Hapo kwa Chirwa, Ajib ndiyo penyewe

Muktasari:

  • Washambuliaji hao walifunga mabao mawili yaliyoipa Yanga ushindi dhidi ya Kagera Sugar

Yanga imeweka kambi ya muda hapa Tabora ikijiandaa kuelekea Shinyanga kucheza na Stand United.

Akili ya kocha wa timu hiyo,  George Lwandamina kwenye matumizi ya Obrey Chirwa na Ibrahim Ajibu imekubalika na wakuu wake wa kazi.

Iko hivi katika mchezo uliopita dhidi ya Kagera Sugar ambao Yanga ilishinda kwa mabao 2-1 Lwandamina aliwatumia Ajib na Chirwa kama washambuliaji wa kati na wawili hao kuonyesha uwezo mkubwa wakifanya mambo mawili muhimu yanayofanana.

Chirwa ndiye aliyefunga bao la kwanza kwa timu yake lakini pasi ya bao hilo ilitengenezwa kifundi na Ajib iliyowafanya mabeki wa Kagera kupotea akitumia mguu wake wa kulia huku Chirwa naye akimalizia kwa mguu kama huo.

Ajib naye alifunga bao la pili katika kipindi cha pili kwa akili kama hiyo akipiga shuti la hesabu lililokwenda nyavu ndogo akitumia mguu wake wa kulia lakini pasi ya bao hilo ilitengenezwa na Chirwa akitumia mguu wa kulia.

Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili wa Yanga Hussien Nyika amesema; "Nimefurahishwa na safu ya ushambuliaji hii ya Chirwa na Ajib unajua hawa wote wana akili nyingi sasa nilivyoona mimi kama wataendelea kucheza pamoja watakuwa hatari zaidi. Ndicho tunachokitaka."

Yanga kesho Jumatano itashuka katika Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi kuwavaa wenyeji wao Rhino ya hapa katika mchezo wa kirafiki dhidi ya timu hiyo ya daraja la kwanza.