Mastaa watatu wa Yanga waitwa Takukuru, Chirwa ruksa
Muktasari:
Taarifa kutoka ndani ya klabu hiyo zilizothibitishwa na kiongozi mmoja, ambaye hakupenda kutajwa jina lake gazetini, zinasema Takukuru mara baada ya kutua Yanga wameomba mikataba ya wachezaji watatu wa timu kwa uchunguzi zaidi.
HUKO Jangwani yaliko makao makuu ya Yanga, kumeanza kufukuta baada ya majina matatu ya nyota wa klabu hiyo kutua Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), huku mikataba yao nayo ikiwasilishwa katika taasisi hiyo.
Taarifa kutoka ndani ya klabu hiyo zilizothibitishwa na kiongozi mmoja, ambaye hakupenda kutajwa jina lake gazetini, zinasema Takukuru mara baada ya kutua Yanga wameomba mikataba ya wachezaji watatu wa timu kwa uchunguzi zaidi.
Mikataba ambayo imeombwa na Takukuru ni wa winga kinda, Burhan Akilimali ‘Kiberenge’ aliyesajiliwa msimu uliopita. Mbali na Akilimali pia Yanga imepeleka taarifa ya usajili wa beki Mkongomani, Fistoo Kayembe, ambaye alikaribia kabisa kutua Yanga.
Kayembe alisajiliwa na Yanga, lakini klabu yake ya Sangabalenge ikagoma kumwachia ikidai bado ana mkataba, hivyo kuzuia hati yake ya uhamisho (ITC).
Pia, klabu hiyo ilitaka ilipwe Dola 5000 (Sh11 milioni) kama ada ya uhamisho, lakini Yanga iligoma na kukubaliana kumsubiri amalize mkataba.
Mbali na hao pia mkataba wa kiungo kiraka, Jafary Mohamed aliyesajiliwa msimu huu akitokea Majimaji ya Songea nao umepelekwa Takukuru. Hata hivyo, inaelezwa kuwa baadhi ya vigogo wa Yanga nao wanaweza wakaitwa kujieleza juu ya mambo mbalimbali ya kiutendaji ndani ya klabu hiyo.
Kutokana na taarifa hiyo, Mwanapoti lilimtafuta Msemaji wa Takukuru, Mussa Misalaba ambaye hakukubali wala kukataa juu ya suala hilo, lakini akasema hayuko kwenye wakati sahihi kulizungumzia.
“Kwa sasa siwezi kusema hilo lipo au halipo, hatuoni kama kuna sababu ya kulitolea ufafanuzi kwa wakati huu, kama tutakuwa na kitu cha kuwaeleza tutafanya hivyo wakati ukifika,” alisema Misalaba.
CHIRWA RUKSA
Katika hatua nyingine mabosi wa Yanga wameridhia aliyekuwa straika tegemeo wa timu hiyo, Obrey Chirwa kurejea kama tu, watakubaliana na benchi la ufundi.
Bosi mmoja wa Kamati ya Usajili ya Yanga, alisema benchi lao la ufundi limeanza kuangalia juu ya matumizi ya Chirwa na Heritier Makambo kwenye eneo la ushambuliaji na kubaini inaweza kuongeza makali na kuwa tishio zaidi.
Inaelezwa kuwa mabosi hao wameambiwa endapo Chirwa atarejea na kucheza sambamba na Makambo, anaweza kuifanya safu ya Yanga kuwa tishio na kutupia nyavuni kadri watakavyo.
Hata hivyo, mabosi hao wameelezwa kuwa hatima ya kurejea ama kutorejea kwa Chirwa, kutategemea na uamuzi wa mwisho kutoka kwa Kocha Mkuu, Mwinyi Zahera ambaye kwa sasa yuko kwenye majukumu ya timu ya Taifa ya DR Congo.
“Makocha wamesema ukiacha tabia yake, lakini kama dili hilo litafanikiwa Chirwa anaweza kuongeza uhai kwa Makambo kwa kumwongezea makali zaidi ya kufunga.
“Kazi ya kuifanyia tathimini pacha hiyo imeanza, unajua Chirwa ni mbishi kwa mabeki na anajua kupambana hivyo, wakati akiwania mipira kazi ya Makambo itakuwa ni kufunga tu. Ngoja tutaona hatima yake kwa Zahera,” alisema bosi huyo.