Kichuya ateka kijiji
Muktasari:
Tangu alipotua Simba akitokea Mtibwa Sugar, Kichuya amekuwa katika kiwango bora
Mwanza. Mashabiki wa Ushirombo na Mbogwe mkoani Geita wamemwambia winga wa Simba, Shiza Kichuya kuwa furaha yao ipo kwake pale atakapowanyamazisha Wanajangwani kesho Jumapili.
Mechi hiyo ya Ligi Kuu itachezwa kesho kwenye Uwanja wa Taifa ambapo Simba wanahitaji ushindi ili kuweza kujihakikishia kutwaa ubingwa msimu huu.
Kichuya amekuwa na rekodi nzuri ya kuwafunga Yanga ambapo katika mechi tatu walizocheza Winga huyo amefunga bao kila pambano walilocheza na watani wao.
Winga huyo alifunga bao la kwanza mwaka 2016 katika mchezo uliomalizika kwa sare ya 1-1 kisha akapachika tena Februari 25 mwaka 2017 ambapo Simba walishinda 2-1 na msimu huu kwenye mtanange wa raundi kwanza alifunga bao kwenye mchezo waliotoka sare ya 1-1.
Mashabiki hao walisema licha ya kuwepo kwa washambuliaji wengine kwenye kikosi hicho, lakini wanamtegemea sana Kichuya kuwanyamazisha Yanga.
Shabiki Sospeter Magessa alisema wanatamani kuona rekodi ya Kichuya ya kuwafunga Yanga ikiendelea katika mpambano huo.
“Kichuya tunamtegemea najua watamkaba sana, lakini mwisho wa siku wataona mpira huko nyavuni” alisema Magessa.
Shabiki Kazobya Kanzu alisema pamoja na Simba na washambuliaji wengi, lakini Kichuya lazima awafunge kwani mabeki wa Yanga watakuwa makini na Emmanuel Okwi na John Bocco.
Nassoro Mohamed alisema kwa mabeki wa Yanga wa msimu walivyokuwa uchochoro lazima Kichuya awafunge tu.