Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Baada ya miezi ya mateso, Majaliwa afika kwa Mkubwa Fella

FELLA Pict

Muktasari:

  • Majaliwa alifika nyumbani kwa Mkubwa Fella Julai 25, 2026 kwa lengo la kumjulia hali, kuzungumza naye na kuona maendeleo yake baada ya kipindi kirefu ambacho afya yake ilikuwa gumzo kwenye jamii ya burudani.

Baada ya miezi kadhaa ya mapambano ya afya yaliyowafanya mashabiki wa muziki na wadau mbalimbali kuendelea kumwombea, hatimaye mdau wa muziki na mlezi wa vipaji nchini, Said Fella maarufu kama Mkubwa Fella, amepata faraja kubwa baada ya kutembelewa na Waziri Mkuu Mstaafu, Kassim Majaliwa.

Majaliwa alifika nyumbani kwa Mkubwa Fella Julai 25, 2026 kwa lengo la kumjulia hali, kuzungumza naye na kuona maendeleo yake baada ya kipindi kirefu ambacho afya yake ilikuwa gumzo kwenye jamii ya burudani.

Mbali na maneno ya faraja, Majaliwa alimkabidhi Mkubwa Fella msaada wa Sh20 milioni, hatua iliyogusa wengi na kuonekana kama ishara ya kuthamini mchango wake mkubwa katika kuendeleza muziki wa Tanzania.

FEL 01

Majaliwa afanya jambo lililogusa wengi

Katika ziara hiyo, kilichowavutia wengi zaidi ni namna waziri mkuu huyo mstaafu alivyoamua kushiriki kufanya mazoezi mepesi ya viungo pamoja na Mkubwa Fella.

Kitendo hicho kilionekana kuwa zaidi ya ziara ya kawaida ya kumjulia hali, bali kilikuwa ni kumpa hamasa na kumuonyesha kuwa bado anaungwa mkono katika safari yake ya kurejesha afya yake.

Wawili hao walionekana wakiwa katika hali ya furaha huku wakifanya mazoezi hayo ambayo ni sehemu ya hatua za Mkubwa Fella kuendelea kujenga nguvu za mwili.

Kwa mashabiki waliokuwa wakifuatilia hali yake tangu alipoanza kuugua, hatua hiyo imeonekana kuwa ishara kubwa kuwa mambo yanaendelea kuwa mazuri.

FEL 02

Safari ya ugonjwa ilivyomtikisa Mkubwa Fella

Safari ya afya ya Mkubwa Fella imekuwa na changamoto kubwa na imekuwa ikifuatiliwa kwa karibu na wadau wa muziki nchini.

Mwanamuziki huyo ambaye kwa miaka mingi amekuwa nyuma ya mafanikio ya wasanii wengi, alikumbwa na changamoto ya kiafya iliyomfanya kupunguza shughuli zake za kawaida na kuanza safari ya matibabu.

Katika kipindi hicho, taarifa kuhusu hali yake zilisambaa kwa kasi huku mashabiki wakitaka kufahamu kinachoendelea kwa mtu ambaye amekuwa sehemu muhimu ya historia ya Bongo Fleva.

Mwanaspoti lilikuwa miongoni mwa vyombo vya kwanza kufuatilia kwa karibu hali yake na lilizungumza na Mkubwa Fella mwenyewe pamoja na mke wake kuhusu safari hiyo ya ugonjwa, hatua za matibabu na maendeleo aliyokuwa akiyapata.

Katika mahojiano hayo, lilielezwa kuwa kipindi cha mwanzo kilikuwa kigumu kwake kutokana na kupungua kwa nguvu za mwili na kushindwa kufanya baadhi ya shughuli alizokuwa akizifanya kawaida.

FEL 03

Mke wake afichua hali halisi

Mke wa Mkubwa Fella, Sweet Fella aliwahi kueleza namna familia ilivyopitia kipindi kigumu wakati wa ugonjwa huo, huku akisema walikuwa wakimpa uangalizi mkubwa na kuhakikisha anapata matibabu yanayohitajika.

Alieleza pamoja na changamoto zilizokuwepo, walifarijika kuona watu mbalimbali wakisimama pamoja nao na kutoa moyo.

Katika kipindi hicho, Mkubwa Fella pia aliendelea kupokea wageni mbalimbali wakiwemo wasanii, viongozi na wadau wa muziki waliokwenda kumuona na kumtia nguvu.

Mkubwa Fella: “Nimeumwa sana, lakini Mungu amenisaidia”

Katika mazungumzo yake na Mwanaspoti, Mkubwa Fella aliweka wazi uzito wa kipindi alichopitia, akisema ugonjwa huo ulimfanya kupitia wakati mgumu lakini hakupoteza matumaini.

Amesema hatua aliyokuwa amefikia ya kuanza kutembea na kufanya mazoezi ilimpa faraja kubwa baada ya kipindi cha mateso.

“Ukweli nimeumwa sana, nimepitia kipindi kigumu, lakini namshukuru Mungu kwa sababu sasa naendelea vizuri na ninaendelea kufanya mazoezi,” amesema Mkubwa Fella.

Kauli hiyo iliwapa matumaini mashabiki waliokuwa wakifuatilia hali yake kwa karibu.

FEL 05

Mchango wake Bongo Fleva

Mkubwa Fella si jina geni kwenye muziki wa Tanzania. Kwa miaka mingi amekuwa mmoja wa watu walioandika historia ya Bongo Fleva kupitia kazi yake ya kugundua, kulea na kusimamia vipaji mbalimbali.

Kupitia lebo yake ya Mkubwa Fella Entertainment, amekuwa sehemu ya safari za wasanii waliokuja kuwa majina makubwa katika muziki wa Tanzania.

Miongoni mwa wasanii waliopita kwenye mikono yake ni pamoja na Diamond Platnumz, ambaye alianza safari yake ya muziki chini ya usimamizi wake kabla ya kuwa mmoja wa wasanii wakubwa Afrika.

Mbali na Diamond, Mkubwa Fella amekuwa akihusika katika kukuza vipaji vya vijana wengi na kutoa mchango mkubwa katika ukuaji wa tasnia ya burudani.

FEL 04

Sasa aanza ukurasa mpya

Baada ya kipindi cha majaribu, kuonekana kwake akiwa anafanya mazoezi pamoja na Majaliwa ni hatua inayowapa matumaini wengi kuwa safari yake ya kurejea katika hali yake ya kawaida inaendelea.

Kwa sasa, Mkubwa Fella anaendelea na mpango wa kurejesha nguvu za mwili huku akiendelea kupata sapoti kutoka kwa familia, marafiki, wasanii na wadau mbalimbali wa muziki.

Ziara ya Majaliwa imekuwa kama ujumbe mwingine kuwa mchango wa Mkubwa Fella haujasahaulika na kwamba mtu aliyesaidia kukuza vipaji vya wengine naye anastahili kushikwa mkono wakati wa changamoto.