Bocco aisubiria Mtibwa Sugar tu!

Muktasari:

Simba iliyoondoka mkoani Arusha kuelekea jijini Mwanza baada ya kucheza mechi ya kirafiki dhidi ya Arusha United na kushinda bao 2-1, wamesema kuwa kikosi kizima kilichotua Arusha ndio kitakachocheza Mwanza.

ARUSHA. Kama kuna watu wanadhani nahodha wa timu ya Simba, John Bocco bado anasumbuliwa na majeraha ya paja aliyoyapata akiwa mazoezini nchini Uturuki na kudhani atakosa mchuano mkali wa Ngao ya Hisani dhidi ya Mtibwa, basi wajue wanakosea.

Simba iliyoondoka mkoani Arusha kuelekea jijini Mwanza baada ya kucheza mechi ya kirafiki dhidi ya Arusha United na kushinda bao 2-1, wamesema kuwa kikosi kizima kilichotua Arusha ndio kitakachocheza Mwanza.

Msemaji wa Simba, Haji Manara alisema kuwa John Bocco kwa sasa ni mzima ila waliamua kwa pamoja na uongozi kumpumzisha kwa ajili ya kuvuta nguvu katika mchezo wao dhidi ya Mtibwa Sugar unaotarajiwa kufanyika katika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

“Bocco yuko poa kabisa hana shida yoyote ila tulichokifanya ni kuangalia huu mchezo wa kirafiki na hatuwezi kuingiza wachezaji wote uwanjani wakati idadi ya 11 pekee hivyo hata walioingia wanatosha na Bocco ataonekana dhidi ya Mtibwa kwa mapendekezo ya mwalimu.”

Kwa upande wake John Bocco alisema kuwa kiafya yuko mzima kabisa kikubwa katika klabu yake ni ushindani wa namba kutokana na wachezaji wote waliosajiliwa ni wazuri uwanjani hivyo mechi zinazofuata akipata namba atacheza

“Kwa sasa niko vizuri sina majeraa yoyote ila itambulike tu kuwa mimi ni mchezaji kama wachezaji wengine nawania namba kama wengine hivyo Mungu akinisaidia mechi zijazo nikipata namba nitacheza maana hayo ni maamuzi ya mwalim” alisema Bocco

Bocco aliyekuwa anasumbuliwa na majeraha ya paja na kusababisha kukosa mechi za kujipima uwezo ikiwemo dhidi ya Asante Kakonko Simba Day na Namungo ya mkoani Lindi, uongozi Wa klabu yake walisema kwa sasa amepona kabisa na atashiriki mechi zijazo.

Hata hivyo matumaini ya Bocco kupona yalionekana alivyojiunga na timu yake kwenye mazoezi na kutoa matumaini zaidi kwa wanachama wa Simba mara baada ya kumuona kwenye kikosi jijini Arusha walipokuja kucheza na timu ya Arusha United na kuongeza matamanio ya kuona kiwango chake.

Hata hivyo Bocco alizima matumaini hayo baada ya kutokuingia uwanjani kucheza hali iliyozua kelele za mashabiki waliojitokeza kushuhudia mpambano huo.