Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

El Mando: Diamond, Nandy, Harmonize wameniblock

Muktasari:

  • El Mando amejijengea jina kupitia uchambuzi wa muziki wa Bongo Fleva unaohusu ubora wa nyimbo, video, lebo na ushindani wa soko la kimataifa.

MTANGAZAJI wa kipindi cha Recap, Ally Jumanne Mwanga, maarufu El Mando, amefichua changamoto anazokutana nazo katika uchambuzi wa muziki, akiwataja Diamond Platnumz, Nandy, Harmonize, Baraka The Prince, Chino Wana Man na Zuhura Othumani kuwa miongoni mwa wasanii aliowahi kutofautiana nao, huku baadhi wakim-block mitandaoni.

El Mando amejijengea jina kupitia uchambuzi wa muziki wa Bongo Fleva unaohusu ubora wa nyimbo, video, lebo na ushindani wa soko la kimataifa.

Akizungumza na Mwanaspoti katika mahojiano maalum, mtangazaji huyo amefunguka kuhusu safari yake ya kazi, namna anavyokabiliana na ukosoaji kutoka kwa wasanii, mchango anaotaka kuutoa katika muziki wa Tanzania pamoja na maisha yake nje ya utangazaji.


Diamond, Nandy, Harmonize wam-block

El Mando anasema kazi yake ya kuchambua muziki imemweka katika mazingira ya kutofautiana na baadhi ya wasanii, hasa maoni yake yanapogusa ubora wa kazi zao au mafanikio yao katika soko la muziki.

Anawataja Diamond Platnumz, Baraka The Prince, Nandy, Harmonize, Chino Wana Man na Zuhura Othumani kuwa miongoni mwa wasanii aliowahi kupata nao changamoto zinazohusiana na kazi yake, huku baadhi yao wakifikia hatua ya kum-block kwenye mitandao ya kijamii.

Anasema hali hiyo inatokana na namna baadhi ya wasanii wanavyopokea uchambuzi, ambapo wakati mwingine maoni kuhusu kazi zao huchukuliwa kama mashambulizi binafsi badala ya kuwa sehemu ya mjadala wa kitaalamu unaolenga kuboresha tasnia.

“Kitu nisichopenda ni wasanii kuchukulia ukosoaji kwa hisia binafsi. Wengi hawakuamini kama nafanya kazi yangu kwa uhuru, walihisi natumwa, lakini baadaye wameanza kuelewa na kunipa ushirikiano,” anasema.

Hata hivyo, anabainisha kuwa hali imeanza kubadilika, kwani baadhi ya wasanii wameanza kuelewa namna anavyofanya kazi na kumpa ushirikiano tofauti na ilivyokuwa awali.


Safari ya utangazaji ilianza 2018

El Mando anasema safari yake ya utangazaji ilianza mwaka 2018 alipokuwa akijitolea katika kituo cha televisheni cha TV One, kabla ya kujiunga rasmi na Bongo5 kama mtangazaji.

Anasema katika kipindi hicho, mtangazaji aliyemvutia na kumtia moyo zaidi alikuwa B Dazen, ambaye alimtazama kama mmoja wa watu waliompa hamasa ya kuendelea na kazi hiyo.

Kwa sasa anaendesha kipindi cha Recap kupitia tovuti ya Bongo5.com, ambacho kimekuwa kikijikita katika uchambuzi wa muziki, video, lebo, mafanikio ya wasanii na namna muziki wa Tanzania unavyoshindana katika soko la kimataifa.


Mbosso kutoka WCB, Harmonize na uchambuzi wake

Miongoni mwa uchambuzi wake ulioibua mijadala ni makala yenye kichwa “RECAP: Mbosso alikosea kutoka WCB??”, iliyojikita katika safari ya msanii Mbosso baada ya kuondoka katika lebo ya WCB Wasafi na kuangalia mwelekeo wa kazi zake.

Pia amewahi kuchambua video ya Harmonize ya I Made It, akieleza namna ubora wa kazi hiyo unavyoweza kuchangia kukuza muziki wa Bongo Fleva katika soko la kimataifa.

Katika uchambuzi mwingine, El Mando amekuwa akizungumzia ushindani wa lebo za muziki nchini, akiwahi kueleza kuwa WCB Wasafi ndiyo inayoongoza kwa streams na viewers kwenye majukwaa ya kidijitali nchini Tanzania.


Muziki ni biashara, si burudani pekee

El Mando anasema lengo la uchambuzi wake ni kuonesha kuwa muziki haupaswi kutazamwa kama burudani pekee, bali ni biashara inayoweza kuzalisha ajira, mapato na fursa kwa wasanii pamoja na watu wengine wanaofanya kazi ndani ya tasnia.

Anasisitiza umuhimu wa kutumia takwimu sahihi za views na streams kupima mafanikio ya wasanii, badala ya kutegemea hisia au taarifa zinazozagaa mitandaoni.

Kwa mtazamo wake, ubora wa video, matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii na mikakati ya kuitangaza kazi ni miongoni mwa mambo yanayoweza kumsaidia msanii kufikia soko kubwa zaidi.

Anaamini muziki wa Tanzania una nafasi ya kushindana kimataifa, lakini ili kufikia hatua hiyo, wasanii wanahitaji kuwekeza katika ubunifu, ubora wa kazi na mikakati ya kibiashara.


Taarifa sahihi ni changamoto

Mbali na kutofautiana na baadhi ya wasanii, El Mando anasema ukosefu wa taarifa sahihi ni moja ya changamoto zinazomkabili katika kazi yake.

Anabainisha kuwa tasnia ya burudani mara nyingi hutegemea taarifa zinazotoka mitandaoni, ambazo si zote huwa na uhakika, hivyo anahitaji kufanya utafiti na kujifunza kila siku ili kuhakikisha uchambuzi wake unakuwa na msingi wa taarifa sahihi.

Pia anasema mabadiliko ya teknolojia na mitandao ya kijamii yanamlazimu kuendelea kujifunza ili kuendana na mazingira mapya ya muziki na namna kazi za wasanii zinavyosambazwa na kupimwa.


Diamond, Kiba, Marioo, Mbosso na Zuchu

Akizungumzia wasanii anaowaona wakifanya vizuri kwa sasa, El Mando anawataja Diamond Platnumz, Ali Kiba, Marioo, Mbosso na Zuchu.

Anasema wasanii hao ni miongoni mwa majina yanayoendelea kuwa na nafasi kubwa katika muziki wa Tanzania kutokana na kazi zao na namna wanavyoendelea kuvutia mashabiki.

Kwa ujumla, anaamini ushindani katika muziki unapaswa kuwa chachu ya wasanii kuboresha kazi zao, badala ya kuishia katika malumbano au kuchukulia maoni tofauti kama uadui.


Maisha nje ya Recap

Mbali na kazi zake za uchambuzi wa muziki, El Mando anajieleza kuwa ni kijana mchangamfu anayependa kubadilishana mawazo na watu wa aina mbalimbali.

Anasema bado hajaoa, lakini yupo katika mahusiano makini.

Pia ni mpenzi mkubwa wa michezo, hasa mpira wa miguu, ambapo ni shabiki wa Simba Sports Club nchini Tanzania na Manchester United katika soka la Ulaya.

Michezo mingine anayopenda ni kuogelea na mpira wa kikapu, akiwa shabiki wa timu ya Dar City.

Kutokana na kazi zake, amepata nafasi ya kusafiri na kuripoti mechi katika nchi mbalimbali, zikiwemo Misri, ambako alitembelea Cairo, Qatar, Afrika Kusini, Rwanda, Uganda na Kenya.


Ndoto ya kuwa mtangazaji wa kimataifa

Mzaliwa wa Singida, El Mando ni mtoto wa mwisho katika familia ya Bwana na Bi Jumanne Mwanga.

Anasema ndoto yake kubwa ni kuwa mtangazaji wa kimataifa pamoja na mfanyabiashara mkubwa, huku akiwa na mchango katika kukuza muziki wa Afrika.

Licha ya changamoto na upinzani anaokutana nao kutokana na uchambuzi wake, anasema hana mpango wa kurudi nyuma, kwani anaamini ukosoaji wa kujenga ni sehemu muhimu ya maendeleo ya tasnia.

Kwa El Mando, mafanikio ya muziki wa Tanzania hayatategemea umaarufu wa wasanii pekee, bali pia ubora wa kazi, uwekezaji, takwimu sahihi na uwezo wa kukabiliana na ushindani wa kimataifa.