ aliyowashirikisha Dogo Pateni na Malume pamoja na ‘Nampenda’.

Msanii huyo anasema miezi saba aliyokaa nje ya soko la muziki haikuwa kipindi cha kupumzika, bali alikuwa akijipanga upya kufuatia mabadiliko ya uongozi na timu iliyokuwa ikimsimamia.


MABADILIKO YA TIMU

Suleyman Salim, maarufu kama Platform, anasema baada ya kumaliza mkataba na uongozi wake wa awali uliokuwa chini ya Abbah Classic, baadhi ya watu aliokuwa akifanya nao kazi hawakuweza kuendelea naye kwa sababu walikuwa bado ndani ya mikataba na lebo nyingine. Hali hiyo ilimlazimu kusubiri hadi taratibu hizo zikamilike.

Anasema aliamua kutumia kipindi hicho kutafuta timu mpya yenye nidhamu ya muda, uelewano na uwezo wa kushirikiana naye katika nyakati nzuri na ngumu za kazi.

“Nilihitaji kupata watu ambao tutaendana nao, wenye kemia nzuri ya kazi, sikutaka kukurupuka,” anasema Platform.


HII SIYO EP, NI TRIPLE RELEASE

Baada ya kipindi hicho cha ukimya, Platform amerejea na mradi wa Hatua Tatu wenye nyimbo ‘Siwezi’, ‘Tilalila’ na ‘Nampenda’.

Anasema licha ya baadhi ya mashabiki kuuchukulia kama EP, mradi huo ni Triple Release, alioutengeneza kama kifurushi maalumu cha kuwapa mashabiki wake muziki baada ya kusubiri kwa muda mrefu.

Katika mpango wa awali, anasema alikusudia kutoa nyimbo nne, lakini ilishindikana kutokana na maandalizi ya kazi nyingine aliyoshirikiana na Vanillah, inayotarajiwa kutoka mwishoni mwa Novemba.

“’Hatua Tatu’ ni package kwa mashabiki wangu ambao wamekaa muda mrefu wakisubiri muziki wangu,” anasema.

Kuhusu utayarishaji, anasema Laizer amehusika katika nyimbo mbili, ‘Siwezi’ na ‘Nampenda’, huku Good Master akisimamia ‘Tilalila’ aliyowashirikisha Dogo Pateni na Malume. Anasema ilikuwa mara yake ya kwanza kufanya kazi na Laizer, lakini walielewana na kupata matokeo mazuri.


DOGO PATENI, MALUME

Uamuzi wa kuwashirikisha Dogo Pateni na Malume kwenye ‘Tilalila’ haukuwa wa bahati mbaya. Platform anasema amekuwa akifuatilia namna vijana hao wanavyoupambania muziki wa Singeli na anathamini mchango wao katika kuuweka muziki huo kwenye ramani.

Anasema Singeli una utambulisho wa Tanzania, unaobeba ladha ya Kiswahili na maisha halisi ya watu wengi, hivyo ni muhimu kuendelea kuupa nafasi katika kazi zake.

SINGELI KUVUKA MIPAKA

Akizungumzia nafasi ya Singeli katika soko la muziki, Platform anaamini kuwa una uwezo mkubwa wa kukua na kufika katika masoko ya kimataifa.

Anasema tayari kuna dalili za muziki huo kuanza kuvuka mipaka kupitia ma-DJ na wasanii wanaopata nafasi za kutumbuiza nje ya nchi. Anamtaja Sholo Mwamba kuwa miongoni mwa wasanii wanaofanya maonesho nje ya Tanzania, akiamini kuwa ni suala la muda tu kabla Singeli haijapata nafasi kubwa zaidi kimataifa.


KILA KITU MWENYEWE

Tofauti na baadhi ya wasanii wenye kampuni au uongozi mkubwa unaosimamia kila hatua ya kazi zao, Platform anasema kwa sasa yeye na timu yake wanasimamia kwa karibu shughuli zote zinazohusu muziki wake.

Anasema anahusika katika maandalizi ya nyimbo, uzalishaji na utengenezaji wa video, huku akifuatilia matumizi ya bajeti ili kuhakikisha kila kitu kinaenda kulingana na mipango yake.

Akitolea mfano video ya ‘Siwezi’, anasema amehusika moja kwa moja katika usimamizi wake badala ya kutegemea mtu mwingine kufanya maamuzi kwa niaba yake.


URAFIKI NA MARIOO

Kuhusu uhusiano wake na uongozi wa awali uliokuwa chini ya prodyuza Abbah pamoja na ukaribu wake na Marioo, Platform anasema hakuna uhasama uliojitokeza baada ya mabadiliko ya usimamizi.

Anasema bado ana mawasiliano mazuri na Abbah, ambaye anamchukulia kama kaka na mtu aliyekuwa sehemu muhimu ya maendeleo yake kimuziki.

Kuhusu Marioo, anasema bado wako vizuri na hakuna tatizo kati yao, huku akidokeza uwezekano wa kufanya kazi pamoja tena.


FUNDI SIMU HADI MSANII

Kabla ya kujulikana katika muziki, Platform alikuwa akifanya shughuli mbalimbali za kujitafutia kipato.

Msanii huyo alizaliwa mkoani Tanga, ambako alipata elimu ya msingi na sekondari kabla ya kuhamia Dar es Salaam kutafuta maisha.

Anasema alipofika jijini alikuwa na ujuzi mdogo wa kutengeneza simu, hivyo alianza kukaa na mafundi ili kujifunza zaidi na baadaye kujishughulisha na kazi hiyo.

Wakati huo kaka yake alikuwa akijishughulisha na muziki. Siku moja alimwomba waende pamoja kwa mkurugenzi wa muziki aliyekuwa Temeke. Walipofika studio, kaka yake alianza kuonesha uwezo wake wa kuimba, kisha Platform naye akajaribu. Baada ya kuwasikiliza, waliambiwa kuwa wote walikuwa na mawazo mazuri ya muziki.

Waliamua kufanya mazoezi kwa takribani mwaka mmoja huku Platform akiendelea na ufundi simu. Baadaye, kupitia rafiki yake Frank, ambaye kaka yake alikuwa fundi wa aluminiamu, alianza pia kujifunza kutengeneza madirisha na milango ya aluminiamu.

Hata hivyo, baada ya mwaka mmoja, kaka yake aliamua kujikita zaidi katika majukumu ya kifamilia na kuachana na muziki, hali iliyomfanya Platform aendelee na muziki peke yake.

Mwishoni mwa mwaka 2019 kuelekea 2020, anasema ndipo alipoachia wimbo wake wa kwanza, ‘Chuki’, ambao ulipokelewa na Watanzania na kuwa mwanzo wa kutambulika kwake katika tasnia ya muziki.


FARAGHA NI MUHIMU

Tofauti na baadhi ya mastaa wanaopenda kuweka wazi maisha yao ya kimapenzi kwenye mitandao ya kijamii, Platform anasema ameamua kutenganisha kazi zake za muziki na maisha binafsi.

Anasema umaarufu una changamoto zake, ikiwemo kuchukiwa na watu ambao mtu hajawahi hata kuwafahamu. Hivyo, anaona ni muhimu kulinda faragha yake na ya mwenza wake.

“Si kila kinachokupa furaha ni lazima ukilete public, kuna vitu vingine ni vya kwako binafsi,” anasema.


NGOMA BILA KUKAA KIMYA

Baada ya kurejea kwenye muziki, Platform amewaomba mashabiki wake kuendelea kumuunga mkono, huku akiwashukuru kwa kuwa naye tangu siku za mwanzo za kazi zake.

Anasema kupitia Triple Release yake yenye nyimbo ‘Siwezi’, ‘Tilalila’ na ‘Nampenda’, amewaandalia muziki wa kufurahia. Video ya ‘Siwezi’ tayari imetoka kupitia YouTube.


WALIOMTANGULIA

Platform anasema moja ya mambo anayojivunia ni kupata msaada wa wasanii na wadau waliomtangulia katika tasnia ya muziki.

Anasema mchango wao haukuwa lazima uwe wa fedha au kufanya naye kazi moja kwa moja, bali pia ulihusisha mawazo, ushauri, connection na kumfungulia njia katika tasnia hiyo.

Anauona mchango huo kuwa muhimu katika kujenga mazingira ambayo wasanii wa kizazi kipya wanaweza kujifunza, kukuza vipaji vyao na kupata nafasi ya kufanya kazi zao.

“Bila wao kutengeneza njia na kutuonesha muziki ni kazi kama kazi nyingine, nadhani tusingekuwa na nafasi hii leo,” anasema.