Fedha zaleta mzuka Yanga

Muktasari:

  • Hata hivyo, unaambiwa lile bakuli lililoasisiwa Jangwani, limeanza kulipa na mabosi wa klabu hiyo wamewawatia ndimu wana Yanga kuendelea kuangusha moja moja, ili mambo yazidi kwenda vizuri wakati Ligi Kuu Bara ikianza kushika kasi.

HUKO mitaani ilikuwa gumzo kubwa. Mashabiki wa Simba walipata pa kusemea baada ya kusikia Yanga inatembeza bakuli wakiomba kuchangiwa fedha za kuisaidia klabu yao. Hata baadhi ya Wana Yanga wenye roho nyepesi nao walianza kuingia baridi kila walipokuwa wakitaniwa na wenzao wa Simba kuwa, kutoka kuwa wazee wa Kimataifa hadi kuwa ombaomba Matonya.

Hata hivyo, unaambiwa lile bakuli lililoasisiwa Jangwani, limeanza kulipa na mabosi wa klabu hiyo wamewawatia ndimu wana Yanga kuendelea kuangusha moja moja, ili mambo yazidi kwenda vizuri wakati Ligi Kuu Bara ikianza kushika kasi.

Mabosi hao wa Yanga walidai harambee inayoendelea imewasaidia hata kuisafirisha timu kwenye pambano lao la kumalizia mechi za CAF dhidi ya Rayon Sports na kwamba wanaamini zoezi likiendelea waliowakejeli watatulia wenyewe.

Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga, Omary Kaya ameliambia Mwanaspoti kuwa michango ya mashabiki wao tangu mwezi uliopita, wamefanikiwa kuipata zaidi ya Sh30milioni ambazo zimewasaidia kwa mambo mbalimbali ikizingatiwa, hali yao kiuchumi bado haijakaa vizuri.

Kaya alisema kwa kuwa walishamaliza jukumu la mechi za kimataifa, anaamini nguvu inastahili kuelekezwa kwenye kuisaidia timu katika Ligi Kuu Bara inayotarajiwa kuendelea wikiendi hii baada ya kusimama kwa muda kupisha mechi za kimataifa kwa timu za taifa.

Bosi huyo mkuu wa utendaji wa kazi za kila siku za klabuni hapo alisema endapo michango hiyo itaendelea kwa kasi sasa inaweza kuja kuibeba klabu yao katika mbio za ligi kuu bara.

“Wengine wanaweza kudharau hii michango, lakini kwa wanaochangia wanatakiwa kutambua hii ni hatua nzuri kwa klabu hasa baada ya kufanikisha kugharamia safari yetu ya Rwanda,” alisema Kaya.

“Tulipokwenda Rwanda mimi najua ni jinsi gani hizi fedha zilitumika kuhakikisha timu inaenda na kurudi salama hapa nchini, haya ni mafanikio ya nguvu ya wanaotuchangia na tunawashukuru wote waliojitoklea na tunaomba waendelee.”

“Michango hii kama itaendelea nafikiri inaweza kuisaida sana timu hata katika mechi za ligi na hili hata wachezaji wanalitambua na wameniahidi watapambana kulipa fadhila kwa wanachama na mashabiki wao.”

POINTI TATU

Yanga iliyocheza mechi moja katika Ligi hiyo dhidi ya Mtibwa Sugar na kuvuna pointi tatu, imesisitiza kuwa inazitaka pointi nyingine katika mechi yao Jumapili hii wakati watakapoialika Stand United ya Shinyanga.

Mabosi wa Yanga walisema baada ya kucheza mechi ya kirafiki dhidi ya African Lyon, vijana wanaendelea na mazoezi kama kawaida Uwanja wa Chuo cha Polisi Kurasini leo Jumanne, ili kuziwinda alama tatu kutoka kwa Chama la Wana.

Mratibu wa klabu hiyo, Hafidh Saleh alisema wanashukuru nyota wao waliokuwa majeruhi wamerudi uwanjani na wamsubiri Kocha Mkuu, Mwinyi Zahera arejee toka DR Congo alipoenda kwa majukumu ya timu ya taifa ya kwao ili mambo yaendelee.

Wachezaji ambao waliokuwa majeruhi, lakini wamerejea uwanjani na walicheza mechi ya Lyon ambapo Yanga ilishinda bao 1-0 ni pamoja na Heritier Makambo na Amissi Tambwe, huku Burhan Akilimali naye akiwa fiti kuelekea mchezo wa Stand.