Ngoma na Tambwe wapindua meza

Muktasari:

>>Yanga ilikuwa ikijiandaa kuwafanyia majaribio nyota watano akiwamo Mkongomani Chris Magalu ili wawili kati yao wasainishwe kuchukua nafasi ya Tambwe na Ngoma

MABOSI wa Yanga na hata mashabiki wao walikuwa wakipiga hesabu kali ya kushuhudia nyota watano wa kigeni wakitua Jangwani ili kuwania nafasi ya kusajili kuchukua nafasi za Amissi Tambwe na Donald Ngoma.

Hata hivyo mpango huo umekufa zikiwa zimesalia saa chache kabla ya dirisha dogo la usajili kufungwa usiku wa kesho Ijumaa, baada ya mastraika hao kupindua meza bila kutarajiwa.

Tambwe ambaye amerejea kutoka benchi la majeruhi akiwa fiti, jana Jumatano kwenye mazoezi alifunga bonge la bao kiasi cha kuwafanya makocha wake, George Lwandamina na Shadrack Nsajigwa kutabasamu, amezuia usajili wa wageni hao.

Yanga ilikuwa ikijiandaa kuwafanyia majaribio nyota watano akiwamo Mkongomani Chris Magalu ili wawili kati yao wasainishwe kuchukua nafasi ya Tambwe na Ngoma ambaye amekuwa msumbufu tangu mapema mwaka huu.

Hata hivyo, Ngoma amemalizana na mabosi wake kwa kuahidi kurudi kikosini akiwa mtiifu huku Tambwe akirejesha mvua ya mabao Jangwani baada ya kuanza mazoezi na wenzake na kuonekana kama hakuwa majeruhi.

Kurudi kwa Mrundi huyo mkongwe kutawafanya mabosi wa klabu hiyo kuingia katika utata wa maamuzi gani yafanyike juu ya kufanya usajili ambao walipanga kuufanya.

Mabosi wa klabu hiyo walikuwa tayari na majina ya washambuliaji sita wa maana katika simu zao wakisubiri maamuzi ya hatma ya Tambwe na Ngoma ili waweze kuwashusha nchini kwa majaribio mafupi.

Katika idadi hiyo ya washambuliaji hao, jina kubwa ni lile la Magalu aliyekuwa Mfungaji Bora katika Ligi Kuu Zambia akifunga mabao 23 ambaye aliwavutia vigogo hao.

Magalu ambaye uwezekano wa usajili wake uliibuka wiki hii baada ya kuingia katika malumbano na klabu yake ya Lusaka Dynamo ya Zambia iliyoshindwa kumpatia gari ya kisasa kama walivyokubaliana wakati akisaini katika klabu hiyo.

Mbali na Magalu, wengine ni Badara Kella, Bensua Da Silva, Togui William na Adam Zikiru kutoka Ghana ambaye alinyakuliwa na Zesco ya Zambia kipindi Yanga wakiendelea kupiga hesabu kwa vidole ili kumnasa.

Mpango huo ni wazi hautakuwa na afya tena katika utekelezaji kutokana na kitendawili kilichopo sasa ni nani akatwe katika wawili hao.

Habari za uhakika ni kwamba Yanga ambayo bado haijamalizana na Ngoma juu ya kesi yake ya kurudi kwao Zimbabwe bila ruhusa,  Mwanaspoti linafahamu kuwa klabu hiyo haitaweza kumuacha kwa sasa kutokana na muda mfupi uliobaki kabla ya kufungwa kwa usajili kesho saa sita kamili usiku.

Mmoja wa mabosi wa Yanga alilidokeza Mwanaspoti kwa muda uliosalia ni vigumu kwao kuwasajili wachezaji wengine wapya kwa maana kwamba timu yao itaendelea kutegemea huduma za Ngoma na Tambwe katika mechi za kimataifa. Hao wataungana na Fiston Kayembe, Thabani

Kamusoko, Kabamba Tshishimbi, Obrey Chirwa na kipa Youthe Rostand kwa nyota wa kigeni.

Lakini Yanga isipokuwa makini inaweza kulia katika kutupia nyavuni iwapo nyota hao wakipata pancha mbele ya safari.