Zahera kukutana na wakongwe Yanga
Muktasari:
Alisema amewakubalia wachezaji hao lakini kikubwa alichowasisitiza ni kuwaomba wazungumzie namna watakavyoisaidia timu kutwaa ubingwa na sio kumzungumzia Kakolanya huku akiweka wazi kuwa wakizungumzia suala hilo basi mkutano utavunjika.
KOCHA Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera anatarajia kukutana na wachezaji wa zamani wa Yanga kujadili mambo mbalimbali yanayohusu timu huku akisisitiza kuwa katika mkutano huo hataki kusikia habari za kipa wake Beno Kakolanya.
Akizungumza na Mwanaspoti, Zahera alisema ni kweli kesho atakuwa na kikao na wachezaji wa zamani ambao walimpigia simu wakimuomba kuonana nae kwa ajili ya mambo mbalimbali yanayohusu timu yao na suala la Kakolanya ambaye yupo nje ya timu kwa muda.
Alisema amewakubalia wachezaji hao lakini kikubwa alichowasisitiza ni kuwaomba wazungumzie namna watakavyoisaidia timu kutwaa ubingwa na sio kumzungumzia Kakolanya huku akiweka wazi kuwa wakizungumzia suala hilo basi mkutano utavunjika.
"Kwa kila mwanachama au shabiki wa Yanga ambaye anatamani kuonana na mimi nikiwa na nafasi hawezi kupata tabu nipo tayari kukaa na viongozi, mashabiki, wanachama wa Yanga kwaajili ya kujadili masuala mbalimbali ya timu lakini siwezi kupokea magroup au watu wowote wanaotaka kuzungumza na mimi kuhusiana na ishu ya Beno,"
"Nimeulizwa mengi kwamba katika kikao changu cha kesho nitaweza kumsamehe Beno naomba nitolee ufafanuzi hili kama yatazungumzwa hayo basi icho kikao hakiwezi kuchukua ata dakika tano kitakuwa kimeisha," alisema Zahera.