Tshabalala: Azam, Yanga mtupishe tunarudi kileleni

Muktasari:

Beki wa Simba, Mohamed Hussein 'Tshabalala' amewatumia salama Azam FC ambao wapo kileleni kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara kwamba wamekaa kwenye nafasi hiyo kwa muda.

Dar es Salaam. Nahodha msaidizi wa Simba, Mohamed Hussein 'Tshabalala' amesema waliokaa kileleni mwa Ligi Kuu Bara wajiandae kuwapisha wanarudi kwenye nafasi hiyo.

Tshabalala anasema kupoteza pointi saba baada ya kutoka sare mbili dhidi ya Ndanda FC na Yanga (zilipotea pointi nne) na kupoteza pointi tatu baada ya kufungwa na Mbao FC, kunawapa changamoto ya kuona kila mechi kwao fainali.

"Tunahitaji umakini wa kuhakikisha tunakokotoa pointi zote kwa mechi zilizosalia mzunguko wa kwanza, ambao una jumla ya mechi 19, naamini tukifanya hivyo tutarejea kileleni na walipo watakuwa wamekaa kwa muda.

"Ligi ni ngumu kila timu imejipanga, lakini lazima Simba tuwe na kitu cha tofauti ili kuonyesha kwamba sisi ni mabingwa watetezi na raha yake ni kuchukua mara mbili mfululizo,"anasema.

Tshabalala amezungumzia pia ushindani wa namba katika nafasi yake kwamba unampa kujituma na kutojisahau akijua akifanya uzembe basi benchi litamhuhsu.

"Simba kila namba ina ushindani mkali, hilo linanipa imani ya kutetea ubingwa kwani kila atakayepewa nafasi ya kucheza ataitumia kwa umakini akitaka kuaminiwa na kocha wetu Patrick Aussems,"anasema.