Huyo Bance atapita wapi?

Muktasari:

Mitaani tayari mashabiki wa Yanga wameanza kuwatania watani zao

ASIKUAMBIE mtu bwana, inapokuja ishu za michuano ya kimataifa, Simba achana nao kabisa, huwa haitanii. Juzi Jumanne imevuka hadi raundi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa kuing’oa Gendarmerie National ya Djibouti kwa jumla ya mabao 5-0. Simba ilishinda awali mabao 4-0 nyumbani kabla ya Jumanne kushinda 1-0 ugenini na sasa imeingia anga za Al Masry ya Misri.

Mitaani tayari mashabiki wa Yanga wameanza kuwatania watani zao, Simba kuwa wamekwisha kwa kukutana na Wamisri kwani  timu hiyo kuundwa na  nyota hatari akiwamo mkali wa mabao kutoka Bukinafaso, Aristide Bance aliyewahi kucheza klabu za Ulaya zikiwamo za Bundesliga.

Al Masry imetinga raundi hiyo kwa kuing’oa Green Buffaloes ya Zambia kwa jumla ya mabao 5-2, ikishinda nyumbani mabao 4-0 na kulala juzi ugenini  2-1.

Inawezekana hata mashabiki wa Simba mioyo inawadunda kwa timu yao kukutana na Al Masry, ila hawatakiwi kuwa na presha kwani, rekodi za safu ya ulinzi ya Msimbazi inatia moyo na pengine mabeki hao wanajisemea “Bance? Atapita wapi!”

Ukiacha nyota huyo mwenye asili ya Ivory Coast, Al Masry pia ina wakali wengine kama Ahmed Gomaa, Islam Siemen na Ahmed Shoukry waliotengeneza kombinesheni matata ya kikosi hicho kilichofunga mabao 22 katika Ligi Kuu yao.

Wakati wadau wa soka nchini wakimtaja Bance zaidi, takwimu zinaonyesha Gomaa ambaye ameshinda mataji mawili ya Kombe la Mataifa ya Afrika na Misri ndiye hatari zaidi kwani anakimbiza kwa mabao ndani ya klabu hiyo.

Gomaa aliyewahi kutamba na El Raja ya nchini humo ndiye kinara wa mabao wa klabu hiyo akiwa amefunga mara 11 msimu huu na kufuatiwa na Bance Siemen na Shoukry wenye mabao matano kila mmoja.

Straika huyo ni  tishio kutokana na umbile kubwa alilonalo lililojengeka kimazoezi jambo linalozua maswali kama mabeki wa Simba wenye miili ya kawaida kama Yusuf Mlipili wataweza kumkaba.

Straika huyo ana rekodi nzuri na timu ya taifa ya Bukinafaso na mbali na kuisaidia kufanya vizuri kwenye michuano ya Afrika, ameifungia mabao 21 katika mechi zote kimataifa.

Bance alianza kucheza soka la kulipwa katika klabu ya Stade d’Abidjan mwaka 2000 kabla ya kutimkia nchini Ubelgiji anakocheza Mbwana Samatta mwaka 2003 alikojiunga na Lokeren aliyoichezea kwa miaka mitatu na kuifungia mabao 27.

Staa huyo alicheza pia Ukraine, Uholanzi na kisha Ujerumani alikojiunga na FSV Mainz 05 mwaka 2008 na kuichezea kwa miaka miwili akiifungia mabao 24 katika mechi 62.

Baada ya kucheza katika nchi kadhaa za Ulaya na Arabuni, Bance alirejea Afrika 2015 na kujiunga na Chippa United ya Afrika Kusini kabla ya kutamba na Asec Mimosas ya Ivory Coast,kisha Al Masry.

SIMBA KAMILI GADO

Kwa upande mwingine, Al Masry inaonekana kuwa na kiwango cha wastani msimu huu ambapo kwenye Ligi Kuu ya Mirsi inashika nafasi ya nne ikiwa imeachwa pointi 24 na vinara Al Ahly, wakati Simba inakimbiza Ligi Kuu Bara na pointi tano mbele ya Yanga. Simba ina pointi 42 kileleni.

Kwenye mechi nane za mwisho ilizocheza, Masry imeshinda mara nne, sare mbili na kupoteza mbili, ikiwa imefunga mabao 12 na kufungwa manne.

Rekodi hiyo sio tamu kama ya Simba ambao kwenye mechi nane za mwisho imeshinda saba na kupata sare moja tu.

Simba inaonekana hatari zaidi ikifunga mabao 21 na kuruhusu mawili tu na Kocha Msaidizi, Masudi Djuma alinukuliwa kabla ya Simba kwenda Djibouti akitamba yu tayari kucheza na timu yoyote kwani ana kikosi kipana.

UKUTA WA SIMBA

Licha ya uwepo wa Bance na Gomaa ndani ya Al Masry huenda wakakutana na ugumu kutoka kwa Simba yenye ukuta mgumu.

Safu hiyo inayoongozwa na kipa Aishi Manula na mabeki Shomary Kapombe, Erasto Nyoni, Juuko Murshid na Asante Kwasi inaonekana kuwa moto na isiyofungika kirahisi, ikipewa sapoti kubwa na kiungo wa kati Jonas Mkude.

Wakali hao wametengeneza maelewano makubwa yanayoweza kuwapa shida kina Bance katika mechi ya awali itakayopigwa jijini Dar es Salaam kati ya Machi 6-8.

Simba imekuwa na chaguo pana katika eneo hilo kwani pia ina mabeki wengine Yusuf Mlipili, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Nicholas Gyan na James Kotei anayemudu pia ulinzi, wako tayari kuvaa viatu vya staa yeyote anayekosekana kwa sababu yoyote ile.