Bocco awataka mashabiki Simba uwanjani
Dar es Salaam. Nahodha wa Simba, John Bocco amesema mwanzo wa ligi unakuwa wa ushindani wa hali ya juu na kadri siku zitakavyokuwa zinaendelea ndivyo watakavyopata ya picha ya nini wanatakiwa kufanya ili waweze kutetea ubingwa.
Bocco alisema kitendo cha kuanza na ushindi dhidi ya Prisons kimewaongezea kujiamini na kuendelea kutamani kushinda kila mechi.
"Mechi za ufunguzi timu zinakuwa zimepania, kwani zinakuwa zimetoka kwenye maandalizi, ndio maana hata mchezo wetu na Prisons, ulikuwa mgumu na waushindani mkubwa.
"Pia tunaamini tutashinda dhidi ya Mbeya City ambayo tunatarajia kucheza nayo, Jumamosi ya wiki hii, tunajipanga kwa ushindani wa hali ya juu kwani si timu ya kubeza,"alisema Bocco.
Amewaomba mashabiki wa timu hiyo kuendelea kujitolea kufika uwanjani kila wanapokuwa wanacheza akisema watafanya vitu ambavyo vitawafanya wawe wanaondoka na tabasamu.
"Kiu ya shabiki ni ushindi, nguvu yao ya kutuunga mkono itatusaidia kutupa moyo kujua tuna deni la kuwalipa pindi wanapokuwa wamefika uwanjani kuishangilia timu yao, wajitoe kwa bidii na sisi tutafanya kwa bidii katika sekta inayotuhusu," alisema Bocco.