Lechantre ashusha Kinda Simba

Monday April 16 2018

 

By THOBIAS SEBASTIAN

SIMBA leo inaingia Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, kusaka pointi tatu muhimu mbele ya Tanzania Prisons huku kazi ya kusaka taji ikikabidhiwa kwa Emmanuel Okwi na John Bocco, na juzi ilijifua kwenye uwanja wake wa mazoezi wa Boko Veteran, lakini wakakutana na saprize.

Wachezaji na mashabiki waliokwenda kutazama mazoezi hayo, walipigwa mshangao baada ya mgeni mmoja kuibuka kwenye mazoezi hayo akiwa sambamba na kocha, Pierre Lechantre.

Mgeni huyo alikuwa straika kinda wa Allience ya Ujerumani, Geofrey Kombole ambaye alifanya majaribio kikosini hapo wakati akisubiri dili kukamilika.

Hata hivyo, Lechnatre amesema kuwa Kombole ni straika matata na kama ataonyesha uwezo basi atakuwa mchezaji wa kwanza kumsajili.

Kambole alitumia saa 1:30 kufanya mazoezi na kikosi cha kwanza cha Simba chini ya uangalizi Lechantre na wasaidizi wake Masoud Djuma na Mohammed Habib.

Lechantre katika mazoezi ya Simba juzi Jumamosi aligawa timu mbili ya kwanza ikiwa na Said Mohammed ‘Nduda’, Vincent Costa, Ally Shomary, Salim Mbonde, Jamali Mwambeleko, Haruna Niyonzima, Mzamiru Yassin, Laudit Mavugo na Kombole.

Nyingine ilikuwa Emmanuel Mseja, James Kotei, Paul Bukaba, Kelvin Faru, Said Ndemla, Mohammed Ibrahim, Mohammed Hussein, Moses Kitandu, Juma Liuzio, Rashid Juma.

Baada ya kupangwa kwa timu hizo walicheza kama mechi dhumuni lilikuwa kuangalia uwezo wa katika kukaba na kushambulia kwani Lechantre alikuwa mkali kwa ambaye atafanya vibaya lakini kuangalia pia uwezo Kombole ambaye aliweza kufunga goli moja safi kumuacha Nduda akishangaa na alipokea pasi safi kutoka kwa Niyonzima.

Lechantre alisema alimuona Kambole katika mechi za vijana katika Uwanja wa JK Kidongo Chekundu akiwa anafanya mazoezi na alivutiwa na uwezo wake kwani, anapenda wachezaji vijana na alimwambia kabla ya kurudi Ujerumani afike kufanya mazoezi na Simba.

“Nilimuona akicheza vizuri katika mashindano ya vijana alinivutia na ndio maana nimemwambia kabla ya kuondoka kurudi Ujerumani afanye kwanza mazoezi na Simba, kama atafanya vizuri naweza kufanya kitu kwa ajili yake,” alisema.

Akizungumza baada ya mazoezi hayo, Kambole alisema: “Lechantre aliniona pale JK na baada ya mashindano kumalizika aliniambia nifike hapa kufanya mazoezi. Nina uwezo wa kucheza katika timu yoyote na nitakaa hapa ataniangalia kama nitafanya vizuri au nitashindwa,” alisema Kombole.