Simba yaibuka kivingine Caf
Muktasari:
- Kuelekea katika mechi ya Kimataifa Simba ambao watacheza klabu bingwa Afrika dhidi ya Mbabane kocha wa kikosi hiko Patrick Aussems ameomba kucheza mechi ya kirafiki na timu kutoka nje ya Tanzania.
- Simba watacheza mechi ya kirafiki na mabingwa wa Ligi Kuu ya Malawi Big Bullets na Ijumaa ndio mchezo huo utapigwa katika uwanja wa Taifa.
MABINGWA watetezi Simba wanajiandaa kucheza mechi ya kwanza ya kimataifa ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Mbabane Swallows ya Swaziland na ili kujiweka fiti kabla ya mechi hiyo, watacheza mchezo wa kirafiki dhidi ya mabingwa wa Malawi, Big Bullets.
Simba itaanzia nyumbani kati ya Novemba 27 hadi 29 na mechi ya marudiano itakuwa Desemba mwanzoni wakati Big Bullets ambao ni mabingwa mara 12 kwenye ligi ya kwao watakwenda Nairobi kucheza na Gor Mahia.
Kocha wa Simba, Patrick Aussems ameomba kucheza mechi mbili za kimataifa za maana ambazo anaamini zitakuwa kipimo sahihi kwake kabla ya kuvaana na Mbabane ili kuona mapungufu na ubora wa kikosi.
Uongozi wa Simba haraka ulitii uamuzi huo kwa kutafuta timu ambazo zitaipa ushindani Simba na walifanikiwa kuipata Big Bullets na Aussems atatesti mitambo yake Ijumaa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mechi nyingine ambayo Simba wameomba kucheza ni dhidi ya Al Hilal ya Sudan lakini imeelezwa haina uhakika sana wa timu hiyo kucheza na Simba kwani siku ambayo walikubali kucheza mechi hiyo Simba watakuwa katika maandalizi makali ya kuwakabili Mbabane.
Mratibu wa Simba, Abbas Selemani alisema kocha aliomba mechi hizo za kirafiki zenye ushindani mkubwa ili azitumie kurekebisha kikosi chake kabla ya mechi yao na Mbabane.
“Tulifanikiwa kuwapata Big Bullets na watakuja kucheza hapa, Al Hilal tulikubaliana nao lakini sidhani kama tutacheza nao kwa sababu walitaka uchezwe kati ya Novemba 25-27 siku ambazo tutakuwa katika maandalizi ya kucheza na Mbabane.
“Wachezaji watakaotumika katika mechi hiyo ya kirafiki ni wale ambao watakuwa kambini na si wale waliokuwa kwenye majukumu ya timu zao za Taifa,” alisema Selemani.
Kwa upande wa Aussems alisema, “Wiki iliyopita tulicheza mechi na timu ya vijana ya Azam ambayo kwangu haikuwa mechi kwani niliona kama mazoezi tu, lakini hii na Big Bullets itakuwa kipimo sahihi kulingana na mazoezi ambayo tunafanya.”
“Yote hayo ni maandalizi ya kuona jinsi gani tunafikia malengo ya kufanya vizuri katika mechi za kimataifa na mashindano mengine ingawa baadhi ya wachezaji wapo timu zao za Taifa lakini naamini mambo yanazidi kwenda vizuri kuliangana na mazoezi ambayo tunafanya,” alisema Aussems.
MBURUNDI AWASHTUA SIMBA
Kocha wa Mbeya City, Mburundi Ramadhan Nsanzurwimo amewashtua Simba wametafuta timu yenye kipimo sahihi kucheza nao kwa ajili ya kujiandaa na mechi zao za Kimataifa.
Anasema ameifundisha Big Bullets kwa miaka mitano na kuwa miongoni mwa watu walioisaidia timu hiyo kufikia mafanikio hapo walipo sasa kwani ni timu yenye vijana wengi ambao wanapenda mafanikio na kushindana nyota wenye majina makubwa kama waliokuwa Simba.
“Mechi itakuwa ya ushindani kwani Big Bullets naifahamu vizuri na ina wachezaji si chini ya wanne ambao wanacheza timu yao ya Taifa kwa hiyo natazama mchezo utakuwa wa ushindani na benchi la ufundi la Simba wanapaswa kuwatumia wachezaji wote ambao wapo kwenye mipango yao,” alisema Nsanzurwimo.
MTUNISIA AKABIDHIWA TIMU
Kama ulikuwa unadhani Simba wanatania katika kuhakikisha wanafanya vizuri kwenye mashindano ya kimataifa, sahau hilo kwani nyota wa kikosi hicho wameongezewa dozi ya mazoezi chini ya Kocha wa viungo, Adel Zrane.
Iko hivi, Aussems Jumamosi aliwakabidhi wachezaji wote kwa msaidizi wake, Zrane awapigishe tizi la kufa mtu katika gym zilizopo ndani ya viwanja vya Gymkhana.
Zrane alikuwa na wachezaji hao na kuwapigisha mazoezi ya gym kwa saa mbili kuanzia saa 2:30-4:30 asubuhi na baada ya hapo walipewa mapumziko ya siku tatu na leo Jumanne wataendelea na mazoezi.
“Baada ya kutoka ratiba ya michuano hiyo tutakuwa na mechi nyingi mfululizo kwa maana hiyo wachezaji wote wanatakiwa kuwa fiti ili kutumika vizuri na haiwezekani kuwa hivyo bila kufanya mazoezi ya nguvu kama haya,” alisema Zrane.