Okwi, Kagere wote hawana uhakika mjue
Muktasari:
Kocha mkuu wa Simba Sc Patrick Aussems ameeleza katika kikosi chake hakuna mchezaji mwenye uhakika wa namba ya kudumu, bali inategemeana na mchezo wa siku hiyo pamoja na kujituma kwa mchezaji kwenye mazoezi kuelekea katika mchezi husika.
LICHA ya mashabiki mtaani kutambia majina ya Emmanuel Okwi, Meddie Kagere na John Bocco wakiamini ndio nyota wanaoibeba Simba kwa sasa, lakini Kocha Mkuu wa timu hiyo, Patrick Aussems amefichua hakuna mwenye uhakika kikosini mpaka sasa.
Mbelgiji huyo alisema, atakuwa akiwatumia au kutowatumia nyota hao ndani ya kikosi cha kwanza kulingana na aina ya pambano wanaloenda kucheza hivyo, hakuna mwenye uhakika wa namba mpaka sasa.
Bocco, aliyeanzia benchi katika pambano na mechi ya Ngao ya Hisani dhidi ya Mtibwa Sugar kumpokea Okwi kuumia na kutoka dakika ya 65, hatakuwepo kwenye mechi ya watani Jumapili hii na kuwapa mchecheto mashabiki wa Simba.
Nyota huyo amecheza mechi zote tano za Ligi Kuu akibadilishiwa Okwi na Kagere ambaye jijini Mwanza alianzia benchi na timu kulala 1-0 dhidi ya Mbao.
Okwi mwenyewe alikosa mechi za awali dhidi ya Prisons na Mbeya City kabla ya juzi dhidi ya Mwadui kuishia benchi tu.
Nyota hao watatu walicheza kwa mara ya kwanza pamoja mechi ya Ndanda kabla ya baadaye Okwi kutolewa baada ya kuumia mguu, huku Kagere nae alitoka na nafasi yake kuchukuliwa na Adam Salamba.
Lakini Kocha Aussems alisema hakuna straika mwenye uhakika wa namba katika kikosi chake cha kwanza na kwamba ataendelea kuwatumia ama kutowatumia kwa pamoja katika mchezo mmoja kulingana na mahitaji yake.
“Kama tunacheza na aina ya timu inayopenda kuzuia kama Ndanda inanilazimu kuwatumia wote watatu, lakini kama tunacheza na timu ambayo inafunguka hata wawili kati ya hao watakaoanza ni sawa,” alisema Aussems.
Simba imeshacheza mechi tano za Ligi Kuu Bara huku, Kagere na Bocco pekee ndio wakiwa wameifungia mabao matano iliyonayo ikishika nafasi ya nne na alama zao 10, tatu pungufu na vinara Mbao FC iliyocheza mechi sita.