Simba yaikasa rekodi Yanga
Dar es Salaam. Miaka 36 imepita tangu Rashid Hanzuruni alipofunga bao wakati Simba na Yanga zilipokutana kwa mara ya kwanza Aprili 29, 1982, katika mchezo wa Ligi Kuu Bara.
Hanzuruni alifunga bao dakika 2, na kuipa Yanga ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Simba, ikiwa ni mara ya kwanza na kesho itakuwa ni mara ya pili kwa timu hizo kukutana tarehe hiyo.
Pamoja na Yanga kupata ushindi katika mchezo huo wa kwanza bado rekodi zinaonyesha timu hizo zimekutana mara tisa mwezi Aprili katika michezo ya Ligi Kuu Bara huku sare zikiwa nne, Simba ikishinda mara tatu na Yanga ikishinda mara mbili.
Mechi iliyozalisha mabao mengi katika mwezi huu ni ile iliyofanyika Aprili 18, 2010 ambapo Simba iliichapa Yanga mabao 4-3.
Mabao ya Simba siku hiyo yalifungwa na Mussa Hassan Mgosi aliyefunga mawili, Uhuru Seleman na Hillay Echesa wakati mabao ya Yanga yalipachikwa wavuni ni Jerryson Tegege aliyefunga mawili na Athuman Iddi 'Chuji'.
Makocha waionya Simba
Makocha mbalimbali wameionya Simba kuchukua tahadhari na kuacha kuidharau Yanga kwani mchezo huo huwa hautabiriki.
Kocha wa Lipuli, Seleman Matola alisema mechi ya Simba na Yanga siku zote huwa ina mambo mengi nje ya uwanja hivyo Simba isijidanganye kuwa ina kikosi bora cha kuipa matokeo Jumapili.
"Enzi nacheza, Simba tuliwahi kufungwa na Yanga mabao matatu tena timu yetu ikiwa bora mno. Kabla ya mchezo tuliamini tunashinda, lakini kibao kikageuka uwanjani.
"Mechi hizi uwa zina mambo mengi mno na hazitabiriki, ni kweli kwa mtizamo wa nje Simba ina kikosi bora hivi sasa lakini kwa Yanga hata ikiwa dhaifu namna gani inapokutana na Simba mechi ni ngumu," alisema Matola.
Kocha wa Njombe Mji, Mrage Kabange alisema mtizamo wa wengi hivi sasa ni kuwa Simba itashinda, lakini akaungana na Matola kusisitiza kuwa siyo kwa Yanga.
"Mechi hiyo itaamuliwa na mbinu za makocha, lakini udhaifu wa Yanga na ubora wa Simba hauwezi kutoa matokeo kwenye mechi kama hiyo," alisema Kabange.
Kocha wa JKT Tanzania, Bakari Shime hakutaka kuuchambua kwa undani mchezo huo, lakini amesisitiza mshindi atapatikana kutokana na namna timu ilivyojiandaa.
"Maandalizi yana vitu vingi, saikolojia ya wachezaji inahitajika, hivyo ushindi hapo utategemea na namna timu ilivyoandaliwa," alisema Shime.