Marioo amshika mkono Malaika Gray
Muktasari:
- Hali hiyo imemfanya Marioo kuonekana kumshika mkono msanii huyo aliyeianza safari yake ya kimuziki rasmi huku akibainisha kwamba wimbo wake huo ameufanyia kila kitu nchini Tanzania kuanzia kuandikwa, kurekodiwa na video yake iliyopigwa katika mitaa ya Dar es Salaam.
MSANII wa Bongo Fleva, Omary Mwanga maarufu Marioo, amekuwa wa kwanza kufanya wimbo na mwimbaji na mtunzi Mtanzania, Malaika Gray uliopewa jina la My Fever.
Hali hiyo imemfanya Marioo kuonekana kumshika mkono msanii huyo aliyeianza safari yake ya kimuziki rasmi huku akibainisha kwamba wimbo wake huo ameufanyia kila kitu nchini Tanzania kuanzia kuandikwa, kurekodiwa na video yake iliyopigwa katika mitaa ya Dar es Salaam.
“Niliutengeneza nyumbani kwa sababu ndiko moyo wangu ulipo Tanzania, na bara ninalolijua na kulipenda. Lakini ninatengeneza muziki kwa ajili ya yeyote atakayeusikia. Nyumbani ndipo unapoanzia, si pale unapoishia,” amesema Malaika Gray.
My Fever ni wimbo wa mapenzi wenye hisia za kiangazi na mvuto kati ya watu wawili, uliojengwa juu ya Afrobeats na Bongo Flava, ukibeba pia mguso wa R&B.
Malaika Gray aliuandika wimbo huo pamoja na Marioo, kisha prodyuza, Abbah Process akamalizia kuufanya kuwa bora.
“Niliuandika nikifikiria hisia ile ambayo kiangazi na mtu huja kwa wakati mmoja. Nilitaka usikike kama Dar,” ameongezea Malaika Gray.
Video ilipigwa kwa siku mbili jijini Dar es Salaam chini ya uongozi wa Joma. Bahari ya Hindi, masoko, daladala, saluni na mitaa ya Dar es Salaam ni sehemu zilizoonekana katika video hiyo.
Malaika ana kipaji cha kweli, na ilikuwa furaha kwangu kushiriki katika wimbo wake wa kwanza. Natarajia tutafanya kazi nyingi zaidi pamoja,” amesema Marioo.
Akiwa amekulia kati ya Tanzania na Afrika Kusini, Malaika Gray anasoma Vocal Performance na Music Business katika Chuo cha Muziki cha Berklee, Boston.
My Fever umetolewa kupitia Africori, kampuni iliyo chini ya Warner Music Group. Wimbo huo unapatikana katika mitandao yote ya kidijitali tangu uachiwe Oktoba 27, 2026.