Straika Simba ashangaa usajili wa Msudan

SIMBA imesajili wachezaji wawili wa kigeni, Mbrazil Wilker Henrique da Silva ambaye ni mshambuliaji na beki Msudan Sharaf Eldin Shiboub.
Usajili huo ni mpya lakini umemshangaza mshambuliaji wa zamani wa Simba, Emmanuel Gabriel 'Batgol' ambaye amesema uongozi wa Simba unafanya usajili wake bila kufuata matakwa ya kocha Patrick Aussems.
Batgol ameonyesha kusikitishwa na madai ya kuachwa kwa kiungo Mghana, James Kotei na kusajili nyota hao ambao alidai amewafuatilia viwango vyao ni vya kawaida sana na hawastahili kucheza klabu kama Simba ambayo ina malengo makubwa.
"Unamuacha mchezaji mzuri kama Kotei, Haruna Niyonzima, Emmanuel Okwi, Deogratius Munishi 'Dida' unakwenda kusajili Wasudan na Wabrazil, wanatupeleka wapi, inashangaza na kufikirisha kidogo.
"Hata kama hawana nidhamu pengine kama ninavyosikia lakini je kazi yao si wanafanya ama hawafanyi, sidhani kama kuna haja ya kuangalia hilo wakati kazi zao wanafanya vizuri, huu usajili hasa wa wachezaji wa kigeni sikubaliani nao kabisa, ni wa mihemko na matakwa yao," anasema Bagtol
Mchezaji huyo alikwenda mbali kwa kusema; "Ukiangalia usajili wa Simba na Yanga, Yanga wanasajili vizuri kwa kufuata maelekezo ya kocha wao Mwinyi Zahera hata wakija kuchemka mzigo utamwangukia kocha wao na sio Simba.
"Wamesajili Beno Kakolanya ambaye ameachwa Yanga kwa utovu wa nidhamu, huyo ana tofauti gani na hao akina Niyonzima, Okwi na wengineo kwenye suala la nidhamu, nadhani ifike mahala Mohamed Dewji atumie vizuri pesa zake, zisiwasumbue kwa kukusanya tu wachezaji na kuanza upya kuitengeneza, hii itawasumbua na hawatafika mbali michuano ya ndani na nje," anaeleza.