Jesus, Raiane mfano wa upendo ulioshinda visa
Muktasari:
- Gabriel anajulikana na wengi akisifika kwa ustadi, bidii, ufundi na kasi yake ya 'kudribo' mpira awapo uwanjani. Kilele cha mafanikio yake kilikuwa 2019 alipotwaa Copa America akiwa na Brazil - mafanikio ambayo yaliongeza thamani yake kwenye soka la kimataifa.
KATIKA ulimwengu wa soka baadhi ya hadithi za nje ya uwanja hujulikana - moja ya hadithi hizo ni ile ya mshambuliaji wa Arsenal kutoka Brazil, Gabriel Jesus, 28, na mchumba wake Raiane Lima, 24, ambaye wamepitia changamoto nyingi kama mchezo wenyewe.
Gabriel anajulikana na wengi akisifika kwa ustadi, bidii, ufundi na kasi yake ya 'kudribo' mpira awapo uwanjani. Kilele cha mafanikio yake kilikuwa 2019 alipotwaa Copa America akiwa na Brazil - mafanikio ambayo yaliongeza thamani yake kwenye soka la kimataifa.
Hata hivyo, mafanikio yalikuja zaidi akiwa chini ya kocha Pep Guardiola pale Manchester City aliposhinda kila kitu – mataji manne ya EPL, Kombe la FA, mataji matatu ya EFL na Ngao ya Jamii mara mbili. Baada ya kushinda makombe mengi na City, Arsenal ilifanya uamuzi wa kishujaa ikilipa Dola 55 milioni kumchukua.
Sasa Gabriel na Raiane walithibitisha hadharani uhusiano wao walipoonekana wakisubiri ndege binafsi nchini Brazil wakienda Rio de Janeiro kutoka mji alikozaliwa Raiane, Serra Talhada. Kulingana na vyanzo kadhaa inadaiwa penzi lao lilianza Julai 2021. Mchezaji huyo alikuwa amesafiri hadi Serra Talhada, Jimbo la Pernambuco lililopo Kaskazini Mashariki mwa Brazil kwa ajili ya kuwekeza kwenye mradi wa farasi wa mbio fupi.
Katika mahojiano ya awali, Raiane alikanusha uvumi kwamba alikuwa na uhusiano na mwanasiasa maarufu kabla ya kukutana na Gabriel aliyeibuliwa na Klabu ya Palmeiras ya Brazil.
"Nina miaka 20 na nimekuwa mtu mzima kwa muda mrefu. Nilipokutana na Gabriel sikuwa na mtu mwingine, sisi sote tulikuwa single (hatuko katika mahusiano)," alisema Raiane na kauli hiyo iliondoa sintofahamu kuhusu mwanzo wa mapenzi yao.
Uhusiano wa wawili hao ulikua kwa kasi, huku Raiane akionekana mara kwa mara kwenye mechi za Gabriel na kuposti sana picha zao kwenye Instagram. Gabriel akiwa na Man City, alitangaza anatarajia kuwa baba kwa mara ya kwanza mwishoni mwa Septemba 2021 baada ya kufunga bao la ushindi katika mechi ya ugenini iliyoisha kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Chelsea. Aliposti picha ikimuonyesha akiweka kidole gumba mdomoni na kutazama juu na akaandika: "Nimefurahi sana kwa bao hili, ushindi huu muhimu sana kwetu na kwa habari hii nzuri ajabu. Ninatarajia mtoto wangu wa kwanza. Ni sherehe kwa tukio maalum sana!.
"Mungu ambariki na amlinde mtoto wetu wa kike - ndiyo, ni msichana.” Raiane naye alijibu kwa utani: "Asante kwa kufichua bila kuniuliza kwanza" - akionyesha kuwa tangazo hilo lilikuwa zaidi ya furaha kuliko mshangao. Hilo lilijiri mwezi mmoja baada ya wawili hao kukanusha madai ya kuachana yaliyokuwa yameenea Brazil.
Mwandishi maarufu nchini humo, Leo Dias alidai alikuwa ameambiwa na vyanzo vya karibu na wawili hao kuwa waliachana licha ya Raiane kuwa mjamzito. Lakini, ndani ya muda mfupi waliibuka mtandaoni na kukanusha kwa kuposti picha zinazofanana zikionyesha kwamba bado walikuwa pamoja. Moja ya picha ilimuonyesha Gabriel akimkumbatia Raiane huku wakiandika ujumbe: 'mpenzi wangu' kisha kuambatanisha na emoj ya moyo.
Raiane alijifungua mtoto wa kike Mei 2022 - siku mbili tu baada ya Gabriel kushinda tena taji la EPL akiwa na Man City. Mtoto huyo aliyepewa jina la Helena Jesus, mama yake alizungumza kuhusu kuzaliwa kwake baada ya mwezi mmoja. "Nakupenda, napenda kuwa mama yako, napenda harufu yako na amani unayoniletea. Nakupenda kwa kila kitu milele," alieleza Raiane.
Hata hivyo, Januari 2023, uhusiano wao ilibadilika ghafla. Raiane alitangaza kuwa wameachana, ingawa chapisho hilo baadaye lilifutwa Instagram. Alieleza kuwa shinikizo kutoka nje limechangia; "Haikuwa usaliti, bali shinikizo kutoka kwa kila mtu. Siwezi kuvumilia tena," alisema.
Hatua ya kufuta picha zote za Gabriel katika ukurasa wake wa Instagram ilithibitisha kuwa kweli walikuwa wametengana. Tukio hilo lilisababisha mshangao mkubwa kwa mashabiki, kwani lilikuja miezi minane tu baada ya kuzaliwa kwa Helena.
Ila mapenzi yao yalipata nafasi ya nyingine, mwishoni mwa 2023 walionekana tena pamoja jijini London, jambo lililoashiria kurudiana kwao. Kufikia Desemba 2024, Raiane alitangaza kuwa wanatarajia mtoto wa pili - akionyesha kuwa uhusiano wao umekuwa imara zaidi kuliko mwanzo.
Tangazo la ujauzito lilikuwa ishara ya wazi kwamba familia yao inakua. Gabriel na Raiane sasa wanajivunia watoto wawili - binti yao Helena, na mvulana wao aliyezaliwa Juni 2025. Wawili hao wanaoishi London, Uingereza, hatua hii imewafanya kuwa mfano wa upendo ulioshinda changamoto.
Mbali na uhusiano wake na Gabriel, Raiane amejijengea jina kama mshawishi wa chapa mtandaoni akiwa na wafuasi zaidi ya 392,000 Instagram. Maudhui yake yanahusu mitindo, maisha ya kifamilia, na wakati mwingine picha akiwa na watoto wake.
Mrembo huyo mara chache huzungumzia moja kwa moja maisha yao ya kifamilia, amewahi kuandika kuhusu nafasi ya kuwa mama akisema kuwa; Kupata mtoto kunabadilisha kila kitu. Hujui maana ya upendo wa kweli hadi pale utakapomkumbatia mtoto wako!
Ikumbukwe Raiane alizaliwa Februari 8, 2001, huko Serra Talhada, Brazil. Anatoka katika familia ya hali nzuri, ingawa hajawahi kufichua majina ya wazazi wake. Alisoma shule ya msingi na sekondari huko kwao, lakini hakuna taarifa nyingi kuhusu elimu yake ya juu aliyochukua baada ya sekondari.