Jay Mondy & Isabell: Mapenzi, kazi na mafanikio!
Muktasari:
- Ushawishi huo ni fursa kubwa kwao ya kutengeneza fedha, kitu ambacho wamekitumia vizuri na kubadilisha maisha yao na mitazamo ya wengi kuhusu mitandao ya kijamii na utengenezaji wa maudhui.
Mtengeneza maudhui (Content creator) kutokea Tanzania, Jay Mondy pamoja na mpenzi wake, Isabell Afro kutokea Denmark, wanazidi kuwa na nguvu ya ushawishi katika mitandao ya kijamii kupitia kazi yao.
Ushawishi huo ni fursa kubwa kwao ya kutengeneza fedha, kitu ambacho wamekitumia vizuri na kubadilisha maisha yao na mitazamo ya wengi kuhusu mitandao ya kijamii na utengenezaji wa maudhui.
Kile kilichoanza kama utani kwa Jay Mondy akiwa kama dansa na mchekeshaji mtandaoni, kilibadilika na kuwa fursa kubwa ya maisha baada ya kukutana na Isabell Afro aliyeitembelea Tanzania wakati huo.
Jay Mondy alichanganya uwezo wake wa kucheza, yaani dansi pamoja na fursa ya kuzalisha maudhui katika mitandao ya kijamii, uamuzi ambao sasa umemfanya si tu kuwa mtu maarufu Tanzania bali katika nchi nyingi duniani.
Kupitia mitandao ya kijamii kama YouTube, Instagram na TikTok, Jay Mondy na Isabell wamekuwa wakiposti video zilizobeba maudhui ya muziki, dansi, ucheshi na vichekesho. Kwa kuwa sehemu kubwa ya mitandao hiyo inawalipa watengeneza maudhui kama wao, basi kwao tayari ni ajira.
Hii ndio sababu wawili hao wamekuwa akisafiri kwenda nchi mbalimbali duniani kwa ajili ya kutengeneza maudhui yao ambayo yamekuwa yakifuatiliwa na kupendwa na mamilioni ya watu.
Kwa mwaka 2025 pekee, Jay Mondy na Isabell walitembelea nchi 11 kwa ajili ya kuandaa kazi zao, nchi hizo ni Indonesia, Philippines, Ureno, Singapore, Malaysia, Kenya, Tanzania, Uganda, Sweden, Denmark na Bahrain.
"Ulikuwa ni mwaka mkubwa na wa kipekee sana kwetu. Tunajikuta tukitokwa na machozi tunapokumbuka kumbukumbu zote tulizojenga. Kuwa na uwezo wa kushirikisha dunia nzima kile tunachokipenda zaidi ni jambo lisilo la kawaida.
"Kwa kipekee tunawashukuru sana kwa kutazama maudhui yetu na kufuatilia safari yetu pamoja. Haya yote yasingewezekana bila nyinyi. Tutaonana tena mwaka 2026,” Jay Mondy na Isabell walieleza katika taarifa yao kwa wakati huo.
Katika mtandao wa YouTube ambapo wamekuwa wakipata watazamaji wengi zaidi, inaelezwa ndipo hasa wawili wanapopata fedha nyingi, kwa kutazamwa namba zao hakuna ubishi fedha wanayopata si ya kitoto.
Kazi za Jay Mondy YouTube zimetazamwa (views) zaidi ya mara bilioni 17.7 akiwa ndiye Mtanzania pekee mwenye rekodi hiyo, hata wale wanamuziki wa wakubwa wa Bongo Fleva unaowafahamu, hapo kwa Jay Mondy wanangoja.
Mathalani Diamond Platnumz ndiye mwanamuziki wa Bongo Fleva aliyefanya vizuri zaidi YouTube na video zake zimetazamwa mara bilioni 3.9, hivyo kwa hesabu za haraka tu, Jay Mondy amemzidi Diamond 'views' bilioni 13.8.
Tukija kwa Isabell, yeye video zake zimetazamwa YouTube mara bilioni 15.2, hivyo utaona ni kwa kiasi gani kazi ya wawili hao ilivyo na ushawishi mkubwa, kupata namba nyingi kiasi hicho ni ishara tosha wanafuatiliwa katika nchi nyingi.
Machi mwaka huu, Isabell alifikisha wafuatiliaji (subscribers) milioni 10 YouTube na kuweka rekodi kama mtu wa kwanza Denmark kufanya hivyo, na sasa ameshafikia wafuatiliaji milioni 11.3.
Jay Mondy kupitia ukurasa wake wa Instagram, alimpongeza Isabell kwa hatua hiyo akisema anamshukuru Mungu kwa kuwa sehemu ya safari hiyo huku akisisitiza anastahili yote hayo kutokana na jitihada zake.
"Hongera mpenzi wangu kwa kufikia hatua hii kubwa!. Wewe ndiye mtu mwenye bidii kuliko wote niliowahi kukutana nao na ubunifu wako ni wa kipekee sana!,” aliandika Jay Mondy.
Kufikia Mei, Isabell na Jay Mondy waliwafurahisha mashabiki wao baada ya kutangaza kununua nyumba yao nchini Denmark, walieleza nyumba hiyo kubwa na ya kisasa, wataitumia kwa ajili ya kuandaa maudhui (content) yao ya mtandaoni.
"Tunatumaini mmefurahia kuona mahali tulipochagua kuanzisha maisha yetu. Tunawashukuru sana wote mnaotazama video zetu na tuna shauku kubwa ya kutengeneza maudhui mengi zaidi kwa kuwa tumepata nyumba yetu," walieleza wawili hao katika taarifa yao.
Hata hivyo, walisema licha ya kununua nyumba hiyo bado wataendelea kusafiri nchi mbalimbali kuwaletea mashabiki wao kazi ambazo wamekuwa wakiwapa kwa miaka yote. Nchi nyingine ambazo wamewahi kufika ni pamoja na India, Morocco, Brazil, Ufaransa, Afrika Kusini n.k.
Hivyo hadi sasa Jay Mondy na Isabell ambao wamekuwa katika uhusiano kwa zaidi ya miaka minne, wameonyesha jinsi ambavyo mitandao ya kijamii inaweza kubadilisha maisha ya mtu kiuchumi endapo itatumika vizuri kwa malengo ya kufanikisha jambo fulani.