Yanga kunoa makali ya USM Alger kwa Mkamba Rangers

Dar es Salaam. Timu ya daraja la pili ya Mkamba Rangers ya Kilomero, leo inacheza mechi  ya kirafiki na Yanga, mchezo ambao umepangwa kufanyika kwenye uwanja wa CCM, Mkamba Kilosa mkoani Morogoro.

Mchezo huo ni sehemu ya maandalizi kwa timu zote mbili, huku Yanga ikiajiandaa na mechi za Ligi Kuu ya Tanzania Bara na mchezo wa kombe la Shirikisho dhidi ya timu ya USM Alger ya Algeria ambao umaengwa kufanyika Agosti 19 kwenye uwanja wa Taifa jijini.

Mmoja wa viongozi wa Mkamba Rangers, Juma Ligonela alisema kuwa waliongea na uongozi wa klabu ya Yanga kuhusiana na mchezo huo na kukubaliana. Alisema kuwa mchezo huo pia utakuwa fursa kwa timu yao kuwapima wachezaji wapya na kuwaona wachezaji nyota wa yanga ambao wamejiunga msimu huu.

“Tumejiandaa vyema kwa ajili ya mchezo huo na utakuwa wa pili kucheza na timu za Ligi Kuu ya Tanzania Bara. Mara ya kwanza walicheza na timu Mbeya City ya Mbeya na baadhi ya timu nyingine na kupata matokeo mazuri,” alisema Ligonela.

Kocha wa Mkamba Rangers, Juma Omary Mpoka alisema kuwa watatumia fursa hiyo kukitambulisha kikosi chao na wachezaji wapya ambao wamesajiliwa msimu huu.

Mpoka alisema kuwa wamesajili wachezaji wengi chipukizi na wenye vipaji  hivyo Yanga itegemee kupata upinzani mkali.

“Pia tumesajili wachezaji wakongwe, tuna Semmy Kessy na wengine ambao wataonekana wakaonekana kwa mara ya kwanza kwenye mechi hiyo,” alisema Mpoka.