Niyonzima mechi tano anasepa
Muktasari:
Niyonzima alisema kama benchi la ufundi la Simba litaendelea kumchomesha mahindi, basi atakuwa tayari kuvunja mkataba ili kulinda heshima anayopewa na Taifa lake la Rwanda.
WAKATI Kocha Mkuu wake, Patrick Aussems akitangaza kumpa siku 14 ili awe fiti kabla ya kuanza kumtumia, kiungo wa kimataifa wa Simba, Haruna Niyonzima alisema ana mechi tano tu ndani ya Msimbazi kabla ya kusepa zake.
Niyonzima alisema kama benchi la ufundi la Simba litaendelea kumchomesha mahindi, basi atakuwa tayari kuvunja mkataba ili kulinda heshima anayopewa na Taifa lake la Rwanda.
Akizungumza na Mwanaspoti, Niyonzima alisema haumizwi na tatizo la kukosa namba katika kikosi cha Simba kwani uwezo anao na anajiamini lakini kikubwa anachokiomba ni kumpa heshima ili kumlindia namba katika kikosi cha Amavubi.
Alisema yupo fiti na ana uwezo wa kucheza Simba, ila suala la kupangwa au kutopangwa anamuachia kocha na kuweka wazi anaheshimu mipango yake.
“Kupata kwangu nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza cha Simba kinalinda heshima pia kinaniongezea uimara kuelekea michezo yetu iliyobaki atika kuwania nafasi ya kucheza fainali za Afcon 2018,” alisema.
Niyonzima alisema anaendelea vizuri na programu ya Kocha msaidizi Masoud Djuma na anaamini siku akipata nafasi ya kuitumikia timu yake atafanya mambo makubwa yatakayorudisha wapenzi wake wenye kiu ya kumuona akicheza.