Zahera aamsha mzuka Mbeya
Muktasari:
Kikosi cha Yanga ambacho ndiyo vinara kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara, tangu waanze kucheza mechi hizo ambazo ni 13, hawajapoteza hata moja zaidi ya kutoka sare mbili na ushindi mechi 13, itacheza na Tanzania Prisons siku ya Jumatatu.
Mbeya. Klabu ya Yanga, imetua jijini Mbeya leo Jumamosi tayari kwa mchezo wao na Tanzania Prisons maarufu kwa jina la Wajelajela utakaopigwa Jumatatu hii kwenye Uwanja wa Sokoine.
Kikosi hicho ambacho kilikuwa na wachezaji pamoja na benchi la ufundi likiongozwa na Kocha Mkuu Mwinyi Zahera, mara
baada kutua Uwanja wa Kimataifa wa Songwe, mashabiki na wanachama wa Yanga jiji Mbeya walijitokeza kwa uwingi kwa ajili ya kuwaunga mkono.
Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera amesema, mchezo dhidi ya Tanzania Prison si wa kubeza kutokana jinsi kikosi hicho kilivyo jiimarisha katika safu ya ulinzi.
"Tumetua salama Mbeya jukumu lililo mbele yetu ni kusaka ushindi ili tuondoke na pointi tatu. Nina kikosi kizuri na kilicho kamilika kwenye safu ya ushambuliaji. Licha ya kuwa sijaongozana na wachezaji wengine kutokana na matatizo tofauti yakiwemo majeraha tunatakiwa kushinda,"alisema Zahera.
Amefafanua wachezaji ambao hajasafiri nao Mbeya ni Mkongo Harieter Makambo na Beno Kakolanya ambao wana maumivu ya aina tofauti.
Ameongeza kwa kusema kuwa: "Tunashukuru mashabiki wetu wa Mbeya kwa mapenzi waliyotuonyesha na tunawaahidi kuwa tutawafurahisha siku hiyo ya Jumatatu tutakayokuwa uwanjani"