Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kondela: Kutoka ufundi raba za magari hadi jukwaani na Mondi

Muktasari:

  • Leo, anafahamika kwa sauti yake yenye mahaba na jina la King of Love, lakini nyuma ya nyimbo zake kuna safari iliyomfundisha kuwa mafanikio hayaji kwa siku moja.

KUPIGWA na vibaka, kupoteza nyimbo zake zote, presha ya familia na kufanya kazi ya ufundi wa raba za magari ni sehemu ya maisha aliyopitia msanii wa Bongo Flava, Abdurrahman Mikidadi, maarufu kama ‘Kondela’, kabla ya kuanza kuona matunda ya ndoto yake ya muziki.

Leo, anafahamika kwa sauti yake yenye mahaba na jina la King of Love, lakini nyuma ya nyimbo zake kuna safari iliyomfundisha kuwa mafanikio hayaji kwa siku moja.

Kondela ni mzaliwa wa Kahama, mkoani Shinyanga, ambaye amepitia misukosuko mbalimbali tangu alipoamua kuufanya muziki kuwa sehemu ya maisha yake. Kutoka kuimba kwa kujificha hadi kusimama kwenye jukwaa moja na Diamond Platnumz, safari yake ni ushahidi wa kijana aliyekataa kuachana na ndoto zake.


JINA LA BABU UTAMBULISHO

Kondela anasema jina lake la kisanii alipewa na babu yake, aliyekuwa mwanamuziki wa asili. Jina hilo lina maana ya upendo, lakini awali haikuwa rahisi kwake kulikubali kutokana na utani aliokuwa akikumbana nao shuleni.

Badala ya kuliacha, aliamua kulitumia katika muziki wake na baadaye kujijengea utambulisho wa King of Love, jina linaloendana na aina ya nyimbo zake za mapenzi.

Safari yake ilianza akiwa mdogo, akivutiwa na uandishi wa nyimbo. Anasema baba yake alikuwa akinunua magazeti yaliyokuwa na maneno ya nyimbo, jambo lililomsaidia kujifunza kuandika mashairi.

Akiwa kidato cha kwanza, rafiki yake alimpa changamoto ya kubadilisha hadithi kuwa wimbo. Walichangishana fedha na kwenda studio kurekodi wimbo wake wa kwanza. Hata hivyo, nyumbani hakukuwa na imani kubwa kwamba muziki ungeweza kuwa ajira. Familia yake ilimpa muda wa kuonyesha mafanikio, lakini muda huo ulipopita bila kupata mafanikio aliyotarajia, alikumbwa na mawazo ya kurejea Kahama.

Pamoja na hali hiyo, aliamua kuendelea kupambana.

KUPIGWA, KUPOTEZA NYIMBO

Alipofika Dar es Salaam, Kondela alianza kuandika nyimbo kwa ajili ya wasanii wengine ili kujipatia kipato na kuendeleza maisha yake ya muziki.

Hata hivyo, katika kipindi hicho, alikumbana na changamoto iliyotikisa safari yake. Anasema siku moja, majira ya saa nne usiku alipokuwa akitoka studio, alivamiwa na vibaka waliomjeruhi na kumpora simu iliyokuwa na nyimbo pamoja na mashairi yake.

“Ni changamoto zinazotisha, lakini unapopenda kitu lazima uvumilie ili ufikie ndoto ulizojiwekea,” anasema Kondela.

Kupoteza kazi zake kulikuwa pigo kubwa, lakini hakukufuta azma yake ya kuendelea na muziki.


MOCO GENIUS, URAFIKI WA YAMMI

Katika safari yake ya kujifunza na kukua kisanaa, Kondela alipata nafasi ya kukutana na mtayarishaji wa muziki Moco Genius, ambaye aliwasaidia wasanii waliokuwa chini yake kujifunza mambo mbalimbali kuhusu muziki.

Pia, ana uhusiano wa karibu na msanii Yammi, ambaye aliendelea kuwasiliana naye hata baada ya kuondoka katika kundi la African Princess.

Kondela anasema walifurahi kuona Yammi akipata nafasi katika muziki, akiamini kuwa wanawake hukutana na changamoto nyingi wanapojitafuta katika tasnia hiyo.

NDOTO ZAMFIKISHA, JUKWAANI NA MONDI

Miongoni mwa matukio anayojivunia ni kutumbuiza katika tamasha la Retro Tour, ambako alipata nafasi ya kushiriki jukwaa moja na Diamond Platnumz pamoja na TID.

“TID alinisaidia sana kuniunganisha na Diamond ili kupata nafasi ya kuimba kwenye Retro Tour. Yaani, sikuamini kama jambo hilo lingetokea, lakini limetokea,” anasema Kondela.

Anasema tukio hilo lilikuwa la kipekee katika maisha yake kwa sababu lilimpa nafasi ya kutambua thamani ya kazi aliyokuwa akiifanya kwa muda mrefu.

Kwa sasa, Kondela yupo chini ya lebo ya Gogumaga, ambako anaendelea kujipanga kimuziki na kupanua wigo wa kazi zake.


UFUNDI WA RABA, NDOTO ZA NJE

Pamoja na muziki, Kondela ana kipaji kingine ambacho mashabiki wengi hawakifahamu, ambacho ni ufundi wa kutengeneza raba zinazotumika kwenye magari na vyombo vya moto ili kuzuia chuma kusuguana.

Anasema aliurithi ufundi huo kutoka kwa baba yake na aliufanya kwa miaka mitatu mtaani.

Kwa sasa, macho yake yanaelekea nje ya nchi, akitamani kufanya kolabo na wasanii wanaoimba kwa lugha tofauti ili kupanua wigo wa mashabiki wake.

Mbali na muziki, anasema soka ni mchezo uliomkuza, na hupenda kucheza michezo ya video anapokuwa nyumbani.

Ujumbe wake kwa vijana wanaotaka kuingia kwenye muziki ni kwamba wanapaswa kuuchukulia kama kazi, si starehe.

“Kuchelewa kufikia malengo si kushindwa,” anasema Kondela.